108-Al-Kawthar: Utangulizi Wa Suwrah

 

108-Al-Kawthar: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.

 

Idadi Za Aayah: 3

 

Jina La Suwrah: Al-Kawthar

 

Suwrah imeitwa Al-Kawthar (Mto Wenye Kheri Nyingi), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Fadhila na pia kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha Neema za Allaah kwa Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ambazo ni kheri nyingi na kumtetea. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumbashiria Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Neema ya Mto wa Al-Kawthar Siku ya Qiyaamah na kumliwaza.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa kumkumbusha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kheri nyingi alizojaaliwa duniani na Aakhirah. Miongoni mwa kheri za Aakhirah ni kumjaalia mto (Al-Kawthar) ambao pambizo zake ni mahema ya lulu na mchanga wake ni miski. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamwamrisha Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) Amtakase kwa ibaada na achinje mnyama kwa ajili Yake Pekee pamoja na kutaja Jina la Allaah. Suwrah ikakhitimishwa kwa kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kumbainishia kwamba, mgomvi wake anayemchukia kwa sababu ya kubalighisha Risala ya Allaah, ndiye atakayekatiwa kila kheri. Rejea Sababun-Nuzuwl (Sababu ya Kuteremka) Suwrah hii tukufu.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Bishara Kwa Waumini Watakaoshikamana Na Sunnah Wataruhusiwa Kunywa Kinywaji Katika Hodhi Lenye Maji Kutoka Mto Wa Al-Kawthar:

 

‘Ulamaa wametaja kuwa Al-Kawthar ni mto katika Jannah, nao ni katika kheri na fadhila nyingi mno atakazopewa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Siku ya Qiyaamah. Mto huo una tawi lake ambalo ni hodhi litakalozungukwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), Swahaba na Waumini waliothibitika katika Manhaj sahihi, nao watakunywa hapo na hawatapata kiu tena milele. Ama waliozua mambo katika Dini (bidaa), hao watatengwa wasibakie hapo katika Al-Hawdhw. Simulizi kadhaa zimethibiti na miongoni mwazo ni Hadiyth hii:

 

عَنْ أَنَسٍ، قَالَ: بَيْنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ذَاتَ يَوْمٍ بَيْنَ أَظْهُرِنَا إِذْ أَغْفَى إِغْفَاءَةً ثُمَّ رَفَعَ رَأْسَهُ مُتَبَسِّمًا فَقُلْنَا: مَا أَضْحَكَكَ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟  قَالَ: ((أُنْزِلَتْ عَلَىَّ آنِفًا سُورَةٌ ))‏. فَقَرَأَ: (( بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ * فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ * إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الأَبْتَرُ)).‏ ثُمَّ قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْكَوْثَرُ؟)). فَقُلْنَا اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ.‏ قَالَ: ((فَإِنَّهُ نَهْرٌ وَعَدَنِيهِ رَبِّي عَزَّ وَجَلَّ عَلَيْهِ خَيْرٌ كَثِيرٌ هُوَ حَوْضٌ تَرِدُ عَلَيْهِ أُمَّتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ آنِيَتُهُ عَدَدُ النُّجُومِ فَيُخْتَلَجُ الْعَبْدُ مِنْهُمْ فَأَقُولُ رَبِّ إِنَّهُ مِنْ أُمَّتِي‏.‏ فَيَقُولُ مَا تَدْرِي مَا أَحْدَثَتْ بَعْدَكَ))‏.‏ زَادَ ابْنُ حُجْرٍ فِي حَدِيثِهِ بَيْنَ أَظْهُرِنَا فِي الْمَسْجِدِ‏.‏ وَقَالَ:‏ ((مَا أَحْدَثَ بَعْدَكَ))‏.

 

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Siku moja Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa pamoja nasi akawa amepitiwa na lepe la usingizi kisha akanyanyua kichwa chake juu huku akitabasamu, tukasema: Ni kitu gani kimekufurahisha ee Rasuli wa Allaah? Akasema: “Imeniteremkia sasa hivi Suwrah: (Akaisoma Suwrah Al-Kawthar).

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ * فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ * إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الأَبْتَرُ *

Hakika Sisi Tumekupa (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Al-Kawthar (Mto katika Jannah). Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja.  Hakika mbaya wako, yeye ndiye atakayekatiliwa mbali (kizazi na kila kheri).”  [Al-Kawthar: (108)]  

 

Kisha akasema: “Je, mnajua ni nini Al-Kawthar?” Tukajibu: Allaah na Rasuli Wake Ndio Wajuao zaidi. Akasema: “Huo ni mto ambao Allaah (عزّ وجلّ) Ameniahidi. Una kheri nyingi sana, nao una hodhi lake ambalo Ummah wangu watakusudia kulifikia Siku ya Qiyaamah. Vyombo vyake (au bilauri) ni idadi ya nyota. Mja miongoni mwao atatolewa mbali atengwe. Nitasema: Ee Rabb! Hakika yeye ni katika Ummah wangu!  Allaah Atasema: Hujui nini alizusha baada yako!”

 

Ibn Hujri amezidisha katika Hadiyth yake: Alikuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amekaa kitako pamoja nasi Msikitini. Na (Allaah) Atasema: “Hujui walichokizusha baada yako!” [Muslim – Kitaab Asw-Swalaah - Mlango wa hoja anayesema kuwa Al-Basmalah ni Aayah katika kila mwanzo wa Suwrah isipokuwa Suwrah Al-Baraa (At-Tawbah)] 

 

 

   

Share