06-Malaika: Malaika Jibriyl

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

06:  Malaika Jibriyl

 

 

Allaah ‘Azza wa Jalla Amelitaja jina lake katika aayah tatu kwenye Qur-aan Tukufu.

 

1-  Neno Lake ‘Azza wa Jalla:

 

"قُلْ مَن كَانَ عَدُوًّا لِّجِبْرِيلَ فَإِنَّهُ نَزَّلَهُ عَلَىٰ قَلْبِكَ بِإِذْنِ اللَّـهِ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ "

 

“Sema:  Yeyote aliyekuwa adui wa Jibriyl, basi hakika yeye ameiteremsha Qur-aan katika moyo wako (ee Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Idhini ya Allaah inayosadikisha yaliyo kabla yake, na mwongozo na bishara kwa Waumini”.  [Al-Baqarah: (97)].

 

2-  Neno Lake Allaah Ta’aalaa:

 

 "مَن كَانَ عَدُوًّا لِّلَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ فَإِنَّ اللَّـهَ عَدُوٌّ لِّلْكَافِرِينَ"

 

“Yeyote aliyekuwa adui wa Allaah na Malaika Wake, na Rusuli Wake, na Jibriyl, na Miykaala, basi hakika Allaah Ni adui kwa makafiri”.  [Al-Baqarah: (98)].

 

3-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"إِنْ تَتُوبَا إِلَى اللَّـهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا ۖ وَإِن تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ"

 

Ikiwa nyinyi wawili mtatubia kwa Allaah basi ni kheri kwenu), kwani kwa hakika nyoyo zenu zimeelemea (kwa yanayomchukiza Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم). Na mkisaidiana dhidi yake, basi hakika Allaah Ndiye Mlinzi Msaidizi wake na Jibriyl na Waumini wema, na zaidi ya hayo, Malaika pia watasaidia”.   [At-Tahriym: (04)].

 

Ama katika Hadiyth:

 

4-  Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema:

 

"كَانَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم أَجْوَدَ النَّاسِ بِالْخَيْرِ، وَكَانَ أَجْوَدَ مَا يَكُونُ فِي شَهْرِ رَمَضَانَ، حَتَّى يَنْسَلِخَ، فَيَأْتِيهِ جِبْرِيلُ، فَيَعْرِضُ عَلَيْهِ الْقُرْآنَ، فَإِذَا لَقِيَهُ جِبْرِيلُ كَانَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم، أَجْوَدَ بِالْخَيْرِ مِنَ الرِّيحِ الْمُرْسَلَةِ‏"‏

 

“Rasuli wa Allaah alikuwa ni mtoaji zaidi kuliko wote kwa mambo ya kheri, na  alikuwa mtoaji kupita mpaka anapokuwa katika Mwezi wa Ramadhaan mpaka unapomalizika, na hapo Jibriyl humjia akamsomesha Qur-aan. Na Jibriyl anapokutana naye, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa ni mtoaji zaidi wa mambo ya kheri kuliko upepo Alioutuma Allaah (kuleta mvua na baraka).  [Al-Bukhaariy (06) na Muslim (2308)]

 

5-  Bibi ‘Aaishah amesema:

 

"كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا قَامَ مِنَ اللَّيْلِ افْتَتَحَ صَلَاتَهُ فَقَالَ: اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَائِيلَ وَإِسْرَافِيلَ ، فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ، عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ"

 

“Alikuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposimama usiku, anaifungua swalah yake kwa kusema:  “Ee Allaah! Mola wa Jibriyl, Miykaaiyl, na Israafiyl, Muumba wa mbingu na ardhi, Unayejua yaliyofichikana na yenye kuonekana..”  [Muslim (628). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].

 

Jibriyl (‘Alayhis Salaam) ndiye Malaika aliyekurubishwa zaidi kwa Allaah kuliko Malaika wengine.  Ni Malaika mwenye nguvu kubwa mno.  Aliinyanyua miji ya kaumu Luwt kwa ubawa wake, kisha akawapindulia juu chini.  Pia ana nguvu za kutekeleza yote anayoamrishwa, hakuna linalomshinda, na Malaika wote wa mbinguni wanamtii kwa yale anayowaamrisha toka kwa Allaah Ta’aalaa.

 

 

Share