078-An-Nabaa: Utangulizi Wa Suwrah

 

078-An-Nabaa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 40

 

Jina La Suwrah: An-Nabaa

 

Suwrah imeitwa An-Nabaa (Habari Muhimu), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (2).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha dalili za Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa Kufufua (viumbe), na kuwahofisha juu ya mwisho (mbaya). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibisha kufufuliwa na vitisho vyake, na kuwaonya wenye kuipinga.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuwauliza washirikina ni jambo gani wanaulizana? Na kwamba wanaulizana kuhusu habari muhimu iliyo kubwa mno nayo ni Qur-aan ambayo inatoa habari za Tawhiyd ya Allaah na mengineyo yaliyomo humo na kuhusu kufufuliwa, jambo ambalo washirikina hawakuamini. Na kisha kuwatishia kwa mafikio mabaya pindi watakapoendelea katika kufru zao za kupinga kwao yale aliyokuja nayo Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

2-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawabainishia Ishara Zake, na Dalili zenye kudhihirisha Tawhiyd Yake, na Uwezo Wake Mkubwa wa kuumba viumbe na vinginevyo, kama kuumba ardhi na mbingu na yaliyomo, pamoja na Neema Zake kadhaa Alizowajaalia viumbe waweze kuishi katika ardhi hii.   

 

3-Kisha ikatajwa Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo ni Siku ya Uamuzi kati ya viumbe, na kutajwa baadhi ya matukio yake kama kupulizwa baragumu na watu kufufuliwa makaburini, na mbingu kufunguliwa milango yake ili wateremke Malaika, na majabali kulipuliwa yakawa kama mangati.

 

4-Kisha ikatajwa Jahannam kuwa ni marejeo ya makafiri, na ikatajwa yale Aliyoyaandaa Allaah (سبحانه وتعالى) humo ya vyakula na vinywaji vya moto na usaha, kuwa ni jazaa yao humo kwa kukutoamini Siku hiyo ya kuhesabiwa, na kukadhibisha kwao Risala ya Allaah. Basi hakuna watakachopata isipokuwa kuongezewa adhabu.

 

5-Waumini wenye taqwa wamebashiriwa kufaulu na kuingizwa mabustani ya zabibu na mengineyo Aliyowaandalia Allaah humo ya Neema Zake, kama Hurulaini (wanawake wazuri wenye macho makubwa ya kupendeza), na vinywaji safi vizuri, na mengineyo, kuwa ni jazaa yao kwa kuamini kwao na matendo mema duniani.  

 

6-Imebainishwa wazi kwamba Siku ya Qiyaamah ni kweli na haina shaka, na kwamba inapasa kutanguliza matendo mema kabla ya kutokea Siku hiyo.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kuonywa adhabu iliyo karibu, na kudhihirishwa matendo ya waja, ya kheri na ya shari, na kutamani kafiri Siku hiyo lau angekua mchanga.

 

 

 

Share