20-Malaika: Malaika Wenye Sura Na Maumbo Ya Kutisha: (3)- Munkar Na Nakiyr
Malaika
20: Malaika Wenye Sura Na Maumbo Ya Kutisha
(3)- Munkar Na Nakiyr
Hawa ni Malaika wawili wanaomwadhibu na kumtahini maiti kaburini, na ndio wanaomuuliza Mola wake nani, dini yake ipi, na nani Nabiy wake? Na hii ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا قُبِرَ الْمَيِّتُ -أوْ قَالَ: أحَدُكُمْ- أَتَاهُ مَلَكَانِ أَسْوَدَانِ أَزْرَقَانِ، يُقَالُ لَأحَدِهِمَا الْمُنْكَرُ وَالآخَرُ النَّكِيرُ، فَيَقُولَانِ: مَا كُنْتَ تَقُولُ في هَذَا الرَّجُلِ؟ فَيَقُولُ مَا كَانَ يَقُولُ: هُوَ عَبْدُ اللَّهِ وَرَسُولُهُ، أَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَأنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، فَيَقُولَانِ: قَدْ كُنَّا نَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُولُ هَذَا... وَإِنْ كَانَ مُنَافِقًا قَالَ: سَمِعْتُ النَّاسَ يَقُولُونَ فَقُلْتُ مِثْلَهُ، لَا أَدْرِى، فَيَقُولَانِ: قَدْ كُنَّا نَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُولُ ذَلِك"
“Maiti anapotiwa kaburini -au alisema: Mmoja wenu- humjia Malaika wawili weusi wenye macho ya kibuluu. Mmoja wao anaitwa Munkar na mwingine Nakiyr, na watamuuliza: Ulikuwa unasema nini kuhusu mtu huyu? Naye atasema yale aliyokuwa anasema: Yeye ni Mja wa Allaah na Mjumbe Wake. Ninashuhudia kwamba hakuna mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mja Wake na Mjumbe Wake. Malaika watamwambia: Sisi kwa hakika tulikuwa tunajua kwamba wewe utayasema haya. Na kama maiti ni mnafiki, atasema: Nilikuwa nawasikia tu watu wakisema, nami nikasema mfano wake, sijui. Watamwambia: Sisi kwa hakika tulikuwa tunajua kwamba wewe utasema hivyo”. [Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1071) na Ibn Hibaan (3117)].
Kama walivyoelezewa na Hadiyth hii, Malaika hawa Munkar na Nakiyr ambao wanatusubiri tukishazikwa tu, ni weusi wenye macho ya kibuluu. Bila shaka ni mwonekano wa kutisha mno, na hasa tukizingatia kuwa mtu ndio mara yake ya kwanza kukutana nao, akiwa katika mazingira mapya kabisa, na akiwa peke yake baada ya nduguze kuondoka. Ni hali ngumu kwa kweli ambao wengi haiwatikisi hata mshipa wa roho!. Lakini, watakutana nayo tu, na hapo ndipo patakuwa majuto ya kosa lisiloweza kusahihishika!
Ibn Al-‘Arabiy amesema: “Kila anayewaona atasisimkwa vibaya na mwili kutokana na mwonekano wao wa kutisha, sura mbaya na maneno yao makali pamoja na marungu makubwa waliyoyakamata yenye kuzidi kuleta hofu na fazaiko kwa maiti”.
Ibn Al-Malik Ar-Ruwmiy Al-Hanafiy amesema: “Kuja kwao kwa picha hii, ni kuwatia kiwewe makafiri wachanganyikiwe wasiweze kujibu maswali watakayoulizwa”.