42-Malaika: Kazi Za Malaika: (5)- Malaika Wa Milima
Malaika
42: Kazi Za Malaika
(5)- Malaika Wa Milima
Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
"هَلْ أَتَى عَلَيْكَ يَوْمٌ كَانَ أَشَدَّ مِنْ يَوْمِ أُحُدٍ؟ قَالَ: لَقَدْ لَقِيتُ مِنْ قَوْمِكِ مَا لَقِيتُ، وَكَانَ أَشَدُّ مَا لَقِيتُ مِنْهُمْ يَوْمَ الْعَقَبَةِ، إِذْ عَرَضْتُ نَفْسِي عَلَى ابْنِ عَبْدِ يَالِيلَ بْنِ عَبْدِ كُلاَلٍ، فَلَمْ يُجِبْنِي إِلَى مَا أَرَدْتُ، فَانْطَلَقْتُ وَأَنَا مَهْمُومٌ عَلَى وَجْهِي، فَلَمْ أَسْتَفِقْ إِلاَّ وَأَنَا بِقَرْنِ الثَّعَالِبِ، فَرَفَعْتُ رَأْسِي، فَإِذَا أَنَا بِسَحَابَةٍ قَدْ أَظَلَّتْنِي، فَنَظَرْتُ فَإِذَا فِيهَا جِبْرِيلُ فَنَادَانِي فَقَالَ إِنَّ اللَّهَ قَدْ سَمِعَ قَوْلَ قَوْمِكَ لَكَ وَمَا رَدُّوا عَلَيْكَ، وَقَدْ بَعَثَ إِلَيْكَ مَلَكَ الْجِبَالِ لِتَأْمُرَهُ بِمَا شِئْتَ فِيهِمْ، فَنَادَانِي مَلَكُ الْجِبَالِ، فَسَلَّمَ عَلَىَّ ثُمَّ قَالَ يَا مُحَمَّدُ، فَقَالَ ذَلِكَ فِيمَا شِئْتَ، إِنْ شِئْتَ أَنْ أُطْبِقَ عَلَيْهِمِ الأَخْشَبَيْنِ، فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم بَلْ أَرْجُو أَنْ يُخْرِجَ اللَّهُ مِنْ أَصْلاَبِهِمْ مَنْ يَعْبُدُ اللَّهَ وَحْدَهُ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا".
“Ee Rasuli wa Allaah! Je uliwahi kukutana na siku ngumu zaidi kuliko Siku ya Vita vya Uhud? Rasuli akasema: Hakika nimepata mateso mengi na adha nyingi sana toka kwa watu wako (Maquraysh). Lakini siku ngumu zaidi niliyopambana nayo toka kwao ilikuwa siku ya ‘Aqabah. Ni pale nilipojitambulisha kwa Ibn ‘Abdi Yaaliyla bin ‘Abdi Kulaal lakini hakunijibu matakwa yangu. Nikaondoka na huzuni kubwa mno, na sikuzindukana ila baada ya kufika Qarn Ath-Tha’aalib. Nikanyanyua kichwa changu na kushtukizwa kuona wingu limenifunika kwa kivuli chake. Nikaliangalia na tahamaki nikamwona Jibriyl ndani yake. Akaniita na kuniambia: Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Amesikia waliyokwambia watu wako, na majibu waliyokupa, na Yeye Amekutumia Malaika wa milima ili umwamuru lolote ulitakalo. Malaika wa milima akaniita na kunisalimia, kisha akasema: Ee Muhammad! Hakika Allaah Amesikia maneno waliyokwambia watu wako, na mimi ndiye Malaika wa milima, na Mola wako Amenituma kwako ili uniamuru lolote utakalo kwa watu hao. Ukitaka nitawafudikiza kwa milima miwili, basi nitawafudikiza. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Bali ninatumai Allaah Atatoa toka kwenye migongo yao watakaomwabudu Allaah Peke Yake na hawatamshirikisha na chochote”. [Swahiyhul Bukhaariy (3231)]
Siku hii ni pale Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoelekea Taif kulingania Uislamu baada ya kufariki ami yake Abu Twaalib na mkewe Bi Khadiyjah. Akaelekea moja kwa moja kwa viongozi watatu wa kabila la Thaqiyf lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyeitikia wito wake wa kuingia katika Uislamu au hata kumpa ahadi yoyote au usalama. Akakuta mambo ambayo hakuyatarajia kabisa ya kuchezwa shere, kukanushwa, kupingwa na kuzuiwa asifanye lolote kuhusu Uislamu. Lakini pia wakamsumbua na wakawatuma watoto na vijana wahuni, wakampopoa kwa mawe mpaka akatota damu hadi miguuni. Akatoka Taif kurudi Makkah akiwa amegubikwa ghamu na huzuni kubwa kutokana na uzito wa hayo yaliyomkuta mpaka alipofika Qarn Ath-Tha’aalib, ndipo hapo alipozindukana. Haya ndiyo yaliyomkuta Rasuli katika kuifikisha Dini kwetu, lakini sisi hatuioni thamani yake!
Ibn ‘Uthaymiyn amesema: “Tunaamini kwamba Malaika wana kazi walizopewa, na miongoni mwao ni Malaika wa milima”.