04-Malaika: Maana Ya Kuwaamini Malaika
Malaika
04: Maana Ya Kuwaamini Malaika
Kuamini Malaika kunakusanya mambo manne:
1- Kuamini kwamba wapo kwa iymaan ya kukata isiyo na chembe ya shaka.
2- Kuamini majina yao kama tunavyoyasikia kama Jibriyl (‘Alayhis Salaam). Ama wale ambao hatuwajui majina, hao tunawaamini wote kiujumla.
3- Kuamini sifa zao tunazozisikia za kimaumbile na za kitabia.
4- Kuamini kazi zao tunazozisikia.
Haafidh Al-Hakamiy akiielezea nguzo ya pili ya iymaan anasema: “Ni kuamini Malaika ambao wao ni Waja wa Allaah waliotukuzwa. Malaika hawa ni mabalozi kati ya Allaah na Mitume Wake (‘Alayhimus Swalaat was Salaam), wametukuka kimaumbile na kitabia, ni wema waliotwaharika kidhati, kisifa, na kivitendo, wanamtii Allaah ‘Azza wa Jalla bila kuasi, nao ni waja kati ya Waja wa Allaah. Allaah Amewaumba kwa nuru kwa ajili ya kumfanyia Yeye ibada, si mabanati wa Allaah ‘Azza wa Jalla wala watoto wa kiume, wala si washirika pamoja Naye, wala hawako sawa Naye. Allaah Yuko mbali kabisa na wanayodai madhalimu, wapingaji na wasioamini uwepo Wake”.