46-Tukumbushane: Adhabu Kwa Wasiotoa Zakaah
Tukumbushane
46: Adhabu Kwa Wasiotoa Zaka:
Toka kwa Abu Hurayrah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hakuna yeyote mwenye hazina ya mali ambayo haitolei Zakaah, isipokuwa atapashiwa moto kwenye moto wa Jahannam, kisha ifanywe vipande vipana [vya metali], achomwe navyo mbavu zake na kipaji chake mpaka pale Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki ngamia na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa alazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu baina ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki mbuzi na kondoo na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atalazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga kwa kwato zao, na watampiga kwa pembe zao, hakuna kati yao mwenye pembe zilizopinda wala asiye na pembe, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini katika mnayohesabu. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni…”. [Muslim (987) na Abu Daawuwd (1642)].