11-Malaika: Malakul Mawt (Malaika Wa Kutoa Roho)

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

11:  Malakul Mawt (Malaika Wa Kutoa Roho)

 

 

Katika baadhi ya aathaar, Malaika mtoa roho (Malakul Mawt) ametajwa kama ‘Izraaiyl, lakini jina hili halijathibitishwa, si katika Qur-aan wala katika Sunnah.

 

Ibn Kathiyr amesema:  “Malakul Mawt jina lake halijatajwa katika Qur-aan wala katika Hadiyth zilizo swahiyh, lakini ametajwa katika baadhi ya aathaar kama ni ‘Izraaiyl, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Sheikh Bin Baaz (Allaah Amrehemu) aliulizwa kama katika Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) limethibiti jina la ‘Izraaiyl kama ni Malaika mtoa roho?  Naye alijibu akisema:  Sijui chochote kilichothibiti kuhusiana na hili, lakini lililotangaa baina ya Wanazuoni ni kuwa jina lake ni ‘Izraaiyl, lakini mimi sijui Hadiyth yoyote iliyo sahihi kwamba jina lake ni hilo, bali limetajwa kwenye aathaar dhaifu ambazo hazifai kuwa ni hoja”.

 

Ama Al-Albaaniy, yeye kasema:  “Malakul Mawt ndio jina lake lililotajwa ndani ya Qur-aan Tukufu.  Ama kumuita ‘Izraaiyl kama ilivyotangaa kwa watu, hilo halina asili, bali limechukuliwa toka kwenye Israaiyliyyaat (Hadiyth na riwaayah za kutunga toka kwenye Taurati na Injili”.

 

‘Abdulrahmaan Al-Barraak amesema:  “Jina hili la ‘Izraaiyl ni mashuhuri lakini halikuthibiti, bali majina ya Malaika yaliyothibiti ni Jibriyl, Miykaaiyl, Israafiyl, Maalik mlinzi wa moto, pia Munkar na Nakiyr, nao ni Malaika wawili wanaomuuliza maswali maiti kaburini”.

 

Malakul Mawt ametajwa katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ

 

Sema:  Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa”.  [As-Sajdah: 11].

 

 

Share