08-Malaika: Israafiyl na Maalik
Malaika
08: Israafiyl na Maalik
Malaika Israafiyl pia ametajwa kwenye Hadiyth ya Bibi ‘Aaishah:
"كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا قَامَ مِنَ اللَّيْلِ افْتَتَحَ صَلَاتَهُ فَقَالَ: اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَائِيلَ وَإِسْرَافِيلَ ، فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ، عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ"
“Alikuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposimama usiku, anaifungua swalah yake kwa kusema: “Ee Allaah! Mola wa Jibriyl, Miykaaiyl, na Israafiyl, Muumba wa mbingu na ardhi, Unayejua yaliyofichikana na yenye kuonekana..” [Muslim (628). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].
Ibn Al-Qayyim amesema: “Malaika au viongozi wakuu wa Malaika ni watatu: Jibriyl, Miykaaiyl na Israafiyl. Na imetangaa baina ya wanachuoni wengi kwamba Israafiyl ndiye atakayepuliza baragumu Siku ya Qiyaamah. Na baadhi yao wamenukuu ijmaa juu ya hilo, lakini hilo halijathibiti kwa khabari sahihi toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au toka kwa Allaah Ta’alaa.
Wengine wamesema pia kuwa Israafiyl ni mmoja kati ya Malaika wanaobeba Arshi ya Allaah, lakini hili pia halikuthibiti kwa khabari sahihi.
Ama Maalik, Allaah Ta’aalaa Amemzungumzia Akisema:
"وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ ۖ قَالَ إِنَّكُم مَّاكِثُونَ"
“Na wataita: Ee Maalik (Mlinzi wa moto)! Na Atumalize Rabb wako tufe. Atasema: Hakika nyinyi ni wenye kubakia kuishi humo”. [Az-Zukhruf: 77].
Maalik ndiye mlinzi na msimamizi wa moto wa Jahannam. Toka kwa Samurah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"رَأَيْتُ اللَّيْلَةَ رَجُلَيْنِ أَتَيَانِي قَالاَ الَّذِي يُوقِدُ النَّارَ مَالِكٌ خَازِنُ النَّارِ، وَأَنَا جِبْرِيلُ، وَهَذَا مِيكَائِيلُ"
“Niliwaona (kwenye njozi) usiku wanaume wawili wamenijia. Mmoja wao akaniambia: Anayewasha moto ni Maalik, naye ndiye mlinzi wa moto, na mimi ni Jibriyl, na huyu ni Miykaaiyl”. [Swahiyh Al-Bukhaariy: (3236)].