03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Hairuhusiwi Kuunganisha Nywele Asili Na Za Bandia (Kuvaa Wigi)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

03-Hairuhusiwi Kuunganisha Nywele Asili Na Za Bandia (Kuvaa Wigi):

 

 

Asmaa (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema: 

 

"لَعَنَ اللَّهُ الْوَاصِلَةَ وَالْمُسْتَوْصِلَةَ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani msusi wa kuunganisha nywele bandia na mwenye kutaka kuunganishiwa”.  [Al-Bukhaariy (5936) na Muslim (2122)]

Kuvaa wigi kunaingia pia ndani ya duara la uharamu hata kama mwanamke ana tatizo la kukatika nywele zake.  Na hii ni kwa riwaayah nyingine ya Asmaa (Radhwiya Allaah ‘anhaa):

 

"أَنَّ امْرَأَةً جَاءَتْ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  فَقَالَتْ: إِنِّي أَنْكَحْتُ ابْنَتِي، ثُمَّ أَصَابَهَا شَكْوَى فَتَمَرَّقَ رَأْسُهَا، وَزَوْجُهَا يَسْتَحِثُّنِي بِهَا، أَفَأَصِلُ رَأْسَهَا؟ فَسَبَّ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  الْوَاصِلَةَ وَالْمُسْتَوْصِلَةَ‏"

 

“Kwamba mwanamke mmoja alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:  Mimi nimemwoza binti yangu, kisha amepatwa na ugonjwa wa kunyonyoka nywele, na mumewe amenishikilia nimtafutie namna.  Je, naweza kumuunganishia nywele bandia?  Hapo hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamlaani muunganishaji na anayetaka kuunganishiwa  nywele bandia.  [Al-Bukhaariy 5935) na Muslim (2122)]

 

Na imesimuliwa pia kwamba Mu’aawiyah bin Abu Sufyaan alichukua furushi la nywele lililokuwa mkononi mwa mmoja wa walinzi wake akasema: 

 

"أَيْنَ عُلَمَاؤُكُمْ؟ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  يَنْهَى عَنْ مِثْلِ هَذِهِ وَيَقُولُ: "‏إِنَّمَا هَلَكَتْ بَنُو إِسْرَائِيلَ حِينَ اتَّخَذَتْ هَذِهِ نِسَاؤُهُمْ"‏‏

 

“Wako wapi ‘Ulamaa wenu?  Mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikataza mfano wa hii akisema:  “Hakika waliangamia Baniy Israaiyl wanawake wao walipoanza kutumia hili”.  [Al-Bukhaariy (5933) na Muslim (2127)]

 

Kiufupi, mwanamke haruhusiwi kuunganisha nywele zake na nywele zingine au kuvaa wigi, ni sawasawa iwe kwa ajili ya mumewe au kwa mwingine, kwa kuwa ni haramu.

 

Je, Inafaa Kuunganisha Nywele Kwa Nyuzi Za Hariri Au Sufi Na Mfano Wa Hivi Ambavyo Si Nywele?

 

Kauli yenye nguvu kati ya kauli mbili za ‘Ulamaa inasema kwamba inaruhusiwa mwanamke kuunganisha nywele zake kwa nyuzi za hariri, au za sufi, au za kitambaa ambazo hazifanani na nywele. Kutumia hizi hakuzingatiwi kama kuunganisha, na wala hakuingii ndani ya maana kusudiwa ya kuunganisha, bali ni kujipamba na kujiremba.  Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.  [An-Nawawiy ameinukulu toka kwa Al-Qaadhwiy ‘Ayyaadh.  Ahmad bin Hanbal amepondokea kwenye kauli hii]

 

 

Share