04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Kunyoa Kinena Na Kunyofoa Nywele Za Kwapa Ni Katika Sunnah Za Maumbile Asilia (Fitwrah)
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo
الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ
Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu
04-Kunyoa Kinena Na Kunyofoa Nywele Za Kwapa Ni Katika Sunnah Za Maumbile Asilia (Fitwrah):
Kinena ni sehemu inayounganisha mapaja na fumbatio, na ndipo zinapoota nywele pembezoni mwa utupu. Inapendeza kwa mwanamke ajijengee mazoea ya kunyoa nywele za kinena na kwapa, kwani hilo ni katika Sunan za maumbile asilia zinazopendeza azifanye.
Ni karaha kwa mwanamke na hata kwa mwanaume kuziachia nywele za sehemu hiyo kumea hadi kuwa refu, kwa kuwa kufanya hivyo, kutatoa nafasi ya kukusanyika uchafu na kuwa chanzo cha harufu mbaya itakayomkimbiza mke na mume.
Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ameelekeza nywele hizi zisiachwe kwa zaidi ya siku 40. Anas amesema:
"وُقِّتَ لَنَا فِي قَصِّ الشَّارِبِ وَتَقْلِيمِ الْأَظْفَارِ وَنَتْفِ الْإِبِطِ وَحَلْقِ الْعَانَةِ أَنْ لَا تُتْرَكَ أَكثر من أَرْبَعِينَ لَيْلَة"
“Tumewekewa muda wa kukata sharubu, kukata kucha, kunyofoa nywele za kwapa na kunyoa kinena, kwamba zisiachwe kwa zaidi ya siku 40”. [Muslim(258), Abu Daawuwd (420), At-Tirmidhiy (2759), An-Nasaaiy (1/15) na Ibn Maajah (295)]