28-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Ndoa Ambazo Ni Batili Kisharia: Ndoa Ya Mhalalishaji
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الأَنْكِحَةُ الفَاسِدَةُ شَرْعًا
Ndoa Ambazo Ni Batili Kisharia
28: Ndoa Ya Mhalalishaji:
Mhalalishaji ni mtu ambaye anamwoa mwanamke aliyeachwa talaka tatu, halafu anamtaliki ili aweze kuhalalika kwa mume wa awali. Allaah Ameiharamisha ndoa hii, ndoa hii ni katika madhambi makubwa, na Allaah Amemlaani mtekelezaji (mwenye kuoa kuhalalisha) na mwenye kutekelezewa (mume wa awali).
1- Ibn Mas-‘uwd amesema:
"لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمُحِلَّ وَالْمُحَلَّلَ لَهُ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwenye kuoa kwa lengo la kuhalalisha ndoa (baada ya talaka tatu) na mwenye kuhalalishiwa”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1120), An-Nasaaiy (6/149), na Ahmad (1/448)]
‘Ulamaa wote wakiwemo Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Al-Layth, Ath-Thawriy, Ibn Al-Mubaarak na wengineo, wanasema kwamba ndoa hii ya mtu kumwoa mwanamke aliyeachwa talaka tatu ili ahalalike kwa mtalaka wake ni batili. Ni kauli pia ya ‘Umar bin Al-Khattwaab, mwanae ‘Abdullaah, na ‘Uthmaan bin ‘Affaan katika Maswahaba. [Bidaayatul Mujtahid (2/102), Al-Mughniy (6/645), Nihaayatul Muhtaaj (6/282), Al-Muhallaa (10/180), Sunan At-Tirmidhiy (3/420) na Rawdhwat At-Twaalibiyna (7/126)]
2- ‘Umar bin Al-Khattwaab amesema:
"لا أُوتَى بِمُحَلِّلٍ وَبِمُحَلَّلَةٍ إِلاّ رَجَمْتُهُمَا"
“Siletewi aliyeoa ili kuhalalisha ndoa ya talaka tatu wala aliyeolewa kwa lengo hilo ila huwapa adhabu ya kupopolewa kwa mawe”. [Isnaad yake ni swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdulrazzaaq (6/265) na Sa’iyd bin Manswuwr (1992)]
3- Ibn ‘Umar aliulizwa kuhusu mwanamke (aliyeachwa talaka tatu) kuhalalishiwa mumewe aliyemtaliki akajibu: “Hilo ni uchafu na zinaa”. [Isnaad yake ni swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdulrazzaaq katika Al-Muswannaf (10776)]
Hapa ni mamoja ikiwa atashurutishwa amtaliki mwanamke huyo ili ahalalike kwa mumewe wa kwanza, au asishurutishwe lakini akanuwia kuhalalisha, ndoa itakuwa batili tu.
4- Toka kwa Naafi’i:
"جاءَ رجلٌ إلى ابنِ عمرَ فسألَهُ عن رجلٍ طلَّقَ امرأتَهُ ثلاثًا فتزوَّجَها أخٌ لَهُ من غيرِ مُؤامرةٍ منهُ ليُحلَّها لأخيهِ، هل تحلُّ للأوَّلِ؟ فقالَ: لا إلَّا نِكاحَ رَغبةٍ كنَّا نعدُّ هذا سِفاحًا على عَهْدِ رسولِ اللَّهِ صلَّى اللَّهُ عليهِ وسلَّمَ"
“Mtu mmoja alikuja kwa Ibn ‘Umar na kumuuliza kuhusu mtu ambaye amemtaliki mkewe talaka tatu, kisha nduguye akamwoa bila wenyewe kupanga hilo ili aje kuhalalika kwa nduguye, je atahalalika kwa wa kwanza? Akasema: Hapana, isipokuwa kama itakuwa ni ndoa ya utashi wa kuendelea kuishi naye muda mrefu (kama atampendeza). Tulikuwa tunalizingatia hili wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni zinaa”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Haakim (2/199) na Al-Bayhaqiy (7/208)]
Faida:
Linaloangaliwa katika kutofaa ndoa hii ni niya ya mume wa pili (mhalalishaji), na huyu hakosi moja ya hali mbili:
Ya kwanza: Anuwie kumwoa mwanamke kisha amtaliki ili ahalalike kwa mume wake wa kwanza, ni sawa akiwa ameshurutishwa hilo au la, hapa ndoa itakuwa haifai, na itakuwa ni yenye kulaaniwa.
Ya pili: Ashurutishwe kumtaliki mwanamke kabla ya kufunga naye ndoa, kisha yeye akanuwia kinyume na alivyoshurutishwa, yaani akakusudia kuishi na mwanamke huyo maisha yake yote, hapa ndoa inakuwa ni sahihi, kwa kuwa nia ya kuhalalisha na sharti lake havipo. [Ibn ‘Aabidiyna (3/411) na Rawdhwat At-Twaalibiyna (7/126)]
Niya Ya Mume Wa Awali Na Ya Mwanamke Mwenyewe Haizingatiwi:
Kwa sababu mume wa kwanza hana tena lake jambo katika kufungwa ndoa hiyo au kuvunjwa, yeye ni mtu wa kando (ajnabi) kama walivyo wengine wa kando. Hali kadhalika kwa mwanamke, kwa kuwa mamlaka ya talaka na kuendelea na ndoa yako kwa mume wa pili, na si kwake. Kati ya yanayotilia nguvu hili ni:
"جَاءَتِ امْرَأَةُ رِفَاعَةَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَتْ: إِنَّ رِفَاعَةَ طَلَّقَنِي فَأَبَتَّ طَلاَقِي، وَإِنِّي تَزَوَّجْتُ بَعْدَهُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ الزَّبِيرِ وَمَا مَعَهُ إِلاَّ مِثْلُ هُدْبَةِ الثَّوْبِ. فَضَحِكَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَقَالَ: "لَعَلَّكِ تُرِيدِينَ أَنْ تَرْجِعِي إِلَى رِفَاعَةَ، لاَ، حَتَّى يَذُوقَ عُسَيْلَتَكِ وَتَذُوقِي عُسَيْلَتَهُ"
“Mke wa Rifaa’at alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika Rifaa’at amenitaliki talaka zote tatu. Nami baada ya kuniacha, nimeolewa na ‘Abdulrahmaan bin Az-Zubayr ambaye hana ila mfano wa ncha ya nguo (uume wake dhaifu sana). Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akacheka na kumwambia: Inaonyesha unataka kurudi kwa Rifaa’at. Hapana huwezi kurudi, mpaka (‘Abdulrahmaan) aonje utamu wako na wewe uonje utamu wake (yaani akuingilie)]. [Al-Bukhaariy (2639) na Muslim (1433)]
Hapa Rasuli hakuizingatia niya yake.