06-Majini: Majini Wanaoana Na Wanazaana

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

06-  Majini Wanaoana Na Wanazaana:

 

Majini wanaoana na wanazaana.  Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا"

 

Na pindi Tulipowaambia Malaika:  Msujudieni Aadam.  Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini, akaasi Amri ya Rabb wake.  Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami, na hali wao kwenu ni maadui?  Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu!”  [Al-Kahf: 50]

 

Watoto hawapatikani bila mke na mume, na hii ni dalili kwamba wanaoana na kuzaana .

 

Ibn Al-Hajar Al-Haytamiy amesema:  “Hii ni dalili kwamba wanaoana kwa ajili ya kupata watoto”.

 

Qataadah amesema:  “Shetani anaoa na anazaa kama anavyooa mwanadamu na kuzaa”.

 

Na Allaah Ta’aalaa Amesema tena: 

 

"لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ"

 

Hajawabikiri kabla yao binadamu yeyote wala jinni”.  [Ar-Rahmaan:  56]

 

Ibn Hajar Al-Haythamiy amesema:  “Hii inaonyesha kwamba majini wana uwezo wa kuingilia na kuvunja bikira”.

 

Allaah Ta’aalaa Amesema tena:

 

"وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا"

 

Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu”.  [Al-Jinn:  06]

 

Kwa vile wako wanaume katika majini, ni lazima pia waweko wanawake katika majini.  Na uwepo wa jinsia hizi mbili, unawajibisha kuoana na kuzaana.

 

Anas (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoingia msalani husema:

 

"اللَّهُمُ إنِّي أعوذُ بكَ مِنَ الخُبثِ والخَبائِثِ"

 

“Ee Allaah!  Hakika mimi ninajilinda kwako na majini wanaume na majini wanawake”.  [Al-Bukhaariy (142) na Muslim (375)]

 

Share