09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Posa Juu Ya Posa Ya Kafiri
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا
Posa Na Hukumu Zake
09: Posa Juu Ya Posa Ya Kafiri:
Picha ya suala hili iko hivi: “Dhimmiy” (kafiri anayeishi chini ya himaya ya Dola ya Kiislamu) ameposa mwanamke wa Kinaswara au Kiyahudi na posa ikakubaliwa, kisha akaja Muislamu akaposa mwanamke huyo huyo. Au mposaji ni taarikus swalaah, naye anazingatiwa kafiri na ‘Ulamaa wanaoona kwamba asiyeswali ni kafiri. ‘Ulamaa wana kauli mbili katika hali kama hii:
Kauli ya kwanza:
Inajuzu kuposa juu ya posa. Ni kauli ya Ahmad, Al-Awzaaiy, Ibn Al-Mundhir na Al-Khattwaabiy. Dalili zao ni:
1- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"الْمُؤْمِنُ أَخُو الْمُؤْمِنِ فَلاَ يَحِلُّ لِلْمُؤْمِنِ أَنْ يَبْتَاعَ عَلَى بَيْعِ أَخِيهِ وَلاَ يَخْطُبَ عَلَى خِطْبَةِ أَخِيهِ حَتَّى يَذَرَ"
“Muumini ni ndugu ya muumini, hivyo basi, haifai muumini kununua kitu alichokwisha nunua nduguye, au kuposa juu ya posa ya nduguye mpaka aiachie posa”. [Swahiyh. Muslim (1414)]
Allaah Ta’aalaa Ameukata udugu kati ya kafiri na Muislamu, hivyo katazo ni kati ya Muislamu na nduguye Muislamu.
2- Uhalali ndio asili katika mambo yote mpaka lije katazo. Na katazo la kuposa juu ya posa nyingine limekuja likiwa limefungamanishwa na Muislamu tu, na mengineyo yanabakia hivyo hivyo katika uhalali wake.
3- Tamshi la katazo linamhusu Muislamu tu na kumwambatisha nalo mwingine kunaswihi ikiwa ni mfano wake. “Dhimmiy” si kama Muislamu, na hadhi yake si sawa na hadhi ya Muislamu, na kwa ajili hiyo, haikuwa ni wajibu kuwaitikia mwaliko wao wa walima au mfano wake.
Kauli ya pili:
Ni haramu kuposa juu ya posa ya kafiri. Ni kauli ya Jumhuwr. Wanasema kwamba hilo linasababisha adha kwa mposaji wa awali.