27-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Kufanya Vipimo Vya Kitiba Kabla Ya Ndoa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

27:   Kufanya Vipimo Vya Kitiba Kabla Ya Ndoa:

 

Jambo hili halikuweko zamani.  Lakini hivi leo, ukweli na uaminifu umekuwa ni nadra sana.  Watu wanaficha kasoro zao za kisaikolojia na za kimwili kabla ya kuoana.   Na kwa msingi huu, kutokana na mapinduzi makubwa katika nyanja ya tiba, wachumba wawili wanaweza kufanyiwa vipimo vya kitiba ili kujua kama wana magonjwa ya kurithi, au ambukizi, au tatizo la tendo la ndoa au matendo ya kila siku ambayo yataathiri kwa siku za usoni afya ya wanandoa wawili au watoto wao.

 

Rai mashuhuri zaidi ya kitiba kuhusiana na vipimo kwa wanandoa kabla ya kuoana inasema kwamba suala hili lina hali chanya na hasi inayoelezewa kwa muhtasari katika haya yafuatayo:

 

(a)  Yaliyo chanya:

 

1- Ni katika njia bora zaidi za kinga za kuzuia magonjwa hatari ya urithi na ambukizi.

 

2-  Vinaunda kinga kwa jamii, na kinga hii inazuia kuenea kwa magonjwa lakini pia inapunguza idadi ya walemavu.  Hili likifanikiwa linaistawisha jamii kiuchumi na kiutu.

 

3-  Vinatoa dhamana ya kuzaliwa watoto wenye afya kamili na wasio na kasoro zozote za kiakili au kimwili mbali na kutohama magonjwa ya urithi anayoweza kuwa nayo mmoja wa walioposana au wote wawili.

 

4-  Vinafichua uwezekano wa kuzaa au kutokuzaa.  Kuwa tasa kwa mmoja wa wanandoa, kunaweza kuja kuwa miongoni mwa sababu za mivutano na mkorogano kati yao.

 

5-  Vinahakikisha kutokuwepo kasoro za kifisiolojia au za viungo.  Tatizo hili kama liko, litakuwa ni kikwazo kwa kila mwanandoa la kufanya tendo salama la ndoa.

 

6-  Vinahakikisha kutokuweko magonjwa yoyote sugu ambayo ni tishio la utulivu wa maisha ya ndoa.

 

7-  Ni dhamana ya kutodhurika mmoja wao kutoka kwa mwenzake katika kufanya tendo la ndoa, au wakati wa ujauzito au baada ya kuzaa.

 

(b)  Yaliyo hasi:

 

1-   Vinaweza kuleta hali ya kuvunjikwa moyo na kupoteza matumaini.  Lakini ikiwa pia vipimo vitaonyesha uwezekano kwa mwanamke kupata utasa au saratani ya titi, halafu wengine wakajua hilo, hili bila shaka litamsababishia madhara ya kisaikolojia na kutoka kwa jamii yake.  Kwa hali hii, atahisi mustakbali wake umekwisha ingawa mambo ya kitiba hupatia na kukosea.

 

2-  Vinayafanya maisha ya baadhi ya watu kutawaliwa na wasiwasi, huzuni na kukata tamaa anapoelezwa kwamba atakuja kupatwa na maradhi mabaya yasiyoweza kupona.

 

3-  Matokeo ya vipimo hubakia katika hali isiyo ya uhakika kamili katika magonjwa mengi, na si dalili thibitishi ya kugundua na kutabiria magonjwa ya siku za mbeleni.

 

4-  Vinaweza kuwanyima baadhi nafasi ya ndoa kutokana na matokeo ambayo hayana uhakika ndani yake.

 

5-  Ni nadra sana kumkuta mtu bila maradhi yoyote na hususan ya kuthibitishwa uwepo wa magonjwa ya urithi zaidi ya 3000 yaliyo orodheshwa na kuthibitishwa.

 

6-  Kuharakia kutoa ushauri tiba baada ya vipimo kunasababisha matatizo zaidi kuliko kunavyoyatatua.

 

7-  Waliofanya vipimo wanaweza kutendewa vibaya ikiwa siri ya matokeo ya vipimo vyao itafichuliwa na kutumiwa kwa njia ya kuwadhuru.

 

Huu ndio muhtasari wa rai ya tiba kuhusiana na vipimo kabla ya ndoa.  Sasa vipi kwa upande wa msimamo wa sharia ya Kiislamu?  Je, inajuzu kuwalazimisha wanandoa watarajiwa kufanya?

 

Hakuna shaka kwamba hapo zamani hakukuweko haja ya kufanya haya kwa sababu Waislamu enzi hizo walikuwa na sifa kubwa ya uaminifu katika kueleza kasoro za watu, lakini pia hakukuweko maendeleo ya kisayansi ya kuwawezesha kufanya vipimo kama hivi.  Ama ‘Ulamaa wa enzi yetu ya leo, wao wana mielekeo miwili:

 

Mwelekeo wa kwanza: 

 

Vipimo hivi haviruhusiwi na havina haja.  Kati ya wenye msimamo huu, ni Al-‘Allaamah bin Baaz (Rahimahul Laah).  Sababu ni kuwa kufanya hivyo kunakinzana na kumfanyia Allaah dhana njema, na pia matokeo ya vipimo yanaweza kuwa si sahihi.

 

Mwelekeo wa pili:

 

Vinajuzu na wala havipingani na sharia ya Kiislamu.  Hii ni kauli ya ‘Ulamaa wengi wanaosema kwamba hilo halipingani na sharia wala halipingani na kuwa na Imani na Allaah, kwa kuwa mtu anatumia nyenzo alizonazo.  ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) alisema wakati ugonjwa wa tauni ulipoibuka huko Sham:

 

"أَفِرُّ مِن قَدَرِ اللَّهِ إلى قَدَرِ اللَّه" 

 

“Ninakimbia toka kwenye Qadari ya Allaah kwenda kwenye Qadari ya Allaah”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy]

 

Ninasema:   “Huenda mwelekeo huu pamoja na hadhari na kuweka maneno akiba, ndio ulio karibu zaidi.  Na unaweza kutolewa dalili ya kujuzu kwake kwa haya yafuatayo:

 

1-  Kukilinda kizazi ni katika mihimili mikuu mitano ambayo Aayaat na Hadiyth nyingi zimeipa umuhimu na kutoa wito wa kuichunga na kuisimamia vyema.

 

Nabiy Zakariyya (‘alayhis salaam) alimwomba Allaah akisema:

 

"قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً"

 

“Rabb wangu!  Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema”.  [Aal ‘Imraan: 38]

 

Na Waumini pia walimwomba Rabbi wao wakisema:

 

"رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ"

 

“Rabb wetu!  Tutunukie kutoka wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu”.  [Al-Furqaan:  74]

 

2-  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemhimiza Muislamu achague mke toka familia ambayo mabanati zake wana sifa ya uzazi.  Akasema:

 

"تَزَوَّجُوا الْوَدُودَ الْوَلُودَ فَإِنِّي مُكَاثِرٌ بِكُمُ الْأُمَم"

 

“Oeni mwanamke mwenye penzi, mwenye uzazi mwingi, kwani hakika mimi nitajifaharisha kwa wingi wenu kwa umma nyinginezo”.  [Hadiyth Swahiyh]

 

Hadiyth hii inaonyesha umuhimu wa kuchagua kwa kuzingatia afya ya kizazi na uzazi wenyewe.

 

3-  ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: 

 

"أَيُّمَا رَجُلٍ تَزَوَّجَ اِمْرَأَةً فَدَخَلَ بِهَا، فَوَجَدَهَا بَرْصَاءَ، أَوْ مَجْنُونَةً، أَوْ مَجْذُومَةً، فَلَهَا اَلصَّدَاقُ بِمَسِيسِهِ إِيَّاهَا، وَهُوَ لَهُ عَلَى مَنْ غَرَّهُ مِنْهَا"

 

“Ikiwa mwanaume yeyote ameoa mwanamke kisha akamwingilia, halafu akamkuta ana mbalanga, au wazimu, au ukoma, basi mwanamke ana haki ya mahari kwa kuwa amemuingilia.  Ikiwa alihadaiwa na mtu ili amwoe (mwanamke huyo), basi mtu huyo atamrejeshea mahari hiyo”.   

 

4-  Hadiyth zinazomhimiza mwanaume kumkagua vyema mke mtarajiwa ili kujua kasoro zake.  Ni kama Hadiyth ya Abu Hurayrah isemayo kwamba mtu mmoja alimchumbia mwanamke na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: 

 

"انْظُرْ إِلَيْهَا فَإِنَّ فِي أَعْيُنِ الْأَنْصَارِ شَيْئًا"

 

“Nenda ukamwangalie, kwani hakika kwenye macho ya Maanswaar kuna ila fulani”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Muslim]

 

5-  Dalili jumuishi zinazohimizia kuwaepuka wenye magonjwa ambukizi kama kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"لا تُورِدُوا المُمْرِضَ على المُصِحِّ"

 

“Msiwaweke pamoja mgonjwa na mzima”. 

 

Na Hadiyth yake:

 

" وَفِرَّ مِنَ الْمَجْذُومِ كَمَا تَفِرُّ مِنَ الأَسَدِ"

 

“Na mkimbie mwenye ukoma kama unavyomkimbia simba”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5380), Ahmad (2/443) na Al-Bayhaqiy (7/217)]

 

6-  Dalili kiujumla zinazokataza kujiingiza kwenye madhara.

 

Na kwa haya tuliyoyataja, tunaweza kusema kwamba kufanya vipimo vya tiba kabla ya ndoa hakupingani na sharia bali kunaendana na makusudio yake.  Na kwa muktadha huu, ikiwa walii wa msichana ataona kuna ulazima na hususan wakati wa kuenea magonjwa, basi itajuzu.  Na vipimo hivi havina taathira yoyote katika kuswihi ndoa.

 

 

Share