41-Malaika: Kazi Za Malaika: (4)- Malaika Wabebao ‘Arshi

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

41:   Kazi Za Malaika

 

(4)- Malaika Wabebao ‘Arshi

 

Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ"

 

(Malaika) ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih  na kumhimidi Rabbi wao, na wanamwamini, na wanawaombea maghfirah wale walioamini (wakisema):  Rabb wetu!  Umekienea kila kitu kwa rahmah na ujuzi, basi Waghufurie wale waliotubu, na wakafuata njia Yako, na Wakinge na adhabu ya moto uwakao vikali mno”.  [Ghaafir: 07]

 

Malaika hao mbali na kubeba ‘Arshi, Allaah Amewapa kazi nyingine ya kutuombea maghfirah kwa Allaah, Allaah Atukinge na adhabu ya Moto, Allaah Atuingize Pepo za kudumu pamoja na wazazi wetu, wake zetu na dhuria zetu walo wema na Atukinge na maovu na misukosuko ya Siku ya Qiyaamah.  Allaah Anasema:

 

 

 

"رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدتَّهُمْ وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ •  "وَقِهِمُ السَّيِّئَاتِ ۚ وَمَن تَقِ السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ"

 

Rabb wetu!  Waingize Jannaat za kudumu milele ambazo Umewaahidi, pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao, na wake zao, na dhuria wao.  Hakika Wewe Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote   Na Wakinge na maovu, kwani Unayemkinga na maovu Siku hiyo, basi kwa yakini Umemrehemu. Na huko ndiko kufuzu adhimu”.  [Ghaafir: 8-9]

 

 

Amesema tena:

 

"وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا ۚ وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ"

 

Na Malaika watakuwa pembezoni mwake, na watabeba ‘Arsh ya Rabb wako juu yao siku hiyo (Malaika) wanane”.  [Al-Haaqqah: 17]

 

Toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أُذِنَ لِي أَنْ أُحَدِّثَ عَنْ مَلَكٍ مِنْ مَلاَئِكَةِ اللَّهِ مِنْ حَمَلَةِ الْعَرْشِ إِنَّ مَا بَيْنَ شَحْمَةِ أُذُنِهِ إِلَى عَاتِقِهِ مَسِيرَةُ سَبْعِمِائَةِ عَامٍ"

 

“Nimepewa ruksa nimzungumzie Malaika miongoni mwa Malaika wa Allaah Ta’aalaa katika wanaobeba ‘Arshi.  Kati ya ndewe ya sikio lake hadi kwenye bega lake ni mwendo wa miaka 700”.  [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4727), na tamshi ni lake, At-Twabaraaniy (4421), na Al-Bayhaqiy (846).  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Sunan Abiy Daawuwd (4727)]

 

Mwendo huo ni wa spidi ya farasi au ndege kama walivyosema baadhi ya ‘Ulamaa.  Ikiwa kutoka kwenye ndewe ya sikio hadi kwenye bega ni safari ya miaka 700, je kiwiliwili chake kizima toka juu hadi chini utakuwa ni mwendo wa miaka mingapi?!  Ukubwa huu hawezi kiumbe yoyote kuujua isipokuwa Muumbaji Mwenyewe Allaah Aliyetukuka.  Hao pengine ndio viumbe wa pili kwa ukubwa baada ya ‘Arshi ya Allaah Ta’aalaa.  Sasa Aliyewaumba hao, Atakuwaje?  Tumwogopeni sana Allaah.

 

 

Share