053-An-Najm: Utangulizi Wa Suwrah

 

053-An-Najm: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 62

 

Jina La Suwrah:  An-Najm

 

Suwrah imeitwa An-Najm (Nyota), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila. Na pia kwa kutajwa mwanzo kabisa Suwrah, Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuthibitisha kuwa Wahy ni kweli, na kwamba Unatoka kwa Allaah (عزّ وجلّ). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha dalili ya Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

3-Kuthibitisha ya kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni mkweli katika kile anachokifikisha kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kiapo cha Allaah (عزّ وجلّ) kuapia An-Najm (Nyota). Kisha likaja jibu la kiapo ambalo ni yaliyotajwa kuthibitisha ukweli wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutimiza amri za Wahy kutoka kwa Rabb wake, na kwamba hasemi kwa matamanio yake bali ni Wahy aliofunuliwa. Na katika hayo, ni yale yaliyotokea katika Safari ya Al-Israa Wal-Mi’raaj.

 

2-Imetajwa wasifu wa Jibriyl (عليه السّلام) kama vile kuwa ni mwaminifu wa Wahy,  na wasifu wa nguvu zake na ukomavu  wake, na muonekano wake ulio jamili, na umbile lake Alilomuumba Allaah (عزّ وجلّ) ambalo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona.

 

3-Katika yaliyotajwa ya safari ya Al-Israa wal-Mi’raaj, ni Radd ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa washirikina kwa kumtilia shaka Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu safari hiyo, na shaka yao ya kumuona Jibriyl (عليه السّلام).

 

4-Allaah (سبحانه وتعالى) Anawaradd washirikina kwa dhulma yao kubwa, ya kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Ana mabinti, na kubainisha kuwa majina ya waabudiwa wao ni majina waliyowaita wao tu, na kwamba wana dhana za hisia tu, zisizo na ukweli.

 

5-Imethibitishwa kwamba hakuna atakaeruhusika kutoa ash-shafaa’ah (uombezi) isipokuwa ambaye Allaah (سبحانه وتعالى) Atamtolea idhini na kumridhia.

 

6-Imebainishwa uadilifu wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa kuwalipa waovu kwa uovu, na kuwalipa watendaji mema kwa mema. Kisha ikabainishwa Rehma Yake Allaah (سبحانه وتعالى) ya kuwaghufuria waja. Na ikabainishwa upana wa Ilimu Yake (سبحانه وتعالى) na Kuyajua ya ghaibu; Anamjua anayepotoka na anayehidika, Anajua yanayojiri katika fuko la uzazi la mama, na Anajua yaliyomo nyoyoni mwa wanaadam. Akakataza mtu kujitukuza mwenyewe.

  

7-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) analiwazwa kuwapuuza na kujitenga na wanaokengeuka na kujiweka mbali na Ukumbusho wa Allaah na badala yake akajishughulisha na dunia na anasa zake.

 

8-Imetajwa baadhi ya radd na hoja kwa washirikina. Na ikatajwa kuwa hakuna atakayebeba dhambi za mwenziwe, na kwamba hakuna amali atakayolipwa mtu isipokuwa tu ile aliyoifanyia juhudi duniani na kuifanyia kazi, na kwamba mwisho wa mambo yote yanaishia kwa Allaah.

 

9-Ukumbusho kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu nyumati  zilizotangulia kabla yake, kwamba waliwakadhibisha Rusuli wao kama vile alivyokadhibishwa yeye na watu wake. Na yakatajwa maangamizi yao. Nao ni kina ‘Aad kaumu ya Nabiy Huwd (عليه السّلام), kina Thamuwd kaumu ya Nabiy Swaalih (عليه السّلام), kaumu ya Nuwh (عليه السّلام), na waliopinduliwa miji yao chini juu ambao ni watu wa Nabiy Luutw (عليه السّلام).

 

10-Imetajwa mshangao kuhusu washirikina wanavyoghafilika na Qur-aan na kuidharau na kuipuuza wanapoisikia na badala yake kushughulika na anasa za dunia.   

 

11-Suwrah imekhitimishwa kwa amri ya kumnyenyekea Allaah (سبحانه وتعالى) na kumwabudu na kumsujudia.   

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Suwrah An-Najm ni Suwrah ya kwanza kuteremshwa ndani yake Sijdah ya Tilaawah (Sijda inaposomwa Qur-aan).

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ أَوَّلُ سُورَةٍ أُنْزِلَتْ فِيهَا سَجْدَةٌ ‏{‏وَالنَّجْمِ‏}‏‏.‏ قَالَ فَسَجَدَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَسَجَدَ مَنْ خَلْفَهُ، إِلاَّ رَجُلاً رَأَيْتُهُ أَخَذَ كَفًّا مِنْ تُرَابٍ فَسَجَدَ عَلَيْهِ، فَرَأَيْتُهُ بَعْدَ ذَلِكَ قُتِلَ كَافِرًا، وَهْوَ أُمَيَّةُ بْنُ خَلَفٍ‏.‏

Amesimulia ‘Abdullaah (رضي الله عنه): Suwrah ya kwanza kuteremshwa ndani yake Sijdah, ni (Suwrah) An-Najm. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudu (alipoisoma), na wakasujudu waliokuwa nyuma yake, isipokuwa mtu mmoja ambaye nilimuona akichukua mchanga mkononi mwake na kusujudu juu yake. Baadaye nilimuona mtu huyo akiwa ameuliwa hali ya kuwa kafiri. Naye ni Umayyah bin Khalaf. [Al-Bukhaariy]

 

2-Watu wote walisujudu; Waislamu, washirikina na majini:

 

حَدَّثَنَا مُسَدَّدٌ، قَالَ حَدَّثَنَا عَبْدُ الْوَارِثِ، قَالَ حَدَّثَنَا أَيُّوبُ، عَنْ عِكْرِمَةَ، عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ ـ رضى الله عنهما أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم سَجَدَ بِالنَّجْمِ وَسَجَدَ مَعَهُ الْمُسْلِمُونَ وَالْمُشْرِكُونَ وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ‏.‏ وَرَوَاهُ ابْنُ طَهْمَانَ عَنْ أَيُّوبَ‏.‏

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudu alipoisoma Suwrah An-Najm (53) wakasujudu pamoja naye Waislamu, washirikina, majini na watu wote. [Al-Bukhaariy]

 

 

 

 

Share