10-Malaika: Haaruwta na Maaruwta
Malaika
10: Haaruwta na Maaruwta
Hawa ni Malaika wawili walioteremshwa ardhini kama fitnah na majaribio kwa watu toka kwa Allaah Ta’alaa.
Allaah Ta’aalaa Anasema:
"وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ"
“Na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwta na Maaruwta. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru”. [Al-Baqarah: 102]
Waliteremshwa katika mji wa Baabil nchini Iraki, na Allaah Akawapa ruksa ya kuwafundisha watu uchawi kama mtihani kwao, nao walikuwa hawamfundishi mtu ila baada ya kumuusia na kumtahadharisha kwamba asijifundishe fani hiyo, kwani ni ukafiri. Sababu ni kuwa kuwa mtu akishaujua uchawi, bila shaka atakuja kuutumia kudhuru watu bila sababu kutokana na ushawishi wa shaytwaan, au kuutumia katika mambo yasiyo na faida. Hivyo, baadhi ya watu hao walijifundisha fani ya kumtenganisha mtu na mkewe na kuvunja ndoa za watu ambazo Allaah Amejengea ndani yake mapenzi na mahaba kati ya mke na mume.
Na hii ni dalili inayothibitisha kwamba uchawi upo, na wachawi wapo, na kazi yao ni kudhuru watu.