079-An-Naazi’aat: Utangulizi Wa Suwrah

 

079-An-Naazi’aat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 46

 

Jina La Suwrah: An-Naazi’aat

 

Suwrah imeitwa An-Naazi’aat (Wanaong’oa Kwa Nguvu), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwakumbusha watu kumjua Allaah (عزّ وجلّ), na (kuijua) Siku ya Mwisho. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuweka wazi kwamba kufufuliwa ni kweli, na kutaja baadhi ya vitisho vya Qiyaamah, na kuwaradd washirikina wenye kupinga kufufuliwa, na kuwatishia na kuwaogopesha.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia Malaika wanaotoa roho za makafiri kwa mng’oo mkali kabisa. Na kwa Malaika wanaotoa roho za Waumini kwa upole kabisa. Na kwa Malaika wanaoogelea katika kuteremka kwao kutoka mbinguni na kupaa kwenda mbinguni. Na kwa Malaika wanokimbilia kutekeleza Amri za Allaah. Na kwa Malaika wanaopitisha Amri za Allaah.

 

2-Kisha ikafuatia jibu la Kiapo, nalo ni kuthibitisha  Qiyaamah, kwa kutajwa baadhi ya matukio yake, kama ardhi kutetemeka kwa mpulizo wa kwanza wa baragumu, ambao watu wote watakufa isipokuwa Awatakao Allaah. Kisha utafuatilia mpulizo wa pili wa baragumu, ambao watu watafufuliwa kutoka makaburini wakiwa katika umbo jipya. Siku hiyo nyoyo zitapapatika, na macho yatakuwa dhalili kwa vitisho watakavyoviona. 

 

3-Kisha ikabainishwa kauli za washirikina waliokuwa wakiuliza duniani, kama kweli watafufuliwa waumbwe upya, ilhali mifupa imeshasagika na kuoza makaburini. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaradd kwa kuthibitisha kuwa, tukio hilo litatokea kwa mlio mmoja tu wa kuwafisha, kisha baada ya baragumu la pili, watatahamaki wako juu ya ardhi baada ya kuwa makaburini.

 

4-Imetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) alipoitwa na Allaah katika bonde lilobarikiwa la Twuwaa, na kutumwa kwa Firawni. Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) akamwonyesha Firawni Ishara na Dalili za Allaah za miujiza, lakini alimkadhibisha na akaasi, na akawanadia watu wake wamwabudu yeye badala ya Allaah. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamwangamiza kwa adhabu ya duniani kwa kumgharikisha, na anaendelea kuadhibiwa mpaka Siku ya Qiyaamah, ambako atapata adhabu kali zaidi! Basi hayo yawe mazingatio kwa wenye kumkhofu Allaah.

 

5-Ikathibitishwa tena kufufuliwa kwa muonekano wa dalili kadhaa za Uwezo wa Allaah, wa uumbaji wa mbingu na ardhi na yaliyomo. 

 

6-Yakatajwa baadhi ya matukio ya kutisha Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo moto wa Jahannam utaonekana wazi, waingizwe humo waliopinduka mipaka na wakapendelea maisha ya dunia. Ama ambao walijizuia nafsi zao na matamanio, wakakhofu kusimamishwa mbele ya Rabb wao, basi hao makazi yao yatakuwa ni kuingizwa Jannah.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kujibu maswali ya washirikina kuhusu Qiyaamah, na kubainisha kwamba ahadi ya kutokea Siku hii, ujuzi wake uko kwa Allaah Pekee, na lilokuwa wajibu kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), ni kuwakumbusha tu hicho Qiyaamah, na kwamba pindi kitakapowajia na wakakiona, basi kana kwamba wao hawakuishi duniani isipokua sehemu tu katika mchana.

 

 

Share