29-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Ndoa Ambazo Ni Batili Kisharia: Ndoa Ya Mut’a
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الأَنْكِحَةُ الفَاسِدَةُ شَرْعًا
Ndoa Ambazo Ni Batili Kisharia
29: Ndoa Ya Mut’a:
Hii ni ndoa ambayo mtu anamwoa mwanamke kwa muda maalum, ni sawa ikiwa siku moja au mbili au zaidi, kwa kumpa mwanamke chochote kama fedha na mfano wake (kama mahari).
Katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndoa hii ilikuwa ni halali, kisha Allaah Ta’aalaa Aliifuta kupitia kwa ulimi wa Rasuli Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye akaiharamisha uharamu wa milele mpaka Siku ya Qiyaamah. Huu ndio msimamo wa Jumhuwr ya ‘Ulamaa kuanzia kwa Maswahaba, Maimamu waliofuatia baada yao na wengineo. [Al-Mudawwanah (2/196), Bidaayatul Mujtahid (2/101), Nihaayatul Muhtaaj (5/71) na Al-Mabsuwtw (5/152)].
Taarifa zimetofautiana kuhusiana na wakati ambapo ndoa hii ya Mut’a ilifutwa. Kati yake ambazo ni sahihi ni:
1- Ilifutwa Khaybar:
Imepokewa kwa njia sahihi kwamba ‘Aliy alimwambia Ibn ‘Abbaas:
"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنِ الْمُتْعَةِ وَعَنْ لُحُومِ الْحُمُرِ يَوْمَ خَيْبَرَ "
“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza (ndoa ya) mut-‘a na nyama ya punda wa mjini walipokuwa Khaybar”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (5115) na Muslim (1407)]
Kisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliruhusu mut-’a baada ya hapo, lakini habari ya ruksa hiyo haikumfikia ‘Aliy, na yeye akabaki na Hadiyth ya kuharamisha aliyoisikia toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Khaybar. [Fat-hul Baariy (9/168)]
2- Ilifutwa Mwaka Wa Ufunguzi Wa Makkah:
Imepokelewa toka kwa Ar-Rabiy’i bin Saburata kwamba baba yake alishiriki vita pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Ukombozi wa Makkah. Amesema: Tukakaa hapo usiku na michana 30 (wiki mbili), na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaturuhusu ndoa ya mut-‘a. Kwa ruksa hiyo, mimi nikaoa msichana kwa ndoa hiyo, na sikuwahi kutoka ila Rasuli akawa ameshaiharamisha”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1406)]
Na katika tamko jingine:
"فَكُنَّ مَعَنَا [يَعْنِي النِّسَاءُ اللاتِيْ اسْتَمْتَعُوا بِهِنَّ] ثَلاثًا ثُمَّ أَمَرَنَا رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِفِرَاقِهِنَّ"
“Wakawa pamoja nasi (yaani wanawake waliowaoa kwa mut-‘a) kwa siku tatu, kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuamuru tuwaache”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1406) na Al-Bayhaqiy (7/202)]
Na katika tamko jingine:
"أَمَرَنَا رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِالمُتْعَةِ عَامَ الفَتْحِ حِيْنَ دَخَلْنَا مَكَّةَ ثُمَّ لَمْ نَخْرُجْ مِنْهأ حَتَّى نَهَانَا عَنْهَا"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru tuoe mut-‘a mwaka wa ukombozi tulipoingia Makkah, kisha hatukutoka humo, ila akawa ameshatuharamishia”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1406)]
3- Ilifutwa Mwaka Wa Awtwaas:
Toka kwa Salamah bin Al-Akwaa:
"رَخَّصَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَامَ أَوْطَاسٍ فِي الْمُتْعَةِ ثَلَاثًا ثُمَّ نَهَى عَنْهَا"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliruhusu mut-‘a Mwaka wa Awtwaas siku tatu, kisha akaipiga marufuku”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1405), Al-Bayhaqiy (7/204) na Ibn Hibaan (1451)]
Kisha marufuku hii ikawa ya milele hadi Siku ya Qiyaamah.
Zindushi Mbili:
1- Jaabir bin ‘Abdullaah amesema:
"كُنَّا نَسْتَمْتِعُ بِالْقُبْضَةِ مِنَ التَّمْرِ وَالدَّقِيقِ الأَيَّامَ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأَبِي بَكْرٍ حَتَّى نَهَى عَنْهُ عُمَرُ فِي شَأْنِ عَمْرِو بْنِ حُرَيْثٍ"
“Tulikuwa tunaoa mut-‘a kwa mahari ya konzi ya tende na unga kwa masiku kadhaa wakati wa uhai wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr mpaka alipoikataza ‘Umar kutokana na ndoa ya ‘Amri bin Hurayth”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1405) na Abu Daawuwd (2110)]
Hili linajengewa uwezekano wa kuwa waliofunga ndoa za mut-‘a katika enzi hiyo ya Abu Bakr na ‘Umar, walikuwa hawajapata habari ya kufutwa na kuharamishwa ndoa hii. [Sharhu Ma’aaniy Al-Aathaar (3/27) na Sharhu Muslim (3/555)]
2- Imethibiti toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) ya kwamba yeye alikuwa anaona uhalali wa ndoa ya mut-‘a kama iko dharura. Toka kwa Abu Hamzah:
"سَمِعْتُ ابْنَ عَبَّاسٍ، سُئِلَ عَنْ مُتْعَةِ النِّسَاءِ، فَرَخَّصَ فَقَالَ لَهُ مَوْلًى لَهُ إِنَّمَا ذَلِكَ فِي الْحَالِ الشَّدِيدِ وَفِي النِّسَاءِ قِلَّةٌ أَوْ نَحْوَهُ. فَقَالَ ابْنُ عَبَّاسٍ نَعَمْ."
“Nilimsikia Ibn ‘Abbaas akiulizwa kuhusu ndoa ya mut-‘a, naye akaruhusu. Mwachwa huru wake akauliza: Je, hiyo ni katika hali ya mtu kuzidiwa sana (na matamanio), au wanawake kuwa wachache au mfano wake? Ibn ‘Abbaas akajibu: Na’am”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5116), At-Twahaawiy (3/26) na Al-Bayhaqiy (7/204)]
Jibu hili ni katika misimamo nadra ya kipekee ya Mwanachuoni huyu mkubwa Ibn ‘Abbaas, na Allaah bila shaka Atamlipa kwa ijtihadi yake hii. Ama sisi, bila shaka tutaendelea kushikamana na taarifa iliyotufikia toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba ndoa hii ni haramu. Na Ibn ‘Abbaas kwenda kinyume na Jumhuwr ya Maswahaba hakuziharibu dalili za kuharamisha, na sisi pia hatuna udhuru wowote wa kutozitumia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Nini Afanye Aliyeoa Ndoa Ya Mut-‘a?
Tumeshasema kwamba ndoa ya mut-‘a haifai, ni batili. Hivyo basi, atakayefunga ndoa hii, ni lazima aachane mara moja na mwanamke aliyemwoa, kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamuru waliooa ndoa ya mut-‘a watengane na wanawake waliowaoa kama ilivyo katika Hadiyth ya Sabrah.
Nini Hukmu Ya Mwanaume Anayeoa Mwanamke Akiwa Na Niya Ya Kumwacha Baada Ya Muda?
Jambo hili wanalifanya wanaume wengi wanaosafiri kwenda nje. Huko wanaoa wakiwa na niya ya kuwaacha wake zao wakati wa kurejea makwao unapowadia. ‘Ulamaa wote wanasema kwamba ndoa hii ni sahihi ikiwa atamwoa bila sharti (la muda) hata kama niya yake ni kumwacha baada ya muda. Wanasema kwamba mtu huyo anaweza kweli kunuwia hivyo lakini asije kufanya, au asinuwie kitu lakini akaja kukifanya.
Al-Awzaa’iy amekwenda kinyume nao. Anasema hiyo ni ndoa ya mut-‘a. Pia ni chaguo la Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn. [Al-Istidhkaar (16/301)]
Huenda kauli hii ya Al-Awzaaiy ikawa na mantiki zaidi. Na inatiliwa nguvu na kauli ya Ibn ‘Umar iliyogusiwa nyuma kidogo alipoulizwa kuhusu mtu ambaye alitaka kumwoa mke wa nduguye ili amhalalishie, naye akasema: “Hapana, isipokuwa kama itakuwa ni ndoa ya utashi wa kuendelea kuishi naye (kama atampendeza). Tulikuwa tunalizingatia hili wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni zinaa na uchafu”.
Kuongezea na hilo, aina hii ya ndoa inakuwa na ghushi na udanganyifu ndani yake, inazalisha uadui na chuki, inaondosha kuaminiana kati ya Waislamu, inaitweza nafsi na kuitosa ndani ya dimbwi la matamanio, mbali na uharibifu mkubwa unaozalikana. Na kwa matatizo haya, ndoa hii inastahiki kuwa batili.