052-Atw-Twuur: Utangulizi Wa Suwrah

 

052-Atw-Twuur: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 49

 

Jina La Suwrah: Atw-Twuur

 

Suwrah imeitwa Atw-Twuur (Mlima), na yanayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Faida. Na pia kwa kutajwa mwanzo kabisa Aayah namba (1). Na Mlima huo ni ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Aliongea na Nabiy Muwsaa (عليه السّلام).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Hoja na dalili zinazopinga shubha za wanaomkadhibisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha kufufuliwa, na kubainisha mwisho mbaya wa wenye kukadhibisha, na mwisho mzuri wa Waumini.

 

3-Majibu juu ya uzushi wa washirikina na uongo wao.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1- Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) kuapia baadhi ya vitu Alivyoviumba kama vile Atw-Twuur (Mlima) na Kitabu kilichoandikwa (katika Lawh Al-Mahfuwdhw au Qur-aan), na vinginevyo vinavyodalilisha Uwezo Wake Allaah (سبحانه وتعالى) wa Uumbaji. Kisha ikafuatia jawabu la kiapo kuthibitisha kutokea Adhabu ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba hakuna wa kuizuia.

 

2-Zimetajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah, na Ahadi ya Allaah kwa wanaokadhibisha, na kubainisha mwisho wao mbaya wa kuingizwa katika moto wa Jahannam.

 

3-Zimetajwa Neema kadhaa Alizoziandaa Allaah (سبحانه وتعالى) Peponi kwa wenye kumcha Yeye Allaah (سبحانه وتعالى), na Waumini kuahidiwa kukutana na dhuriya wao pindi wote wakiendelea kuthibitika katika imaan zao. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akaendelea kutaja neema za humo Peponi na kwamba Waumini watakabiliana kukumbushana mema yao ya duniani na kumshukuru Allaah kwa kuwafadhilisha na kuokolewa na moto.

 

4-Zikafuatilia Aayah kadhaa zinazotaja Ishara na Dalili mbalimbali za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kuwaradd  washirikina shubha zao, shirki na kufru zao, na uovu wao wa kumpachika Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) sifa ovu, pamoja na kumsingizia Allaah kuwa Ana mabinti. Na hayo ni katika kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumtaka awapuuze, nao wangojee adhabu na maangamizi.

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kumliwaza tena Nabiya avute subira kwa ibaada na Dhikru-Allaah nyakati zote na katika Dhikru-Allaah hizo ni Kumsabbih na Kumhimidi Rabb.

 

Faida:

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma Suwrah Atw-Twuur katika Swalaah ya Maghrib:

 

حَدَّثَنِي إِسْحَاقُ بْنُ مَنْصُورٍ، حَدَّثَنَا عَبْدُ الرَّزَّاقِ، أَخْبَرَنَا مَعْمَرٌ، عَنِ الزُّهْرِيِّ، عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ جُبَيْرٍ، عَنْ أَبِيهِ، قَالَ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْمَغْرِبِ بِالطُّورِ، وَذَلِكَ أَوَّلَ مَا وَقَرَ الإِيمَانُ فِي قَلْبِي‏.‏

 

Amesimulia Jubayr Bin Mutw’im (رضي الله عنه): Nilimsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Suwrah Atw-Twuur katika Swalaah ya Magharibi, na hicho ndicho cha kwanza kilichopandikiza imaan moyoni mwangu. [Al-Bukhaariy]

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma Suwrah Atw-Twuur alipokuwa akiswali pembeni ya Al-Ka’bah.

 

حَدَّثَنَا إِسْمَاعِيلُ، حَدَّثَنَا مَالِكٌ، عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ نَوْفَلٍ، عَنْ عُرْوَةَ بْنِ الزُّبَيْرِ، عَنْ زَيْنَبَ بِنْتِ أَبِي سَلَمَةَ، عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ ـ رضى الله عنها ـ زَوْجِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَتْ شَكَوْتُ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنِّي أَشْتَكِي‏.‏ فَقَالَ ‏"‏ طُوفِي مِنْ وَرَاءِ النَّاسِ، وَأَنْتِ رَاكِبَةٌ ‏"‏‏.‏ فَطُفْتُ وَرَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم حِينَئِذٍ يُصَلِّي إِلَى جَنْبِ الْبَيْتِ، وَهْوَ يَقْرَأُ ‏وَالطُّورِ * وَكِتَابٍ مَسْطُورٍ

 

Amesimulia Ummu Salamah mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Nilimshtakia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu maradhi yangu, akasema, "Fanya Twawaaf huku ukiwa juu ya mnyama nyuma ya watu." Nikafanya hivyo, na kwa wakati huo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali pembeni ya Ka’bah na kusoma Suwrah Atw-Twuur. [Al-Bukhaariy]

 

 

Share