102-At-Takaathur: Utangulizi Wa Suwrah
102-At-Takaathur: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 8
Jina La Suwrah: At-Takaathur
Suwrah imeitwa At-Takaathur (Kushindana Kukithirisha), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuwakumbusha wale wanaotaka kuwa na mali nyingi, na wanaofanya upuuzi hapa duniani, (kuwakumbusha) makaburi na kuhesabiwa (matendo). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Tahadharisho la kutokushindana kutafuta mali kwa wingi huku wakighafilika na Aakhirah, na ukumbusho wa kuulizwa Siku ya Qiyaamah.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
Suwrah imefunguliwa kwa kutahadharishwa watu wanaoghafilika na kutenda yanayowawajibikia ya utiifu kwa Allaah (سبحانه وتعالى), kwa kushindana kutafuta wingi wa mali na watoto na mengineyo yenye kuwasterehesha na kuwanufaisha duniani na wakajifakharisha nayo. Kushughulika kwao huko, kunaendelea mpaka yanapowafika mauti, wakazikwa makaburini. Basi humo ndimo kutakapohakiki mambo wakajuta kushughulika kushindana kwa mali na mengineyo, jambo ambalo limewafanya wasahau Aakhirah. Na watakapokuwa wanaadhibika humo kaburini, basi watatamani warudi duniani ili wajiandaalie mema ili waepukana na adhabu humo kaburini. Lakini wapi! Hakuna uwezekano wa kurudi duniani, na Allaah (سبحانه وتعالى) Anahakikisha kwamba humo kaburini, kwa yakini watauona moto wa Jahiym ambao una waka vikali mno! Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Amesisitiza tena kuwa watauona waziwazi na kwa yakini kabisa. Kisha wataulizwa kuhusu kila neema walizojaaliwa duniani, ambazo walinufaika nazo, kama walishukuru au walikufuru. Basi wataulizwa: Je, wamezipata vipi? Je, wamezitumia vipi? Je, walitimiza haki za Allaah na haki za jamaa, masikini na mafuqaraa?