38-Malaika: Kazi Za Malaika: (1)- Jibriyl (‘alayhis salaam): Kumteremshia Qur-aan Tukufu Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Malaika
38: Kazi Za Malaika
(1)- Jibriyl (‘alayhis salaam): Kumteremshia Qur-aan Tukufu Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Huyu anajulikana kama “Ar Ruwhul Amiyn” au “Ruwhul Qudus”. Allaah Ta’alaa Anasema:
"وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ ● نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ ● عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ ● بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ"
“Na hakika hii (Qur-aan) ni Uteremsho wa Rabb wa walimwengu ● Ameiteremsha Ar-Ruwh (Jibriyl) mwaminifu ● Juu ya moyo wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ili uwe miongoni mwa waonyaji.● Kwa lugha ya Kiarabu bayana”. [Ash-Shu’araa: 192-195]
"قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ لِيُثَبِّتَ الَّذِينَ آمَنُوا وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ"
“Sema: Ameiteremsha Ruwhul-Qudus (Jibriyl) kutoka kwa Rabb wako kwa haki ili iwathibitishe wale walioamini, na ni mwongozo na bishara kwa Waislamu”. [An-Nahl: 102)]
Ibn ‘Atwiyyah amesema: “Allaah Ta’aalaa Amemwamuru Mtume Wake aeleze kwamba Qur-aan hii kwa aayaat zake zenye kufuta na zenye kufutwa, kwa hakika Aliyeiteremsha ni Jibriyl (‘Alayhis Salaam), naye ndiye Ruwhul Qudus, na hakuna mvutano wowote kuhusu hili”.
Na Allaah Ta’alaa Ameendelea kusema:
"إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ●عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ● ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ"
“Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa ● Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi ● Mwenye muonekano jamili, muruwa na nguvu na kisha akalingamana sawasawa”. [An-Najm: 4-6]
Na Anasema tena:
"إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ● ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ ● مُّطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ"
“Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli (ameifikisha) Mjumbe mtukufu (Jibriyl) ● Mwenye nguvu na cheo kitukufu kwa (Allaah) Anayemiliki ‘Arsh ● Anayetiiwa (na Malaika), mwaminifu huko (mbinguni)”. [At-Takwiyr: 19-21]
Ibn Al-Qayyim amesema: “Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Amemsifu kwa sifa njema kabisa mja Wake Jibriyl katika Qur-aan. Amemweleza kama ni Mjumbe Wake, anaheshimika heshima kubwa Kwake, ana nguvu na hadhi kubwa mbele Yake, anatiiwa na kusikilizwa huko mbinguni, na yeye ndiye mbeba dhamana ya wahyi”.
Ibn Kathiyr naye kasema: “Neno Lake: “Ni kauli ya Mjumbe Mtukufu (Jibriyl)” lina maana: Hakika Qur-aan hii imefikishwa na Mjumbe mwenye heshima kubwa, naye ni Malaika mwenye umbo zuri na mwonekano wa kupendeza, na Malaika huyu ni Jibriyl (‘alayhis salaam).
Hizi ndizo baadhi ya sifa za Malaika Jibriyl (‘alayhis salaam) kama Alivyosifiwa na Allaah Ta’aalaa pamoja na jukumu lake la kumteremshia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Qur-aan Tukufu. Na hapa kuna Jibriyl Mtukufu anayeiteremsha Qur-aan, kuna Rasuli Mtukufu (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Qur-aan Tukufu. Ni utukufu juu ya utukufu.
Mbali na kumteremshia Rasuli Qur-aan, Jibriyl (‘alayhis salaam) alikuwa akiteremka kuja kwa Rasuli kwa ajili ya kujibu maswali ya waulizaji, kumsomesha Rasuli Qur-aan na hususan katika Mwezi wa Ramadhaan, na mengineyo.
Toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba:
"سَمِعَ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَلاَمٍ، بِقُدُومِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَهْوَ فِي أَرْضٍ يَخْتَرِفُ، فَأَتَى النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ إِنِّي سَائِلُكَ عَنْ ثَلاَثٍ لاَ يَعْلَمُهُنَّ إِلاَّ نَبِيٌّ فَمَا أَوَّلُ أَشْرَاطِ السَّاعَةِ وَمَا أَوَّلُ طَعَامِ أَهْلِ الْجَنَّةِ وَمَا يَنْزِعُ الْوَلَدُ إِلَى أَبِيهِ أَوْ إِلَى أُمِّهِ قَالَ " أَخْبَرَنِي بِهِنَّ جِبْرِيلُ آنِفًا".
“Kwamba Abdullaah bin Salaam alisikia kwamba Rasuli wa Allaah ((Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yuko njiani anakuja Madiynah, na yeye alikuwa shambani kwake akivuna matunda. Akamwendea Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (baada ya kuwasili) akamwambia: Nitakuuliza maswali matatu ambayo hajui majibu yake yeyote isipokuwa Nabiy. Ni ipi alama ya kwanza ya Qiyaamah? Ni kipi chakula cha kwanza cha watu wa Peponi? Kipi kinachosababisha mtoto kufanana na baba yake au mama yake? Rasuli akamwambia: Jibriyl amenieleza majibu ya hayo muda si mrefu uliopita”. [Al-Bukhaariy: (3329)]
Abu Dharri Al-Ghiffaariy (Radhwiya Allaah ‘anhu):
" أَتَانِي جِبْرِيلُ - عَلَيْهِ السَّلاَمُ - فَبَشَّرَنِي أَنَّهُ مَنْ مَاتَ مِنْ أُمَّتِكَ لاَ يُشْرِكُ بِاللَّهِ شَيْئًا دَخَلَ الْجَنَّةَ. قُلْتُ: وَإِنْ زَنَى وَإِنْ سَرَقَ . قَالَ : وَإِنْ زَنَى وَإِنْ سَرَقَ"
Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Jibrily alinijia na kunipa habari ya kufurahisha kwamba yeyote katika umma wako atakayekufa hali ya kuwa hamshirikishi Allaah na chochote ataingia Peponi. Nikamuuliza: Na hata kama ameiba, na hata kama amezini!. Akasema: Hata kama ameiba, hata kama amezini”. [Al-Bukhaariy (1237) na Muslim (94)]