103-Al-‘Aswr: Utangulizi Wa Suwrah

 

103-Al-‘Aswr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 3

 

Jina La Suwrah: Al-‘Aswr

 

Suwrah imeitwa Al-‘Aswr (Zama), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuelezea sababu za kuokoka na za kupata khasara. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha ni watu wepi watakaopata khasara, na ni wepi watu watakaofaulu.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia zama, kwa sababu ya matukio mengi yaliyojiri kwa watu waliotangulia, yakiwemo ya maajabu; waliotenda ya kheri na malipo yao, na waliotenda ya shari na adhabu zao. Kisha ikahakikishwa kiapo kwamba, binaadam yuko katika khasara na maangamizi kwa kughafilika kutii Amri za Allaah (سبحانه وتعالى). Lakini waliokhasirika si wanaadam wote, kuna watakaofaulu. Hawa ni ambao wana imaan nyoyoni mwao, wakaamini nguzo za imaan, na wakamwamini Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutii Amri Zake, na kujiepusha makatazo Yake, na wakamwamini Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na kutii amri zake na kujiepusha makatazo yake. Kisha wakatenda amali njema za kila aina; amali za kudhihirika na amali za kufichika. Na pia wakalingania (da’wah), jambo ambalo limesisitizwa mno katika Qur-aan na Sunnah; kuamrishana mema na kukatazana munkari. Kisha wakavuta subira kutokana na tabu na mashaka watakazozipata katika da’wah, wakathibitika katika Dini. Basi hawa ndio watakaosalimika na khasara na ndio watakaofaulu duniani na Aakhirah.

 

Faida:

 

Imaam Ibn Kathiyr (رحمه الله) amenukuu katika Tafsiyr yake kwamba, Al-Shaafi’iyy (رحمه الله) amesema: “Lau watu wangeitafakari Suwrah Al-‘Aswr, ingewatosheleza.” Na lilokusudiwa katika kauli yake hiyo kwamba, ingawa Suwrah hii ni fupi, lakini ina maana ya kina, ambayo inaongoza njia kamili ya maisha ya mwanaadam, na hivyo basi Suwrah inawaongoza wanaadam katika kuhimizana kushikamana na Dini ya Allaah kwa imaan, matendo mema, da’wah (kulingania Dini), na kuvuta subira katika hayo. Na hivyo basi, inamtosheleza mtu kupata mafaniko ya maisha ya dunia na Aakhirah.  

 

 

Share