76-Malaika: Kuzidiana Ubora Kati Ya Malaika Na Wanadamu

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

76:   Kuzidiana Ubora Kati Ya Malaika Na Wanadamu

 

Ulamaa wametofautiana kuhusiana na suala hili katika kauli kadhaa. 

 

Kauli ya kwanza:  Ni ya Jumhuwr Ahlis Sunnat wal Jama’ah.   Inasema kwamba Manabii na watu wema wamewazidi Malaika kwa ubora kutokana na dalili nyingi.  Miongoni mwa dalili hizo ni:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَقَدِ اخْتَرْنَاهُمْ عَلَىٰ عِلْمٍ عَلَى الْعَالَمِينَ"

 

Na kwa yakini Tuliwakhitari (wana wa Israaiyl) kwa elimu kuliko walimwengu wowote”[Ad-Dukhaan: 32]

 

2-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ "

 

“Hakika Allaah Amemkhitari Aadam na Nuwh na kizazi cha Ibraahiym na kizazi cha ‘Imraan juu ya walimwengu”.  [Aal-‘Imraan: 33]

 

Ibn Taymiyah ametofautiana na kundi hili kwa kusema:  “Neno "العَالَمِيْنَ" linaweza kuja kwa maana ya aina zote za viumbe kama katika "الحَمْدُ للهِ رَبِّ العَالَمِيْنَ" . Pia linaweza kuja kwa maana ya wanadamu tu kama katika aayah:

 

 

"أَتَأْتُونَ الذُّكْرَانَ مِنَ الْعَالَمِينَ "

 

Je, mnawaendea wanaume miongoni mwa walimwengu?"  [Ash-Shu’araa: 165]

 

Au:

 

"وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ"

 

“Na (Tulimtuma) Luwtw, alipowaambia kaumu yake:  Je, mnafanya uchafu (wa liwati) ambao hajakutangulieni nao yeyote katika walimwengu?”  [Al-A’araaf: 80]

 

Na inavyojulikana ni kwamba walikuwa hawawaingilii wanyama au majini au viumbe vingine, isipokuwa wanaume wenzao.

 

Kadhalika, "العَالَمِيْنَ" linaweza kuja kwa maana ya watu walioishi zama moja.  Ni kama katika Neno Lake Ta’aalaa:

 

 

"وَلَقَدِ اخْتَرْنَاهُمْ عَلَىٰ عِلْمٍ عَلَى الْعَالَمِينَ"

 

Na kwa yakini Tuliwakhitari (wana wa Israaiyl) kwa elimu kuliko walimwengu wowote”.  [Ad-Dukhaan: 32]

 

Kwa msingi huu, "العَالَمِيْنَ" inaweza kubeba maana ya aina zote za viumbe, au wanadamu tu.  Ni jina linalowahusu viumbe wote ambao kupitia kwao Allaah Anajulikana, nao ndio dalili ya uwepo Wake na hususan kwa watambuzi kama Malaika.  Na kwa muktadha huu, ni lazima jina libebe maana ya ujumla isipokuwa kama itakuja dalili ya kulihusisha na kiumbe fulani pasi na wengineo.

 

Kauli ya pili:   Ni ya Ibn Hazm na wengineo.  Wanasema kwamba Malaika wamewazidi wanadamu katika hali zote.  Dalili zao ni:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا"

 

Na kwa yakini Tumewakirimu wana wa Aadam, na Tukawabeba katika nchi kavu na baharini, na Tukawaruzuku katika vizuri na Tukawafadhilisha juu ya wengi miongoni mwa Tuliowaumba kwa ufadhilisho mkubwa”.   [Al-Israa:  70]

 

Ibn Hazm amesema kuhusu aayah hii:  “Allaah Amemfadhilisha mwanadamu juu ya viumbe wengi Aliowaumba lakini si juu ya viumbe wote.  Hakuna shaka yoyote kwamba wanadamu ni bora kuliko majini, wanyama na viumbe visivyo na roho, lakini kiumbe pekee anayetolewa nje ya duara hilo ni Malaika ambao Allaah Amewafadhilisha juu ya mwanadamu”.

 

 

2-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"لَّن يَسْتَنكِفَ الْمَسِيحُ أَن يَكُونَ عَبْدًا لِّلَّـهِ وَلَا الْمَلَائِكَةُ الْمُقَرَّبُونَ ۚ وَمَن يَسْتَنكِفْ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيَسْتَكْبِرْ فَسَيَحْشُرُهُمْ إِلَيْهِ جَمِيعًا "

 

“Al-Masiyh kamwe hatojiona bora aje akatae kuwa ni mja kwa Allaah, wala Malaika waliokurubishwa. Na atakayejiona bora akakataa Kumwabudu (Allaah) na akatakabari, basi Atawakusanya wote Kwake.  [An-Nisaa:  172]

 

Ibn Hazm kasema pia kuhusu aayah hii:  “Neno Lake Ta’aalaa baada ya kumtaja Al-Masiyh:  “Wala Malaika waliokurubishwa”, ni kielelezo wazi kuhusu daraja kubwa waliyonayo Malaika ya ukaribu wao kwa Allaah Mtukufu”.

 

3-  Al-Hadiyth Al-Qudsiy:

 

Imesimuliwa na Abu Hurayrah:  “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي، وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي، فَإِنْ ذَكَرَنِي فِي نَفْسِهِ ذَكَرْتُهُ فِي نَفْسِي، وَإِنْ ذَكَرَنِي فِي مَلَأٍ ذَكَرْتُهُ فِي مَلَأٍ خير مِنْهُم"

 

“Allaah Ta’aalaa Anasema: Mimi Niko kwa mujibu wa dhana ya Mja Wangu anavyonidhania, na Mimi Ninakuwa pamoja naye anaponidhukuru.  Akinidhukuru ndani ya nafsi yake, Mimi Nitamdhukuru ndani ya Nafsi Yangu, na Akinidhukuru katika hadhira,  Mimi Nitamdhukuru katika hadhira iliyo bora zaidi kuliko hiyo”.  [Swahiyhul Bukhaariy:  7405]

 

Ibn Battwaal amesema:  “Hadithi hii ni uthibitisho kwamba Malaika ni bora kuliko wanadamu, na hii ndiyo kauli ya jopo la ‘Ulamaa”.

 

Kauli ya tatu:  ‘Ulamaa wa kundi hili wameamua kukaa kimya kuhusiana na suala hili. Wameamua kutosema ni nani mbora kati ya wawili hawa.  Wametosheka kusema tu kwamba lililo wajibu kwetu ni kuamini Malaika na Manabii, na si kuamini kundi lipi lililo bora kuliko jingine, na kama hili lingekuwa ni wajibu, basi lingegusiwa na Qur-aan au Sunnah”.

Share