106-Quraysh: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

106-Quraysh: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 4

 

Jina La Suwrah: Quraysh

 

Suwrah imeitwa Quraysh (Kabila La Quraysh), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha Neema za Allaah kwa Maquraysh, na haki Yake Allaah kwao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwakumbusha watu wa Makkah Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwao.  

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa kustaajabu mazowea ya Maquraysh, kuhusu amani waliyonayo, na kupangika kwa sahali na vizuri kabisa safari zao za kwenda Yemen katika msimu wa baridi, na safari za kwenda Sham katika msimu wa joto, kwa ajili ya biashara zao. Basi wamshukuru Rabb wao na wampwekeshe katika ibaada kwani Yeye Allaah (سبحانه وتعالى), Ndiye Aliyewaezesha hayo, na Yeye Ndiye Aliyewajaalia wawe na hadhi na heshima kubwa kwa kuwajaalia wawe wakaazi wa Makkah, mji ambao ni mtukufu kabisa, uliomo ndani yake Al-Ka’bah (Nyumba ya Allaah). Na pia wamshukuru na wampwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) kwani Yeye Ndiye Aliyewaruzuku chakula kipindi cha njaa, na Akawajaalia amani na utulivu kutokana na khofu, kwa vile Allaah Aliwaangamiza wale waliowakusudia mabaya. Basi kujaaliwa rizki na amani, ni katika neema kubwa za kidunia.

 

 

Share