07-Majini: Majini Wanakula Na Wanakunywa

 

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

07-  Majini Wanakula Na Wanakunywa:

 

Malaika kama inavyojulikana hawali wala hawanywi, lakini majini na mashetani wanakula na wanakunywa.  Na dalili ya hili ni haya yafuatayo:

 

1-  Toka kwa ‘Aamir, amesema:

 

 سألتُ عَلْقَمةَ: هل كان ابنُ مسعود شَهِدَ مع رسول الله صلى الله عليه وسلم ليلةَ الجنِّ قال: فقال عَلْقَمةُ، أنا سألتُ ابنَ مسعود فقلتُ: هل شَهِدَ أحدٌ منكم مع رسول الله صلى الله عليه وسلم ليلةَ الجنِّ؟ قال لا، ولكنَّا كنَّا مع رسول الله ذاتَ ليلة ففَقَدْناه فالتمسناه في الأودية والشِّعاب. فقلنا استُطِير أو اغْتِيل قال: فبِتْنَا بِشَرِّ ليلة بات بها قومٌ، فلما أصبحْنا إذا هو جاء من قِبَل حِرَاء. قال:  فقلنا يا رسول الله فقدْناك فطلبْناك فلم نجدْك، فبِتْنَا بِشَرِّ ليلة بات بها قوم. فقال: أتاني داعي الجِنِّ فذَهَبْتُ مَعَه فقَرَأتُ عليهمُ القُرآنَ، قال: فانطَلَقَ بنا فأرانا آثارَهم، وآثارَ نيرانِهم، وسَألوه الزَّادَ، فقال: لَكَم كُلُّ عَظمٍ ذُكِرَ اسمُ اللَّهِ عليهِ يَقَعُ في أيديكُم أوفَرَ ما يَكونُ لَحمًا، وكُلُّ بَعرةٍ عَلَفٌ لدَوابِّكُم. فقال رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: فلا تَستَنجوا بها؛ فإنَّها طَعامُ إخوانِكُم" 

 

“Nilimuuliza ‘Alqamah kama Ibn Mas-‘uwd alihudhuria pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa kukutana na majini.  ‘Alqamah akasema:  Mimi nilimuuliza Ibn Mas-‘uwd kama kuna yeyote kati yao ambaye alihudhuria pamoja na Rasuli (Swalla nAllaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku huo.  Akasema:  Hapana, lakini sisi usiku mmoja tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah, kisha akatupotea.  Tukaanza kumtafuta kwenye mabonde na njia za milimani tusimpate.  Tukasema:  Pengine majini wameruka naye, au pengine ameuawa.  Hapo tukakesha usiku mbaya kabisa ambao watu hawajawahi kukesha.  Kulipopambazuka, ghafla tukamwona anakuja kutokea pande za Hiraa.  Tukamwambia:  Ee Rasuli wa Allaah!  Tumekukosa, tukakutafuta sana na wala hatukukupata, na tukakesha usiku mbaya mno ambao hatujawahi kuupitia.   Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia:  Alinijia mjumbe wa majini (kunialika) nami nikaongozana naye, kisha nikawasomea Qur-aan.  Halafu (Rasuli) akaondoka nasi na akawa anatuonyesha athari zao na athari za mioto yao.  Na majini hao walimwomba awaainishie kitu ambacho kitakuwa ni chakula kwao.  Akawaambia:  Ni haki yenu mifupa yote mnayoipata ambayo imetajiwa Jina la Allaah, mnapoipata itakuwa na nyama nyingi, na pia vinyesi vyote vya wanyama ni malisho kwa wanyama wenu.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:  Basi msistanji kwavyo, kwani ni chakula cha ndugu zenu”.  [Swahiyh Muslim:  450]

 

Ibn Hubayrah amesema:  “Katika Hadiyth hii, kuna mambo yanayoonyesha huruma na upole wa Allaah kwa sisi wanadamu.  Ametuchagulia sisi vitu vyema na vizuri vya kuvila na Akavifanya baadhi ya tusivyoweza kuvila kama mifupa kuwa chakula kwa ndugu zetu majini.  Kwa picha hii, inatakikana kwa Muislamu auhifadhi vizuri mfupa kisha autupe sehemu nzuri kwa niya ya kuwa ni swadaqah kwa majini, lakini pia alitaje Jina la Allaah ili Waumini wa kijini waupate wakiwa na hisia njema.  Vile vile, asiuvunje ili waupate ukiwa katika hali bora zaidi ya inavyokuwa nyama”.

 

Kadhalika, Hadiyth hii inatuonyesha Huruma ya Allaah kwetu kwa kukifanya chakula chetu kitokane na nafaka halisi za mahindi, mpunga, ngano, na kadhalika, na chakula cha wanyama wetu kitokane na majani, ukoka, pumba, chuya na kadhalika.  Kadhalika, Amekifanya kinyesi cha wanyama wetu kuwa pia ni chakula kwa majini ili Atufundishe sisi wanadamu kwamba hakuna chochote katika Alivyoviumba Allaah ambacho kinapotea bure, na kwamba vitu pamoja na wingi wake, vimeshakadiriwa kwa kila mmoja katika Viumbe Vyake kuweza kuvitumia.

 

Jaabir bin ‘Abdullaah (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"إذا دَخَلَ الرَّجُلُ بَيتَه، فذَكَرَ اللَّهَ عِندَ دُخولِهِ وعِندَ طَعامِهِ، قال الشَّيْطَانُ: لا مَبيتَ لَكُم، ولا عَشاءَ، وإذا دَخَلَ فلَم يَذكُرِ اللَّهَ عِندَ دُخولِهِ، قال الشَّيْطَانُ : أدرَكتُمُ المَبيتَ، وإذا لَم يَذكُرِ اللَّهَ عِندَ طَعامِهِ، قال: أدرَكتُمُ المَبيتَ والعَشاءَ"

 

“Mtu akiingia nyumbani kwake na akamdhukuru Allaah wakati wa kuingia na wakati wa kula, shetani husema (kuwaambia wasaidizi wake):  Hamna pa kulala wala pa kula hapa.  Na anapoingia bila ya kumdhukuru Allaah wakati anaingia, shetani huwaambia:  Mmepata pa kulala hapa.  Na kama hakumdhukuru wakati wa kula huwaambia:  Mmepata malazi, na mmepata na chakula pia”.  [Swahiyh Muslim (2018)]

 

Hadiyth hii inatufunza fadhla ya kumtaja Allaah ambayo pia ni sababu ya kumfukuza shetani.  Shetani anaitumia vizuri nafasi kama mtu ataghafilika kumdhukuru Allaah, na kwamba shetani huyu anakula sambamba na mtu asiyemdhukuru Allaah.  

 

Toka kwa Hudhayfah (Radhwiya Allaah ‘anhu): 

 

"كُنَّا إذا حَضَرنا مَعَ النَّبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم طَعامًا لَم نَضَع أيديَنا حَتَّى يَبدَأَ رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم فيَضَعَ يَدَه، وإنَّا حَضَرنا مَعَه مَرَّةً طَعامًا، فجاءَت جاريةٌ كأنَّها تدفَعُ، فذَهَبَت لتَضَعَ يَدَها في الطَّعامِ، فأخذَ رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم بَيدِها، ثُمَّ جاء أعرابيٌّ كأنَّما يُدفَعُ فأخذَ بيدِهِ، فقال رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم:  إنَّ الشَّيْطَان يَستَحِلُّ الطَّعامَ ألَّا يُذكَرَ اسمُ اللَّهِ عليهِ، وإنَّه جاءَ بهذه الجاريةِ ليَستَحِلَّ بها فأخَذْتُ بَيدِها، فجاءَ بهَذا الأعرابيِّ ليَستَحِلَّ بهِ فأخَذْتُ بيدِه، والَّذي نَفسي بيدِه، إنَّ يَدَه في يَدي مَعَ يَدِها"

 

“Tulikuwa tunapokula chakula pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hatunyooshi mikono yetu mpaka Rasuli aanze kuweka mkono wake.  Na mara moja tulikula naye chakula, na ghafla akaja msichana mdogo haraka akiwa kama anasukumwa na kitu.  Halafu akasogea ili amege chakula lakini, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkamata mkono. Kisha akaja bedui kana kwamba anasukumwa na kitu, na Rasuli akaukamata mkono wake.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:  Hakika shetani hukihalalisha chakula ambacho hakijatajiwa Jina la Allaah, na shetani amekuja pamoja na binti huyu ili ahalalishe chakula kupitia kwake, na mimi nimeuzuia mkono wake.  Akaja pia na bedui huyu ili akihalalishe kupitia kwake, na mimi nimeuzuia mkono wake.  Naapa kwa Yule Ambaye Nafsi Yangu iko Mkononi Mwake, hakika mkono wake (shetani) pamoja na wa bedui na wa binti, iko mkononi mwangu nimeikamata”.  [Swahiyh Muslim: 2017]

 

Ibn Hubayrah amesema:  “Hapa tunapata kutambua kwamba ni jambo lililokokotezwa kusema “Bismil Laahi” wakati wa kuanza kula, na kwamba Allaah Ta’aalaa Hukibarikia chakula ambacho mlaji anakianza kwa kutaja Jina Lake, kwa vile Anakilinda kutokana na shetani.  Shetani anashiriki chakula cha mtu kama hakulitaja Jina la Allaah, kwa sababu Allaah ni nuru kama Alivyosema:  “Allaah Ni Nuru ya mbingu na ardhi”.  Linapotajwa Jina lake wakati wa kula, nuru hiyo hukifunika chakula hicho.  Mwanadamu anaponyooosha mkono wake kwenye chakula bila kusema “Bismil Laah”, hapo humfungulia shetani njia ya kunyoosha mkono wake na kuwa sambamba na mkono wake”.

 

‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لا يَأكُلَنَّ أحَدٌ مِنكُم بشِمالِهِ، ولا يَشرَبَنَّ بها؛ فإنَّ الشَّيْطانَ يَأكُلُ بشِمالِهِ، ويَشرَبُ بها"  

 

“Asithubutu mmoja wenu kula kwa mkono wake wa kushoto, na wala asinywe kwa mkono huo, kwa sababu shetani anakula kwa mkono wake wa kushoto na anakunywa nao pia”.  [Swahiyh Al-Bukhaariy (2020)]  

 

An Nawawiy amesema kuhusu Hadiyth hii:  “Tunatakiwa kujiepusha na vitendo vinavyofanana na vya shetani, na tujue kwamba shetani ana mikono miwili”.

 

Ash-Shibliy amesema:  “Wanaosema kwamba majini hawali wala hawanywi, ikiwa wanakusudia kwamba majini wote hawali wala hawanywi, basi kauli yao hiyo ni batili, kwa kuwa inakinzana na Hadiyth nyingi ambazo ni swahiyh zinazothibitisha hili.  Lakini ikiwa wanakusudia aina miongoni mwao kwamba hawali wala hawanywi, basi hili lina uwezekano wa kuwa ndio au siyo, isipokuwa ujumla unaashiria kwamba wote wanakula na wanakunywa”.

 

 

Share