18-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Wanawake Walioharamika Kwa Muda: iii-Mke Wa Mtu, Au Mwanamke Ambaye Bado Yuko Kwenye Eda Isipokuwa Mateka, Na Mke Wa Kafiri Akisilimu
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
18-Wanawake Walioharamika Kwa Muda: 3-Mke Wa Mtu, Au Mwanamke Ambaye Bado Yuko Kwenye Eda Isipokuwa Mateka, Na Mke Wa Kafiri Akisilimu:
Hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ"
“Na (mmeharamishiwa pia) wanawake walio katika ndoa isipokuwa iliyowamiliki mikono yenu ya kuume”. [An-Nisaa: 24]
Maana ya aayah hii ni kwamba mmeharamishiwa wanawake walioolewa isipokuwa wale iliyowamiliki mikono yenu ya kiume kwa kuwateka vitani. Mwanamke akitekwa vitani, ndoa yake na mumewe kafiri inavunjika, na atakuwa halali kwa Waumini unapomalizika muda wa kujua kama ana kitu tumboni au la (istibraa), nayo ni hedhi moja. Maana hii inazatitiwa na Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriyy:
"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ حُنَيْنٍ بَعَثَ جَيْشًا إِلَى أَوْطَاسٍ فَلَقُوا عَدُوًّا فَقَاتَلُوهُمْ فَظَهَرُوا عَلَيْهِمْ وَأَصَابُوا لَهُمْ سَبَايَا، فَكَأَنَّ نَاسًا مِنْ أَصْحَابِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ تَحَرَّجُوا مِنْ غِشْيَانِهِنَّ مِنْ أَجْلِ أَزْوَاجِهِنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ تَعَالَى فِي ذَلِكَ: وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ النِّسَاء إِلَّا مَا ملكت أَيْمَانكُم، أَيْ فَهُنَّ لَهُمْ حَلَالٌ إِذَا انْقَضَتْ عِدَّتُهُنَّ"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituma jeshi Siku ya Hunayn kwenda Awtwaas. Na huko walikutana na maadui wakapambana nao, wakawashinda nguvu na wakawateka wanawake wao. Ikawa kama vile Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanaona ukakasi kuwaingilia kwa sababu ya waume zao washirikina. Na hapo Allaah ‘Azza wa Jalla Akateremsha Kauli Yake:
"وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ"
“Na (mmeharamishiwa pia) wanawake walio katika ndoa isipokuwa iliyowamiliki mikono yenu ya kuume”. [An-Nisaa: 24]
Yaani, wanawake hao ni halali kwenu zinapomalizika eda zao. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1456), Abu Daawuwd (2155), An-Nasaaiy (6/110) na At-Tirmidhiy (1132)]
Ibn ‘Abbaas amesema:
"كُلُّ ذاتِ زَوْجٍ إِتْيَانُهَا زِنَا إِلاّ ما سُبِيَتْ"
“Kumuingilia mwanamke yeyote mwenye mume ni zinaa isipokuwa aliyetekwa”. [Isnaad yake ni swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Jariyr katika Tafsiyr yake (8961)].
Naye Ibn Mas-‘uwd amesema kuhusiana na aayah hii:
كُلُّ ذَاتِ زَوْجٍ عَلَيْكَ حَرَامٌ إِلاَّ أَنْ تَشْتَرِيَهَا أَوْ مَا مَلَكَتْ يَمِيْنُكَ"
“Mwanamke yeyote mwenye mume ni haramu kwako isipokuwa kama utamnunua, au aliyemilikiwa na mkono wako wa kuume (kijakazi)”. [Wapokezi wake wanaaminika. Imekharijiwa na Ibn Jariyj (8972), isipokuwa riwaayah ya Ibraahiym aliyoipokea toka kwa Ibn Mas-‘uwd imekatika]
Mwanamke ambaye mume wake alikuwa kafiri kisha akasilimu, huyu anaingia ndani ya duara la wanawake walioolewa, kwa kuwa kusilimu kwake kunamtenganisha yeye na mume wake mushrik. Na hii ni kwa Neno Lake Allaah Ta’aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا جَاءَكُمُ الْمُؤْمِنَاتُ مُهَاجِرَاتٍ فَامْتَحِنُوهُنَّ ۖ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِهِنَّ ۖ فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَاتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى الْكُفَّارِ ۖ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ ۖ وَآتُوهُم مَّا أَنفَقُوا ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَن تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ ۚ وَلَا تُمْسِكُوا بِعِصَمِ الْكَوَافِرِ وَاسْأَلُوا مَا أَنفَقْتُمْ وَلْيَسْأَلُوا مَا أَنفَقُوا ۚ ذَٰلِكُمْ حُكْمُ اللَّـهِ ۖ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ"
“Enyi walioamini! Wanapokujieni Waumini wa kike waliohajiri basi wajaribuni. Allaah Ni Mjuzi zaidi wa iymaan zao. Kisha mkiwatambua kuwa ni Waumini, basi msiwarejeshe kwa makafiri. Wao si wake halaal kwao, na wala wao waume hawahalaliki kwao. Na wapeni (makafiri mahari) waliyotoa. Na wala si dhambi kufunga nao nikaah mkiwapa mahari yao. Na wala msiwaweke wanawake makafiri katika fungamano la ndoa. Na takeni mlichotoa (katika mahari), nao watake walichotoa. Hiyo ndio Hukumu ya Allaah, Anahukumu baina yenu. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Mumtahinah: 10]