08-Majini: Majini Wanakufa Na Watafufuliwa Baada Ya Kufa

 

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

 

08-  Majini Wanakufa Na Watafufuliwa Baada Ya Kufa:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ حَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ"

 

Hao ndio wale ambao imehakiki juu yao kauli (ya adhabu) kama katika umati nyingi zilizokwishapita kabla yao miongoni mwa majini na wanadamu.  Hakika wao wamekuwa ni wenye kukhasirika”[Al-Ahqaaf: 18]

 

Ibn ‘Atwiyya amesema:  “Kauli Yake:  “Umati nyingi zilizokwishapita kabla yao miongoni mwa majini na wanadamu”, inamaanisha kwamba majini wanakufa kama wanavyokufa wanadamu karne baada ya karne”.

 

Al-Hasan bin Abil Hasan alisema kwenye baadhi ya vikao vyake vya kusomesha ilmu kwamba majini hawafi, lakini Qataadah alimpinga kwa aayah hii, naye akanyamaza.

 

Lakini baadhi wamemtetea wakisema kwamba anamaanisha kuwa majini wamepewa muhula wa kuishi mpaka siku ya kufufuliwa pamoja na Ibliys.  Atakapokufa, na wao pia watakufa pamoja naye kama zinavyoeleza aayaat za Suwrat Al-A’araaf:

 

"قَالَ أَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ   قَالَ إِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ"

 

“(Ibliys) akasema:  Nipe muhula hadi Siku watakapofufuliwa ● (Allaah) Akasema:  Hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula”.  [Al-A’araaf: 14-15]

 

Aayah hii inaonyesha kwamba wako watakaopewa muhula wa kuishi mpaka siku hiyo pamoja na Ibliys.  Inawezekana ni baadhi ya majini na si wote, kwani hakuna dalili ya kuwa ni wote katika Qur-aan au Sunnah.

 

Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasema:

"اللَّهُمُ لَكَ أسلَمتُ، وبِكَ آمَنتُ، وعليكَ تَوَكَّلتُ، وإليكَ أنبْتُ، وبِكَ خاصَمْتُ، اللَّهُمَّ إنّي أعوذُ بعِزَّتِكَ، لا إلَهَ إلَّا أنتَ، أنْ تُضِلَّني، أنتَ الحَيُّ الَّذي لا يَموتُ، والجِنُّ والإنسُ يَموتونَ"

 

“Ee Allaah!  Ni Kwako tu nimejisalimisha, na Wewe tu Ndiye niliyekuamini, na Kwako tu nimetegemeza mambo yangu yote, na Kwako tu ndio nimerejea, na kwa Msaada Wako tu ndio nimeendelea kupambana.  Ee Allaah!  Ninajilinda kwa Nguvu na Utukufu Wako Ulio imara, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe, Usije Kuniachia nikaja kupotea, Wewe Ndiye Uliye Hai Ambaye Hafi ilhali majini na watu ndio wanakufa”.  [Muslim (2717) na Al-Bukhaariy (7383)]

 

Abul-‘Abbaas Al-Qurtubiy amesema: “Sababu ya aina hizi mbili (majini na wanadamu) kuhusishwa na umauti ingawa wanyama wote wanakufa, ni kuwa wao ndio waliokalifishwa, na ndio walengwa wa Risala za Mitume.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إنَّ بالمَدِينَةِ نَفَرًا مِنَ الجِنِّ قدْ أسْلَمُوا، فمَن رَأَى شيئًا مِن هذِه العَوامِرِ فَلْيُؤْذِنْهُ ثَلاثًا، فإنْ بَدا له بَعْدُ فَلْيَقْتُلْهُ، فإنَّه شيطانٌ"

 

“Hakika Madiynah kuna kundi la majini waliosilimu, basi yeyote atakayemwona nyoka yoyote katika hawa ‘awaamir, basi ampe ilani kwamba asionekane tena hapo baada ya siku tatu.  Na kama atajitokeza kwake tena baada ya ilani hiyo, basi amuue, kwani huyo ni shetani”.  [Swahiyh Muslim (2236)]

 

"عَوَامِرٌ" (‘Awaamir) ni aina maalum ya nyoka waliokuwa wamezoeleka kuonekana kwenye nyumba za watu huko Madiynah.  Na amri ya kumuua kama hakuondoka kwenye nyumba na kwamba atakuwa ni shetani, ni dalili kuwa shetani hufa. 

 

Hivyo basi, majini baadhi ya nyakati huwa wanaishi majumbani mwa watu na wanajiweka katika umbo la nyoka hawa waitwao ‘awaamir. 

 

 

Share