04-Majini: Dalili Za Kiakili Za Uwepo Wa Majini

 

 

Majini

 

   

Alhidaaya.com 

 

04-  Dalili Za Kiakili Za Uwepo Wa Majini:

 

Kutojua uwepo wa kitu fulani hakulazimishi kitu hicho kwamba hakipo.  Katika maisha ya mwanadamu, kuna vitu vingi sana vinavyomzunguka naye ana uhakika kwamba viko pamoja na kwamba havioni.  Ni kama umeme ambao unapita kwenye nyaya lakini hauoni, au mawimbi ya sauti ambayo yanasafiri na kumfikia na kuhisi athari yake bila ya kuyaona mawimbi yenyewe. 

 

Muhammad Rashiyd Riza amesema:  “Lau ingelikuwa kutokiona kitu ndiyo dalili sahihi ya kutokuwepo kwake,  wataalamu wasingelijishughulisha kupekua na kutafiti vitu visivyojulikana, na wasingeliweza kugundua viini, virusi na kadhalika vilivyoifanya nyanja ya tiba na upasuaji kufikia mapinduzi haya makubwa tunayoyaona na tutakayoendelea kuyashuhudia kwa miaka mingi  ijayo.  Katika tone moja tu la maji, vinaweza kuonekana viumbe hai vingi kwa kutumia darubini za nguvu.  Na lau kama angelisema yeyote katika karne zilizopita kwamba kuna viumbe hai vidogo mno visivyoonekana kwa macho na vinaishi kwenye mwili wa mwanadamu, basi watu wangesema kwamba mtu huyo ni mwendawazimu”.

 

Na teknolojia ya mawasiliano ya hivi sasa ni katika mambo ambayo hakuna aliyeweza kudhania kwamba yanaweza kufikia hali hii miaka iliyopita nyuma, lakini yametokea na mengi zaidi ya maajabu yatagunduliwa.

 

Abu Bakr Al-Jazaairiy amesema:  “Athari zinazoonyesha kuwepo kwa majini na mashetani ni nyingi sana.  Zinatutosha hizi zifuatazo:

 

1-  Kifafa ambacho kimekuweko kuanzia enzi na enzi.  Hapa tunamaanisha kile kifafa ambacho kinasababishwa na marohani wabaya.  Hata katika enzi yetu ya leo ambapo tiba imeshuhudia mapinduzi makubwa, bado madaktari hawajaweza kufanya lolote kuhusiana na tiba ya kifafa ambacho ni athari ya majini na mashetani na dalili isiyo na shaka kwamba wapo.

 

2-  Majini wanazungumza kupitia kwa mwanadamu wanayemvaa, na mwanadamu huyu akapata kuzungumza mambo ambayo hakuwa akiyajua.  Kadhalika, anaweza kuzungumza lugha ambayo haijui asilani.

 

3-  Jini hutolewa ndani ya mwili wa mwanadamu aliyekuwa amemvaa kwa njia ya ruqya, na jinni akaeleza kwamba anatoka na hatorudi tena ndani ya mwili wa mtu aliyekuwa amemvaa.

 

4-  Kudhihiri baadhi ya majini kwa baadhi ya watu na kuzungumza nao.  Habari ya hili imetangaa kizazi baada ya kizazi.

 

Share