37-Malaika: Malaika Wamejipanga Vizuri Katika Mambo Yao Yote

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

37:  Malaika Wamejipanga Vizuri Katika Mambo Yao Yote

 

Malaika wanatekeleza majukumu yao wakiwa wamejipanga vyema.  Malaika hawa watakuja Siku ya Qiyaamah wakiwa wamejipanga safu kwa safu zilizonyooka barabara.  Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا"

 

Na Atakapokuja Rabb wako pamoja na Malaika walio safusafu”.  [Al-Fajr: 22]

 

Wanapofanya ibada, pia vile vile hunyoosha safu zao bila kuacha hata mwanya kidogo.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

" أَلاَ تَصُفُّونَ كَمَا تَصُفُّ الْمَلاَئِكَةُ عِنْدَ رَبِّهِمْ؟‏ قَالُوا: وَكَيْفَ تَصُفُّ الْمَلاَئِكَةُ عِنْدَ رَبِّهِمْ؟ قَالَ: ‏ يُتِمُّونَ الصَّفَّ الأَوَّلَ ثُمَّ يَتَرَاصُّونَ فِي الصَّفِّ"

 

“Kwa nini msipange safu kama wanavyopanga safu Malaika kwa Mola wao? Tukasema:  Ee Rasuli wa Allaah, vipi Malaika wanapanga safu kwa Mola wao? Akasema:  Wanakamilisha safu baada ya safu, na wanajipanga vizuri bila kuacha pengo katika safu”.   [Swahiyh Ibn Maajah (818)]

 

Na Siku ya Qiyaamah, Jibriyl (‘alayhis salaam) pamoja na Malaika wengine watasimama mbele ya Allaah kwa unyenyekevu na heshima ya hali ya juu kabisa wakiwa katika safu zilizonyooka barabara.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"يَوْمَ يَقُومُ الرُّوحُ وَالْمَلَائِكَةُ صَفًّاۖ لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابًا"

 

Siku atakayosimama Ruwh (Jibriyl) na Malaika safusafu.  Hatozungumza isipokuwa yule ambaye Ar-Rahmaan Amempa idhini na atasema yaliyo sahihi”. [‘Amma: 38]

 

Mbali ya hivyo, Malaika wako makini sana katika utendaji wao wa kazi na katika kutekeleza maagizo ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa.  Toka kwa Anas (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"آتِي بَابَ الْجَنَّةِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَأَسْتَفْتِحُ، فَيَقُولُ الْخَازِنُ : مَنْ أَنْتَ؟  فَأَقُولُ مُحَمَّدٌ ‏.‏ فَيَقُولُ : بِكَ أُمِرْتُ لاَ أَفْتَحُ لأَحَدٍ قَبْلَكَ"

 

“Nitaujia mlango wa Pepo kisha nitabisha. Mlinzi wake atauliza:  Ni nani wewe? Nitajibu:  Muhammad. Atasema:  Ni kwako tu nimeamuriwa, simfungulii yeyote kabla yako”.  [Muslim: 197]

 

 

Share