03-Majini: Dalili Za Uwepo Wa Majini Toka Kwenye Hadiyth
Majini
03- Dalili Za Uwepo Wa Majini Toka Kwenye Hadiyth:
Addamiyriyy amesema: “Jua kwamba Hadiyth za Rasuli zinazozungumzia uwepo wa majini na mashetani ni nyingi mno. Pia yapo mashairi ya Waarabu na simulizi zao zinazozungumzia uwepo huo”.
Kati ya Hadiyth hizo ni:
1- Toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"خُلِقَتِ الْمَلاَئِكَةُ مِنْ نُورٍ، وَخُلِقَ الْجَانُّ مِنْ مَارِجٍ مِنْ نَارٍ، وَخُلِقَ آدَمُ مِمَّا وُصِفَ لَكُمْ"
“Malaika wameumbwa kutokana na nuru, na majini wameumbwa kutokana na mwako mchanganyiko wa moto, na Aadam ameumbwa kutokana na hicho mlichoelezewa (udongo)”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (2996)]
2- Toka kwa ‘Aamir, amesema:
"عن عامر، قال: سألتُ عَلْقَمةَ: هل كان ابنُ مسعود شَهِدَ مع رسول الله صلى الله عليه وسلم ليلةَ الجنِّ قال: فقال عَلْقَمةُ، أنا سألتُ ابنَ مسعود فقلتُ: هل شَهِدَ أحدٌ منكم مع رسول الله صلى الله عليه وسلم ليلةَ الجنِّ؟ قال لا، ولكنَّا كنَّا مع رسول الله ذاتَ ليلة ففَقَدْناه فالتمسناه في الأودية والشِّعاب. فقلنا استُطِير أو اغْتِيل قال: فبِتْنَا بِشَرِّ ليلة بات بها قومٌ، فلما أصبحْنا إذا هو جاء من قِبَل حِرَاء. قال: فقلنا يا رسول الله فقدْناك فطلبْناك فلم نجدْك، فبِتْنَا بِشَرِّ ليلة بات بها قوم. فقال: أتاني داعي الجِنِّ فذَهَبْتُ مَعَه فقَرَأتُ عليهمُ القُرآنَ، قال: فانطَلَقَ بنا فأرانا آثارَهم، وآثارَ نيرانِهم، وسَألوه الزَّادَ، فقال: لَكَم كُلُّ عَظمٍ ذُكِرَ اسمُ اللَّهِ عليهِ يَقَعُ في أيديكُم أوفَرَ ما يَكونُ لَحمًا، وكُلُّ بَعرةٍ عَلَفٌ لدَوابِّكُم. فقال رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: فلا تَستَنجوا بها؛ فإنَّها طَعامُ إخوانِكُم"
“Nilimuuliza ‘Alqamah kama Ibn Mas-‘uwd alihudhuria pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa kukutana na majini. ‘Alqamah akasema: Mimi nilimuuliza Ibn Mas-‘uwd kama kuna yeyote kati yao ambaye alihudhuria pamoja na Rasuli (Swalla nAllaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku huo. Akasema: Hapana, lakini sisi usiku mmoja tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah, kisha akatupotea. Tukaanza kumtafuta kwenye mabonde na njia za milimani tusimpate. Tukasema: Pengine majini wameruka naye, au pengine ameuawa. Hapo tukakesha usiku mbaya kabisa ambao watu hawajawahi kukesha. Kulipopambazuka, ghafla tukamwona anakuja kutokea pande za Hiraa. Tukamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Tumekukosa, tukakutafuta sana na wala hatukukupata, na tukakesha usiku mbaya mno ambao hatujawahi kuupitia. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia: Alinijia mjumbe wa majini (kunialika) nami nikaongozana naye, kisha nikawasomea Qur-aan. Halafu (Rasuli) akaondoka nasi na akawa anatuonyesha athari zao na athari za mioto yao. Na majini hao walimwomba awaainishie kitu ambacho kitakuwa ni chakula kwao. Akawaambia: Ni haki yenu mifupa yote mnayoipata ambayo imetajiwa Jina la Allaah, mnapoipata itakuwa na nyama nyingi, na pia vinyesi vyote vya wanyama ni malisho kwa wanyama wenu. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Basi msistanji kwavyo, kwani ni chakula cha ndugu zenu”. [Swahiyh Muslim: 450]
3- Toka kwa Abu Hurayrah: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إنَّ عِفْريتًا مِنَ الجِن ِّتَفَلَّتَ البارِحةَ ليَقطَعَ عَليَّ صَلاتي، فأمكَنَني اللَّهُ مِنه فأخَذْتُه، فأرَدتُ أن أربِطَه على ساريةٍ من سَوارَي المَسجِدِ حَتَّى تَنظُروا إليهِ كُلُّكُم، فذَكَرْتُ دَعوةَ أخي سُلَيمانَ: رَبِّ هَبْ لي مُلْكًا لا يَنبَغي لأحَدٍ من بَعْدي، فرَدَدتُه خاسِئًا"
“Hakika afriti mmoja katika majini alinitokezea ghafla ili anivurugie swalah yangu, lakini Allaah Alinipa nguvu nikaweza kumdhibiti. Nikataka kumfunga kwenye nguzo moja kati ya nguzo za Msikiti ili nyinyi nyote muweze kumwona. Na hapo nikakumbuka dua ya ndugu yangu Sulaymaan: Rabb wangu! Nitunukie ufalme asiupate mtu yeyote baada yangu, kisha nikamwachia aende zake akiwa amedhalilika”.. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (461)]
An Nawawiy amesema: “Katika Hadiyth hii, kuna dalili kwamba majini wapo na kwamba baadhi ya wanadamu wanaweza kuwaona. Ama Kauli Yake Ta’aalaa: “Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni yeye na kabila lake (la mashetani) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni”, hii inachukulika juu ya walio wengi ambao hawawaoni katika sisi. Na kama kuwaona isingeliwezekana, basi Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asingelisema haya aliyoyasema ya afriti huyo kumtokezea, akamdhibiti na akataka kumfunga kwenye nguzo ya Msikiti”.
4- Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"وكَّلني رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم بحِفظِ زَكاةِ رَمضانَ، فأتاني آتٍ فجَعَلَ يَحثو مِنَ الطَّعامِ فأخذْتُه، وقُلتُ: واللهِ لأرفَعَنَّك إلى رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، قال: إنِّي مُحتاجٌ، وعليَّ عيالٌ، ولي حاجةٌ شَديدةٌ، قال: فخَلَّيتُ عَنه، فأصبَحْتُ، فقال النَّبيُّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: يا أبا هُريرةَ، ما فعل أسيرُكَ البارِحةَ؟، قال: قُلتُ: يا رَسولُ اللَّهِ، شَكا حاجةً شَديدةً وعِيالًا فرَحمْتُه، فخَلَّيتُ سَبيلَه، قال: أما إنَّه قد كذَبَكَ وسَيَعودُ، فعَرَفْتُ أنَّه سَيَعودُ؛ لقَولِ رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: إنَّه سَيَعودُ، فرَصدْتُه، فجاءَ يَحثو مِنَ الطَّعامِ، فأخَذْتُه، فقُلتُ: لأرفَعَنَّكَ إلى رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، قال: دَعْني فإنِّي مُحتاجٌ وعليَّ عيالٌ، لا أعودُ، فرَحِمْتُه، فخَلَّيتُ سَبيلَه، فأصبَحْتُ، فقال لي رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: يا أبا هُريرةَ، ما فعل أسيرُكَ؟، قُلتُ: يا رَسولَ اللَّهِ شَكا حاجةً شَديدةً وعيالًا، فرَحمْتُه، فخَلَّيتُ سَبيلَه، قال: أمَا إنَّه قد كذَبَكَ وسَيَعودُ، فرَصدَتُه الثَّالِثةَ، فجاءَ يَحثو مِنَ الطَّعامِ، فأخَذتُه، فقُلتُ: لأرفَعَنَّكَ إلى رَسولِ اللَّهِ، وهَذا آخِرُ ثَلاثِ مَرَّاتٍ، أنَّكَ تَزعُمُ لا تَعودَ، ثُمَّ تَعودُ، قال: دَعْني أعلِّمْكَ كَلِماتٍ يَنفَعُكَ اللهُ بها، قُلتُ: ما هوَ؟ قال: إذا أوَيتَ إلى فراشِكَ، فاقرَأْ آيةَ الكُرسيِّ: اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ، حَتَّى تَختِمَ الآيةَ، فإنَّكَ لَن يَزالَ عليكَ مِنَ اللَّهِ حافِظٌ، ولا يَقْرَبَنَّكَ شَيطانٌ حَتَّى تُصبِحَ، فخَلَّيتُ سَبيلَه، فأصبَحْتُ، فقالَ لي رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: ما فعل أسيرُكَ البارِحةَ؟، قُلتُ: يا رَسولَ اللَّهِ، زَعَمَ أنَّه يُعَلِّمُني كَلِماتٍ يَنفَعُني اللَّهُ بها، فخَلَّيتُ سَبيلَه، قال: ما هيَ؟، قُلتُ: قال لي: إذا أويتَ إلى فراشِكَ فاقرَأْ آيةَ الكُرسيِّ مِن أوَّلِها حَتَّى تَختِمَ الآيةَ: اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ، وقال لي: لَن يَزالَ عليكَ مِنَ اللَّهِ حافِظٌ، ولا يَقرَبُكَ شَيطانٌ حَتَّى تُصبِحَ ، فقال النَّبيُّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: أمَا إنَّه قد صَدَقَكَ وهوَ كَذُوبٌ، تَعلَمُ من تُخاطِبُ مُنذُ ثَلاثِ ليالٍ يا أبا هُريرةَ؟، قال: لا، قال: ذاكَ شَيطانٌ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda zaka ya Ramadhani. Akanijia mtu, na akaanza kuteka chakula kwa mikono yake, nami nikamkamata. Nikamwambia: Wal-Laahi, nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akasema: Mimi ni mhitaji, nina watoto, na nina dhiki sana. Nikamwachia. Nilipopambaukiwa, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza: Ee Abu Hurayrah! Alifanya nini mateka wako usiku? Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Alinililia dhiki na watoto, nami nikamhurumia halafu nikamwachilia aende zake. Akasema: Ahaa, basi jua kwamba amekudanganya na kesho atakuja tena, nami nikajua kwa hakika kuwa lazima atarudi tena kutokana na kauli hiyo ya Rasuli. Nikamvizia, na mara akaja tena na kuanza kuchota chakula, nikamkamata na kumwambia: Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaniambia: Niachie, mimi ni mhitaji na nina mzigo wa watoto, sitorudi tena hapa. Nikamwonea huruma na kumwachia aende zake. Nilipokutana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asubuhi aliniuliza: Ee Abu Hurayrah! Nini alifanya mateka wako? Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Alinililia dhiki kubwa na watoto, nami nikamhurumia na kumwacha aende zake. Akasema: Basi ujue kwamba amekudanganya na atarudi tena. Nikamvizia tena mara ya tatu, naye akaja, akaanza kuchota chakula, nami nikamkamata. Nikamwambia: Lazima nikupeleke kwa Rasuli wa Allaah, na hii ni mara ya tatu na ya mwisho, unadai hutorudi kisha unarudi. Akasema: Niache nikufundishe maneno ambayo Allaah Atakunufaisha kwayo. Nikamuuliza: Ni yepi hayo? Akasema: Unapokwenda kitandani kwako kulala, basi soma Aayatul Kursiy اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ mpaka mwisho wa Aayah, hapo wewe utabaki na mlinzi anayekulinda toka kwa Allaah. Na kamwe shetani hatokukurubia mpaka upambaukiwe, nami nikamwachia aende zake. Nilipokutana asubuhi na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza: Mateka wako alifanya nini jana? Nikamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Alidai kwamba atanifundisha maneno ambayo Allaah Ataninufaisha kwayo, nami nikamwachia aende zake. Akaniuliza: Ni maneno gani hayo? Nikamwambia: Aliniambia: Ukienda kitandani kwako kulala, basi soma Aayatul Kursiy toka mwanzo wake hadi mwisho اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ . Akasema: Mlinzi toka kwa Allaah ataendelea kukulinda, na shaytwaan hatokukurubia mpaka asubuhi. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: Basi ujue kwamba amekwambia ukweli lakini yeye ni mwongo kupindukia. Basi je, unamjua ni nani uliyekuwa unazungumza naye toka siku hizo tatu zilizopita ee Abu Hurayrah? Nikasema hapana. Akasema: Basi huyo ni shetani”. [Swahiyhul Bukhaariy (2311)]
Ibn Hajar amesema: “Katika Hadiyth hii kuna faida kadhaa. Kati yake ni:
- Kwamba shetani anaweza kuyajua mambo ambayo yanamnufaisha Muislamu.
- Mtu mwovu anaweza kuipata hikmah lakini asiweze kunufaika nayo, na mtu akaichukua kutoka kwake na kunufaika nayo.
- Mtu anaweza kulijua jambo la faida lakini akashindwa kulitumia.
- Ni tabia ya shetani kusema uongo.
- Shetani anaweza kujiweka katika umbile la mwanadamu akaweza kuonekana.
- Majini wanakula vyakula wanavyokula wanadamu, wanazungumza lugha za wanadamu, wanaiba vya wanadamu na wanahadaa.