75-Malaika: Malaika Wanazidiana Kwa Daraja
Malaika
75: Malaika Wanazidiana Kwa Daraja
Malaika wanazidiana kwa ubora. Baadhi yao ni wabora kuliko wengineo, na walio bora zaidi ni wale waliokurubishwa kwa Allaah Ta’aalaa kama Anavyosema Allaah:
"لَّن يَسْتَنكِفَ الْمَسِيحُ أَن يَكُونَ عَبْدًا لِّلَّـهِ وَلَا الْمَلَائِكَةُ الْمُقَرَّبُونَ ۚ وَمَن يَسْتَنكِفْ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيَسْتَكْبِرْ فَسَيَحْشُرُهُمْ إِلَيْهِ جَمِيعًا "
“Al-Masiyh kamwe hatojiona bora aje akatae kuwa ni mja kwa Allaah, wala Malaika waliokurubishwa. Na atakayejiona bora akakataa Kumwabudu (Allaah) na akatakabari, basi Atawakusanya wote Kwake”. [An-Nisaa: 173]
Aayah hii inaonyesha kwamba tabaka za Malaika zinatofautiana kwa ngazi na ubora, na wanaoongoza ni pamoja na Jibriyl, Miykaaiyl, Israafiyl na wabebaji ‘Arshi ya Allaah.
Na Malaika aliye juu na mbora kuliko wote ni Jibriyl ‘Alayhis Salaam. Yeye ni Mjumbe kati ya Allaah na Mitume Wake ambapo alikuwa akiwateremshia Wahyi kutoka kwa Allaah ili nao wawafikishie watu wao.
Allaah Ta’aalaa Amemwita kwa majina matukufu na kumsifu kwa sifa njema kabisa. Amemwita “Ruwhul Qudus” Aliposema:
"قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ لِيُثَبِّتَ الَّذِينَ آمَنُوا وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ"
“Sema: Ameiteremsha Ruwhul-Qudus (Jibriyl) kutoka kwa Rabb wako kwa haki ili iwathibitishe wale walioamini, na ni mwongozo na bishara kwa Waislamu”. [An-Nahl: 102]
Pia Amemwita “Ruwhul Amiyn”:
"نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ "
“Ameiteremsha Ar-Ruwh (Jibriyl) mwaminifu”. [Ash-Shu’araa: 193]
Isitoshe, Allaah Ta’aalaa Amemwelezea kama ni mjumbe mtukufu, mwenye nguvu, mwenye hadhi maalum Kwake Allaah, anatiiwa na Malaika, lakini pia ni mwaminifu. Allaah Anasema:
"إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ● ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ ● مُّطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ"
“Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli ya Mjumbe mtukufu (Jibriyl) ● Mwenye nguvu na cheo kitukufu kwa (Allaah) Anayemiliki ‘Arsh ● Anayetiiwa (na Malaika), mwaminifu huko (mbinguni). [At-Takwiyr: 19-21]
Ama Miykaaiyl na Israafiyl, hawa pia ni katika Malaika wenye hadhi kwa Allaah, kwani wametajwa mara kadhaa katika Qur-aan pamoja na Jibriyl ‘Alayhis Salaam. Kadhalika, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwataja katika dua ya ufunguzi wa Swalah zake za usiku. Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa amesema:
"كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا قَامَ مِنَ اللَّيْلِ افْتَتَحَ صَلَاتَهُ فَقَالَ: اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَائِيلَ وَإِسْرَافِيلَ ، فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ، عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ"
“Alikuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposimama usiku, anaifungua swalah yake kwa kusema: “Ee Allaah! Mola wa Jibriyl, Miykaaiyl, na Israafiyl, Muumba wa mbingu na ardhi, Unayejua yaliyofichikana na yenye kuonekana..” [Muslim (628). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].