45-Tukumbushane: Sote Tutabanwa Na Kaburi

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

45:  Sote Tutabanwa Na Kaburi:

 

Mbano wa kaburi ni jambo la kwanza analokutana nalo maiti kwenye ulimwengu wa “Barzakh”.  “Barzakh” ni hali anayoishi nayo maiti kaburini hadi siku ya kufufuliwa.  Hadiyth kadhaa za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimethibitisha uwepo wa kubanwa maiti na kaburi.

 

Kati ya Hadiyth hizo:

 

1-  Bibi ‘Aaishah:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ لِلْقَبْرِ ضَغْطَةً وَلَوْ كَانَ أَحَدٌ نَاجِيًا مِنْهَا نَجَا مِنْهَا سَعْدُ بْنُ مُعَاذِ"

 

Hakika kaburi lina mbano, na lau kama kuna ambaye angeweza kuokoka nao, basi angeliokoka nao Sa’ad bin Mu’aadh”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika “As-Silsilat As-Swahiyhah” (1695)].

 

2-  Ibn ‘Umar:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuhusu Sa’ad bin Mu’aadh (Radhwiya Allaah ‘anhu) wakati alipokufa:

 

"هَذَا الَّذِي تَحَرَّكَ لَهُ الْعَرْشُ وَفُتِحَتْ لَهُ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَشَهِدَهُ سَبْعُونَ أَلْفًا مِنْ الْمَلَائِكَةِ ، لَقَدْ ضُمَّ ضَمَّةً ثُمَّ فُرِّجَ عَنْهُ"

 

“Huyu ndiye ambaye ‘Arshi ilitikisika kwa ajili yake, milango ya mbingu ikafunguliwa kwa ajili yake, na Malaika elfu 70 walihudhuria mazishi yake, huyu (aliyefanyiwa yote haya) amebanwa akabanika, kisha akaachiliwa”.   [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika “Swahiyh An-Nasaaiy”].

 

Kwa muktadha huu, hakuna yeyote kati yetu atakayepona na mbano huu, ni sawa awe Muislamu, awe kafiri, awe pagani na kadhalika.  Kwa hiyo kila mmoja wetu ajitayarishe kwa hilo, haliepukiki, halina budi.

 

Lakini kwa hali yoyote, mbano kwa Muislamu ni tofauti na mbano kwa kafiri, au pagani na kadhalika.  ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na mbano kwa Muislamu katika kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Kila Muislamu atabanwa, lakini Muislamu mwema atabanwa haraka, kisha kaburi litamwachia na litatanuka, na mateso kwake hayatakuwa marefu.  Ama Muislamu faasik, huyu mbano utakuwa wa nguvu kubwa, na utarefuka kwa mujibu wa madhambi yake.

 

Abul Qaasim As-Sa’adiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Hatonusurika na mbano wa kaburi mwema wala muovu, isipokuwa kwa Muumini mwema utakuwa ni wa haraka, kaburi litamwachia na litatanuka, na mateso hayatokuwa marefu kwake.   Ama faasik, huyu mbano utakuwa mkali kwake, na kibano cha mwandani wake kitarefuka kwa mujibu wa madhambi yake na maasia yake”.

 

Ya pili:

 

Waumini wema watapatwa na mbano wa kaburi, lakini mbano wao utakuwa ni wa upole na mapenzi bila adha wala maumivu.  Ama Waislamu wenye kumwasi Allaah, hao mbano utakuwa mkali kutokana na hasira za kaburi kwao, na utakuwa kwa mujibu wa madhambi yao na matendo yao mabaya.

 

Al-Haafidh Adh-Dhahabiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Mbano huu si chochote kwa upande wa adhabu ya kaburi, bali hilo ni jambo ambalo atalikuta Muumini kama anavyopata maumivu ya kumpoteza mwanaye au kipenzi chake duniani, na kama anavyopata maumivu ya kuugua, au maumivu ya kutoka roho yake, au maumivu ya kuulizwa maswali kaburini mwake na kujaribiwa, au maumivu ya kuathirika kutokana na kuliliwa na watu wake (vilio vya kijahili), au maumivu ya kufufuliwa toka kaburini, au maumivu ya kisimamo na kizaazaa chake, au maumivu ya kupita juu ya Jahannam na mfano wa hayo.  Misukosuko yote hii mtu atakutana nayo, nayo kamwe si katika adhabu ya kaburi, wala adhabu ya Jahannam.  Bali mja mwema mchaji, Allaah Atamfanyia upole katika baadhi yake au yote.  Basi Sa’ad ambaye tunamjua kuwa ni katika watu wa Peponi, mbali na kuwa ni katika Shuhadaa wa daraja la juu kabisa (Radhwiya Allaah ‘anhu), naye pia hajapona na misukosuko hii.  Kana kwamba wewe unadhani kuwa aliyefaulu hataguswa na misukosuko ya nyumba mbili, wala vitisho, wala maumivu, wala khofu?!  Mwombe Mola wako salama na amani, na Atufufue katika kundi la Sa’ad”.  [Siyar A‘alaamun Nubalaa (1/290-292].

 

Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn amesema:  “Mbano wa ardhi kwa Muumini ni mbano wa huruma na mapenzi, ni kama mfano wa kumbatio la mama kwa mwanaye kifuani.  Ama mbano wake kwa kafiri, huo ni mbano wa adhabu na mateso”. 

 

Nini Sababu Ya Mbano Huu?

 

Hakuna Aayah au Hadiyth yoyote iliyoeleza sababu.  Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wamejaribu kukisia sababu.

 

Al-Hakiym At-Tirmidhiy amesema:  “Sababu ya mbano huu ni kwamba hakuna yeyote isipokuwa atakuwa na makosa fulani hata kama ni mtu mwema.  Na mbano huu utakuwa ni malipo yake, kisha rahmah itamkumbatia”.

 

Wengine wamesema sababu ni maasia na uchache wa kushukuru Neema za Allaah.

 

Lakini pamoja na makisio ya sababu hizi, tunakuta kwamba hata watoto wasio na dhambi, nao pia hawatanusurika.  Abu Ayyuwb (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:  “Mtoto alizikwa, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"لَوْ أَفْلَتَ أَحَدٌ مِنْ ضَمَّةِ الْقَبْرِ لَأَفْلَتَ هذَا الصَّبِيُّ"

 

“Lau angelinusurika yeyote na mbano wa kaburi, basi angenusurika mtoto huyu”.  [Imesimuliwa na At-Twabaraaniy katika Al-Mu’ujamul Kabiyr (4/121).  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As-Silsilat As-Swahiyhah (2164)].

 

Tunamwomba Allaah Atufanyie upole wakati wa kubanwa, na mbano uchukue muda mfupi iwezekanavyo, na Atuepushe na adhabu ya kaburi na adhabu ya moto.  Aamiyn.

 

 

Share