45-Malaika: Kazi Za Malaika: (8)- Malaika Wa Kusajili Amali Za Kheri Na Shari Za Binadamu
Malaika
45: Kazi Za Malaika
(8)- Malaika Wa Kusajili Amali Za Kheri Na Shari Za Binadamu
Ibn Abiy Zamaniyna amesema: “Ahlus Sunnah wanaamini uwepo wa Malaika wenye kusajili amali za mwanadamu; za kheri na za shari”.
Baadhi ya Waislamu wanafahamu kwamba katika Malaika hawa wawili, yuko Raqiyb anayekaa kuliani, na ‘Atiyd anayekuwa kushotoni. Hii ni kosa, kwa kuwa haya si majina yao, bali hizi ni sifa zao. “Raqiyb” ina maana ya mchungaji aliye macho wakati wote, na ‘Atiyd” ina maana ya aliye tayari bila kuchelewa kuandika lolote analolitamka mwanadamu au analolifanya. Hivyo kila mmoja wa Malaika hawa ana sifa hizi mbili za uchungaji na uandishi.
Allaah Ta’aalaa Anasema:
"إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ ● مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ"
“Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni • Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliye tayari (kurekodi)”. [Qaaf: 17-18]
Malaika hawa wana ujuzi kamili wa kazi yao; wanamjua vyema mwanadamu, wanajua matendo yake na kauli zake zote, ya siri yake na ya dhahiri yake.
Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ● كِرَامًا كَاتِبِينَ ● يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ"
“Na hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi (na kuchunga) ● Watukufu wanaoandika (amali) ● Wanajua yale myafanyayo”. [Al-Infitwaar: 10-12]
Na Anasema tena Allaah ‘Azza wa Jalla:
"أَمْ يَحْسَبُونَ أَنَّا لَا نَسْمَعُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُم ۚ بَلَىٰ وَرُسُلُنَا لَدَيْهِمْ يَكْتُبُونَ"
“Au wanadhania kwamba Sisi Hatusikii siri zao na minong’ono yao? Sivyo! (Tunasikia!) Na Wajumbe Wetu wako kwao wanaandika”. [Az-Zukhruf: 80]
As-Sa’adiy amesema kuhusiana na aayah hii: “Hivi wao kwa ujinga wao na dhulma zao wanadhani kwamba Sisi Hatusikii siri zao ambazo hawakuzizungumza zikasikika?! Bali Sisi Tunajua hata siri zilizomo ndani ya nyoyo zao na yote wanayonong’onezana kwa siri. Na wao wanadhani kwamba haya yote yanapita tu hivi hivi! La hasha! Malaika Wetu wako nao na wanaandika yao yote ya siri na dhahiri, na yote yatahifadhiwa mpaka watakapohudhurishwa Siku ya Qiyaamah, yote waliyoyafanya na waliyoyatamka yatahudhurishwa, na Allaah Hatomdhulumu yeyote”.
Al-Baghawiy kasema kuhusiana na aayah hii: “Malaika wawili wenye kazi ya kusajili matendo ya mwanadamu wanapokea matendo yote anayoyafanya mwanadamu na maneno yote anayoyatamka, wanayahifadhi na wanayaandika. Malaika mmoja yuko kulia, na huyu anaandika matendo yote mema na maneno yote mema, na mwingine yuko kushoto, na huyu anaandika matendo yote mabaya na maneno yote mabaya, na kila mmoja wao yuko tayari wakati wote kufuatia matendo na kusikiliza maneno, na hawambanduki mtu hata dakika moja. Chochote unachokitamka, basi uko nao, na chochote ukifanyacho, basi unao”.
Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا هَمَّ عَبْدِي بِسَيِّئَةٍ فَلاَ تَكْتُبُوهَا عَلَيْهِ فَإِنْ عَمِلَهَا فَاكْتُبُوهَا سَيِّئَةً وَإِذَا هَمَّ بِحَسَنَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا فَاكْتُبُوهَا حَسَنَةً فَإِنْ عَمِلَهَا فَاكْتُبُوهَا عَشْرًا"
“Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema (kuwaambia Malaika): Mja wangu akidhamiria kufanya jambo baya, basi msimwandikie, na kama atalifanya, basi mwandikieni baya moja. Na akidhamiria kufanya jambo jema na asilifanye, basi mwandikieni jema moja, na kama atalifanya, basi mwandikieni mema kumi”. [Al-Bukhaariy (7501) na Muslim (128)]
Na amesema tena Abu Hurayrah: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"قَالَتِ الْمَلاَئِكَةُ: رَبِّ ذَاكَ عَبْدُكَ يُرِيدُ أَنْ يَعْمَلَ سَيِّئَةً - وَهُوَ أَبْصَرُ بِهِ – فَقَالَ: ارْقُبُوهُ، فَإِنْ عَمِلَهَا فَاكْتُبُوهَا لَهُ بِمِثْلِهَا . وَإِنْ تَرَكَهَا فَاكْتُبُوهَا لَهُ حَسَنَةً، إِنَّمَا تَرَكَهَا مِنْ جَرَّاىَ"
“Malaika husema: Ee Rabbi wetu! Yule Mja Wako anataka kufanya baya -na Allaah Anamwona zaidi-, Allaah Huwaambia: Mfuatilieni, kama atalifanya, basi mwandikieni mfano wake, na kama ataliacha, basi mwandikieni jema moja, kwani hakika ameliacha kwa ajili Yangu”. [Al-Bukhaariy (42) na Muslim (129)]