25-Malaika: Malaika Hawachoki Wala Hawahisi Tabu
Malaika
25: Malaika Hawachoki Wala Hawahisi Tabu
Malaika wanamwabudu Allaah na kutii Amri Zake bila kuchoka wala kuhisi uzito, hawapati mchoko au kuhisi tabu kama anavyohisi mwanadamu. Allaah Ta’aalaa Anasema:
"فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا فَالَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ يُسَبِّحُونَ لَهُ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُمْ لَا يَسْأَمُونَ"
“Lakini wakitakabari, basi wale (Malaika) walio kwa Rabb wako wanamsabbih usiku na mchana, nao hawachoki”. [Fusswilat: 38]
As-Sa’adiyy akielezea sifa za Malaika amesema: “Allaah Amewasifu kwa sifa zilizokamilika, nao wana nguvu kamili za kumwabudu Allaah na utashi mkubwa kabisa wa kufanya hilo. Wanamsabbih Allaah usiku na mchana na wala hawachoki, hawana kibri cha kukataa kumwabudu, bali wanaliona hilo kuwa ni katika neema kubwa kwao, hawamwasi Allaah kwa Alilowaamrisha na wanafanya wanayoamuriwa”.
As-Suyuwtwiy amesema: “Niliulizwa zamani kuhusu Malaika, je wanalala?” Nikajibu kwamba sikuona nukuu yoyote inayogusia hilo, lakini inavyoonyesha ni kuwa hawalali kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:
"يُسَبِحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ"
“Wanamsabbih usiku na mchana, nao hawachoki”.