44-Malaika: Kazi Za Malaika: (7)- Malaika Wa Kumlinda Mwanadamu Na Hatari
Malaika
44: Kazi Za Malaika
(7)- Malaika Wa Kumlinda Mwanadamu Na Hatari
Malaika wenye kazi ya kumlinda mtu akiwa mjini kwake au safarini, akiwa macho au usingizini, na katika hali zake zote wanajulikana kama “Al-Mu’aqqibaatu”. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ"
“Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa Amri ya Allaah”. [Ar-Ra’ad: 11]
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema kuhusiana na Malaika hawa: “Hawa ni malaika wanaomlinda mwanadamu kutoka mbele yake na nyuma yake, na inapokuja Qadari ya Allaah, huachana naye”.
Malaika hawa kama inavyoashiria aayah, humlinda mwanadamu kwa zamu, wanakamata hawa doria ya kumlinda, na muda wao unapomalizika wengine wa kuchukua nafasi yao wanakuja na kadhalika. Ni huduma ya ulinzi wa bure Aliyotuwekea Allaah Mtukufu. Wanatulinda kutokana na tusivyoviona kama majini, mashetani, wachawi, virusi, vimelea na kadhalika. Hivi visivyoonekana inakuwa mtu haiwezekaniki kujilinda navyo kama virusi vya maradhi ya kuambukiza na kadhalika, na Allaah Anatulinda navyo kupitia Malaika hawa. Kadhalika, wanatulinda na tunavyoviona. Hivi tunaweza kuvikwepa, lakini wakati mwingine vinatutokea ghafla na mtu anajikuta ameokoka navyo kwa njia ya ajabu. Hapa Malaika hawa wanakuwa wamefanya kazi yao, isipokuwa kwa lile tu ambalo mtu kaandikiwa.
Mujaahid kasema: “Hakuna mtu yeyote isipokuwa ana Malaika mwenye jukumu juu yake la kumlinda akiwa macho au usingizini kutokana na majini, wanadamu na vijinyama na wadudu hatari”.
Na Allaah Amesema tena:
"وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ"
“Naye Ndiye Aliyedhibiti vyote chini ya Mamlaka Yake, Aliye juu ya Waja Wake. Na Anakutumieni Malaika wachungaji wadhibiti, hata yanapomfikia mmoja wenu mauti, Wajumbe Wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri. [Al-An’aam: 61]
Ash-Shawkaaniy amesema: “Maana ya aayah hii ni kwamba Allaah Anatutumia Malaika wanaotulinda kutokana na maafa mbalimbali na kulinda matendo yetu pia”.