107-Al-Maa’uwn: Utangulizi Wa Suwrah

 

107-Al-Maa’uwn: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa

 

Idadi Za Aayah: 7

 

Jina La Suwrah: Al-Maa’uwn

 

Suwrah imeitwa Al-Maa’uwn (Misaada Ya Matumizi Madogodogo Ya Kawaida), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha sifa za wanaoikadhibisha Dini. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kushangazwa na hali ya wenye kukadhibisha kufufuliwa na kuhesabiwa matendo, na ubaya wa matendo yao.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa mshangao kuhusu makafiri wasioamini kufufuliwa na kuhesabiwa matendo. Ikafuatia sifa zao ambazo, ni wenye kuacha kutoa haki za waja; kumdhulumu yatima kwa kumyima haki yake na kumkaripia, wala hamhurumii kutokana na ususuavu wa moyo wake, wala hakhofu kuhesabiwa kwa hili. Pia hawahimizi wengine kulisha maskini. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaahidi adhabu kali ya moto kwa wenye sifa za unafiki, ambao huswali lakini wanaghafilika na Swalaah zao; hawazisimamishi kama ipasavyo, wala hawaziswali kwa nyakati zake, bali huswali kwa riyaa-a (kujionyesha kwa watu) ili wasifike kuwa ni waswalihina. Na wanakataa kuwafanyia watu ihsaan, kwa  kuwanyima msaada wa aina yoyote ule unaokidhi haja zao za dharura, kama kutokuwaazima au kutokuwagaia vitu, ambavyo havina gharama kubwa pamoja na kuwa hawapungukiwi kitu kuviazimisha au kuvigawa, kama vile kumyima jirani vitu alivyopungukiwa katika matumizi ya jikoni, au kutokumuazima mtu vyombo au vitendea kazi, atumie kwa ajili ya vitu vilivyomharibikia nyumbani kwake.  

 

 

 

Share