10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake: Kuulizwa Kuhusu Mposa Na Mposwa Na Kutaja Kasoro Zao
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا
Posa Na Hukumu Zake
10: Kuulizwa Kuhusu Mposa Na Mposwa Na Kutaja Kasoro Zao:
Mtu akiulizwa na kushauriwa kuhusu mposaji au mposwa, ni lazima aseme ukweli hata ikibidi kutaja mabaya na kasoro zake, na hii haingii kwenye duara la kusengenya kuliko haramishwa ikiwa makusudio yake ni kunasihi na kuhadharisha, na si kumchafua mhusika. Ni kama Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwambia Faatwimah bint Qays wakati alipomtaka ushauri wake:
""أَمَّا أَبُو جَهْمِ فَرَجُلٌ لا يَضَعُ عَصَاهُ عَنْ عَاتِقِهِ، وَأَمَّا مُعَاوِيَةُ فَصُعْلُوكٌ لاَ مَالَ لَه"
“Ama Abu Jahm, yeye ni mtu ambaye hashushi fimbo yake begani (yaani anapiga sana, au anasafiri sana). ُ Ama Mu’aawiya, huyo ni masikini hohehahe, hana chochote”. [Muslim (1480), An-Nasaaiy (3245) na Abu Daawuwd (2284)]
Na akasema tena:
"إِنَّ الدِّينَ النَّصِيحَةُ"
“Hakika dini (haswa) ni kunasihiana”. [Hadiyth Swahiyh]
Mahala pa kutaja mabaya ni pale tu inapohitajika, ama isipohitajika, basi haifai kuyataja.
Na kama atatakwa ajieleze yeye mwenyewe, basi ni lazima aweke wazi kasoro zake kama vile: “Mimi ni bahili sana”, au “Tabia yangu ni ngumu sana” na mfano wa hivyo. Na kama kuna baadhi ya maasia anayafanya, basi ni lazima atubie haraka na asiyataje. Na kama atawaambia: “Mimi siwafai” bila kueleza sababu za kutofaa, itatosha.