09-Majini: Majini Wana Uwezo Wa Kujibadilisha Maumbo Tofauti

 

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

09-  Majini Wana Uwezo Wa Kujibadilisha Maumbo Tofauti:

 

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamethibitisha kwamba majini wanaweza kujiweka katika maumbo tofauti ya kibinadamu, au wanyama na kadhalika.  Ibn Taymiyah amesema: 

 

“Majini wanaweza kujitengeneza katika umbo la binadamu, wanyama, nyoka, nge, ndege na kadhalika”.

 

Dalili zifuatazo zinathibitisha haya:

 

1-  Toka kwa Abud Dardaai (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"قامَ رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم فسَمِعْناه يَقولُ: أعوذُ باللَّهِ مِنكَ، ثُمَّ قال ألعَنُكَ بلعَنةِ اللهِ ثَلاثًا، وبَسطَ يَدَه كأنَّه يَتَناوَلُ شَيئًا، فلَمَّا فرغَ مِنَ الصَّلاةِ قُلنا: يا رَسولَ اللَّهِ، قد سَمِعناكَ تَقولُ في الصَّلاةِ شَيئًا لَم نَسمَعْكَ تَقولُه قَبلَ ذلك، ورَأيناكَ بَسَطْتَ يَدَكَ، قال: إنَّ عَدوَّ اللَّهِ إبليسَ جاءَ بشِهابٍ من نارِ ليَجعَلَه في وجهي، فقُلتُ: أعوذُ باللهِ مِنكَ، ثَلاثَ مَرَّاتٍ، ثُمَّ قُلتُ: ألعَنُكَ بلعَنةِ اللَّهِ التَّامَّةِ، فلَم يَستَأخِرْ، ثَلاثَ مَرَّاتٍ، ثُمَّ أرَدتُ أخْذَه، واللهِ لَولا دَعوةُ أخينا سُلَيمانَ لأصبَحَ مُوثَقًا يَلعَبُ بهِ وِلْدانُ أهلِ المَدينةِ 

 

 “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama halafu tukamsikia akisema:  Najilinda kwa Allaah kutokana na wewe.  Halafu akasema mara tatu:  Ninakulaani kwa laana ya Allaah, halafu akaukunjua mkono wake kama vile anapokea kitu.  Na baada ya kumaliza swalah, tulimwambia:  Ee Rasuli wa Allaah!  Tumekusikia unasema kitu ndani ya swalah hatujawahi kukusikia ukikisema kabla na tukakuona pia unanyoosha mkono wako.  Akasema:  “Hakika adui wa Allaah Ibliys alikuja na kijinga cha moto ili anitupie nacho usoni nami nikasema mara tatu:  Najilinda kwa Allaah kutokana na wewe, kisha nikasema tena mara tatu:  Nakulaani kwa laana iliyotimia ya Allaah, lakini hakuwa tayari kurudi nyuma, kisha nikataka kumkamata.  Wa-Allaah, lau si du’aa ya ndugu yetu Sulaymaan, angekuwa amefungwa na kuchezewa na watoto wa watu wa Madiynah”.  [Swahiyh kwa sharti ya Muslim]
 

2-  Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: 

 

"وكَّلني رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم بحِفظِ زَكاةِ رَمضانَ، فأتاني آتٍ فجَعَلَ يَحثو مِنَ الطَّعامِ فأخذْتُه، وقُلتُ: واللهِ لأرفَعَنَّك إلى رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، قال: إنِّي مُحتاجٌ، وعليَّ عيالٌ، ولي حاجةٌ شَديدةٌ، قال: فخَلَّيتُ عَنه، فأصبَحْتُ، فقال النَّبيُّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: يا أبا هُريرةَ، ما فعل أسيرُكَ البارِحةَ؟، قال: قُلتُ: يا رَسولُ اللَّهِ، شَكا حاجةً شَديدةً وعِيالًا فرَحمْتُه، فخَلَّيتُ سَبيلَه، قال: أما إنَّه قد كذَبَكَ وسَيَعودُ، فعَرَفْتُ أنَّه سَيَعودُ؛ لقَولِ رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: إنَّه سَيَعودُ، فرَصدْتُه، فجاءَ يَحثو مِنَ الطَّعامِ، فأخَذْتُه، فقُلتُ: لأرفَعَنَّكَ إلى رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، قال: دَعْني فإنِّي مُحتاجٌ وعليَّ عيالٌ، لا أعودُ، فرَحِمْتُه، فخَلَّيتُ سَبيلَه، فأصبَحْتُ، فقال لي رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: يا أبا هُريرةَ، ما فعل أسيرُكَ؟، قُلتُ: يا رَسولَ اللَّهِ شَكا حاجةً شَديدةً وعيالًا، فرَحمْتُه، فخَلَّيتُ سَبيلَه، قال: أمَا إنَّه قد كذَبَكَ وسَيَعودُ، فرَصدَتُه الثَّالِثةَ، فجاءَ يَحثو مِنَ الطَّعامِ، فأخَذتُه، فقُلتُ: لأرفَعَنَّكَ إلى رَسولِ اللَّهِ، وهَذا آخِرُ ثَلاثِ مَرَّاتٍ، أنَّكَ تَزعُمُ لا تَعودَ، ثُمَّ تَعودُ، قال: دَعْني أعلِّمْكَ كَلِماتٍ يَنفَعُكَ اللهُ بها، قُلتُ: ما هوَ؟ قال: إذا أوَيتَ إلى فراشِكَ، فاقرَأْ آيةَ الكُرسيِّ: اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ، حَتَّى تَختِمَ الآيةَ، فإنَّكَ لَن يَزالَ عليكَ مِنَ اللَّهِ حافِظٌ، ولا يَقْرَبَنَّكَ شَيطانٌ حَتَّى تُصبِحَ، فخَلَّيتُ سَبيلَه، فأصبَحْتُ، فقالَ لي رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: ما فعل أسيرُكَ البارِحةَ؟، قُلتُ: يا رَسولَ اللَّهِ، زَعَمَ أنَّه يُعَلِّمُني كَلِماتٍ يَنفَعُني اللَّهُ بها، فخَلَّيتُ سَبيلَه، قال: ما هيَ؟، قُلتُ: قال لي: إذا أويتَ إلى فراشِكَ فاقرَأْ آيةَ الكُرسيِّ مِن أوَّلِها حَتَّى تَختِمَ الآيةَ اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ، وقال لي: لَن يَزالَ عليكَ مِنَ اللَّهِ حافِظٌ، ولا يَقرَبُكَ شَيطانٌ حَتَّى تُصبِحَ ، فقال النَّبيُّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: أمَا إنَّه قد صَدَقَكَ وهوَ كَذُوبٌ، تَعلَمُ من تُخاطِبُ مُنذُ ثَلاثِ ليالٍ يا أبا هُريرةَ؟، قال: لا، قال: ذاكَ شَيطانٌ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda zaka ya Ramadhani.  Akanijia mtu, halafu akaanza kuteka chakula kwa mikono yake, nami nikamkamata.  Nikamwambia:  Wal-Laahi, nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Akasema:  Mimi ni mhitaji, nina watoto, na nina dhiki sana.  Nikamwachia. Nilipopambaukiwa, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza:  Ee Abu Hurayrah!  Alifanya nini mateka wako usiku?  Nikasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Alinililia dhiki na watoto nami nikamhurumia halafu nikamwachilia aende zake.  Akasema:  Ahaa, basi jua kwamba amekudanganya na kesho atakuja tena, nami nikajua kwa hakika kuwa lazima atarudi tena kutokana na kauli hiyo ya Rasuli.  Nikamvizia, na mara akaja tena na kuanza kuchota chakula, na hapo hapo nikamkamata na kumwambia:  Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Akaniambia:  Niachie, mimi ni mhitaji na nina mzigo wa watoto, sitorudi tena hapa.  Nikamwonea huruma na kumwachia aende zake.  Ilipoingia asubuhi, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia:  Ee Abu Hurayrah!  Nini alifanya mateka wako?  Nikasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Alinililia dhiki kubwa na watoto, nami nikamhurumia na kumwacha aende zake.  Akasema:  Basi ujue kwamba amekudanganya na atarudi.  Nikamvizia tena mara ya tatu, naye akaja, akaanza kuchota chakula, nami hapo hapo nikamkamata.  Nikamwambia:  Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah, na hii ni mara ya tatu ya mwisho, unadai hutorudi kisha unarudi.  Akasema:  Niache nikufundishe maneno ambayo Allaah Atakunufaisha kwayo.  Nikamuuliza:  Ni yepi hayo?  Akasema:  Unapokwenda kitandani kwako kulala, basi soma Aayatul Kursiy اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ  mpaka mwisho wa Aayah, hapo wewe utabaki na mlinzi anayekulinda toka kwa Allaah.  Na kamwe shaytwaan hatokukurubia mpaka upambaukiwe, nami nikamwachia aende zake.  Ilipoingia asubuhi, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia:  Mateka wako alifanya nini jana?  Nikamwambia:  Ee Rasuli wa Allaah!  Alidai kwamba atanifundisha maneno ambayo Allaah Ataninufaisha kwayo, nami nikamwachia aende zake.  Akaniuliza:  Ni maneno gani hayo?  Nikamwambia:  Aliniambia:  Ukienda kitandani kwako kulala, basi soma Aayatul Kursiy toka mwanzo wake hadi mwisho اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ .  Akasema:  Mlinzi toka kwa Allaah ataendelea kukulinda, na shaytwaan hatokukurubia mpaka asubuhi.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia:  Basi ujue kwamba amekwambia ukweli lakini yeye ni mwongo kupindukia.  Basi je, unamjua ni nani huyo uliyekuwa unazungumza naye toka siku hizo tatu zilizopita ee Abu Hurayrah?  Nikasema hapana.  Akasema:  Huyo ni shetani”.  [Swahiyhul Bukhaariy (2311)]

 

Akizungumzia faida tuzipatazo kutokana na Hadiyth hii, Ibn Hajar amesema:  “Tunapata kujua kwamba shetani anaweza kujua mambo ambayo Muislamu anaweza kufaidika nayo, lakini pia anaweza kujiweka katika baadhi ya maumbo yatakayomfanya aonekane na mwanadamu, na kwamba Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ" 

 

Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni, linahusiana tu pale shetani anapokuwa katika umbile lake la asili aliloumbiwa kwalo, hapo haiwezekani, (lakini akijiweka katika umbile la binadamu au mnyama, hapo anaonekana kama alivyojiweka)”.

 

Ni kama alivyojiweka katika sura ya mwanadamu mwizi wa chakula kwa Abu Hurayrah kwa mujibu wa Hadiyth iliyotangulia.

 

3-  Toka kwa Abu As -Saaib:

 

"أنَّه دَخَل على أبي سَعيدٍ الخُدْريِّ في بَيتِهِ، قال: فوَجَدتُه يُصَلِّي، فجَلَسْتُ أنتَظِرُه حَتَّى يَقضيَ صَلاتَه، فسَمِعتُ تَحريكًا في عَراجِينَ في ناحيةِ البَيتِ، فالتفَتُّ فإذا حَيَّةٌ، فوَثَبْتُ لأقتُلَها، فأشارَ إليَّ: أن اجلِسْ، فجَلَسْتُ، فلَمَّا انصَرَفَ أشارَ إلى بَيتٍ في الدَّارِ فقال: أترى هَذا البَيتَ؟ فقُلت: نَعَم. فقال: كانَ فيه فتًى مِنَّا حَديثُ عَهْدٍ بعُرسٍ. فخَرَجْنا مَعَ رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم إلى الخَندَقِ، فكانَ ذلك الفَتى يَستَأذِنُ رَسولَ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم بأنصافِ النَّهارِ فيَرجِعُ إلى أهلِهِ، فاستَأذَنَه يَومًا فقال لَه رَسولُ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: خُذْ عليكَ سِلاحَكَ، فإنِّي أخشى عليكَ قُرَيظةَ، فأخذَ الرَّجُلُ سِلاحَه، ثُمَّ رَجَعَ فإذا امرَأتُه بَينَ البابَين قائِمةً، فأهوى إليها الرُّمحَ ليَطعَنَها بهِ، وأصابَتْه غَيرةٌ، فقالت لَه: اكفُفْ عليكَ رُمحَكَ، وادخُلِ البَيتَ حَتَّى تَنظُرَ ما الَّذي أخرَجَني! فدَخلُ فإذا بحيَّةٍ عَظيمةٍ مُنْطَويةٍ على الفِراشِ، فأهوى إليها بالرُّمحِ فانتَظَمَها بهِ، ثُمَّ خَرجَ فرَكزَه في الدَّارِ، فاضطَرَبت عليهِ، فما يُدرى أيُّهُما كانَ أسرَعَ مَوتًا الحَيَّةُ أمِ الفَتى؟ قال: فجِئْنا إلى رَسولِ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم فذَكَرْنا لَه، وقُلنا: ادْعُ اللهَ يُحييهِ لَنا، فقال: استَغفِروا لصاحِبِكُم، ثُمَّ قال: إنَّ بالمَدينةِ جِنًّا قد أسلَموا، فإذا رَأيتُم مِنهم شَيئًا فآذِنوه ثَلاثةَ أيَّامٍ، فإنْ بَدا لَكُم بَعدَ ذلك فاقتُلوه، فإنَّما هوَ شَيطانٌ"

 

“Kwamba aliingia kwenye nyumba ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy.  Anasema:  Nikamkuta anaswali.  Nikakaa kumsubiri mpaka alipomaliza kuswali.  Halafu nikasikia mchakato wa sauti toka kwenye mzigo wa kuni pembezoni mwa nyumba.  Nikageuka, kushtuka, naona ni nyoka.  Nikaruka ili nimuue, lakini yeye aliniashiria niketi, nami nikaketi.  Alipomaliza, alinionyesha chumba kwenye nyumba yake na kuniambia:  Unakiona chumba hiki?  Nikamwambia naam.  Akaniambia:  Humu alikuwemo kijana ambaye alikuwa ndio bado bwana harusi, nasi tukatoka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda kwenye Vita vya Khandaq.  Kijana huyo alikuwa akiomba ruksa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katikati ya mchana ili kwenda kwa mkewe.  Na siku moja, alipomwomba ruksa, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:  Chukua silaha yako, usiisahau, kwani mimi ninakuhofia na Quraydhwah (wanaweza kukudhuru).  Kijana akachukua silaha yake na kuelekea nyumbani kwake.  Alipofika, akashtuka kumwona mkewe amesimama kati ya milango miwili.  Hapo hapo wivu ukamchemka, akainama na kuukamata vizuri mkuki wake ili ampige nao.  Mkewe akamwambia:  Weka chini mkuki wako, halafu ingia ndani uangalie nini kilichonitoa humo.  Akaingia, mara kushtuka, akaona joka limejiviringisha kitandani, na hapo hapo alilidunga kwa mkuki likajisokota, kisha akaukita chini mkuki, akageuka ili atoke nje ya nyumba.  Lakini bila kutarajia, joka lile lilijisukuma likamgonga, haijulikani nani alikufa kabla ya mwingine, ni joka au kijana.  Tukaja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tukamhadithia.  Tukamwambia:  Mwombe Allaah Atuhuishie.  Akasema:  Mwombeeni maghfira mwenzenu.  Kisha akasema:  Hakika Madiynah kuna majini ambao wamesilimu, hivyo basi, mkiona chochote kinachoashiria kwamba ni wao, basi wapeni ilani kwamba wasionekane tena baada ya siku tatu, na kama watajitokeza tena kwenu baada ya hapo, basi waueni, kwani hao ni mashetani”.    

 

Neno lake Rasuli “Hakika Madiynah kuna majini ambao wamesilimu”, haimaanishi kwamba kwingineko kusiko Madiynah hakuna majini waliosilimu, bali wako kila mahali, hivyo basi katazo la kuwaua ni sehemu zote ila tu kama watadhihiri tena baada ya kuwahadharisha  na kutoa onyo kwao.  Kadhalika, hatuwezi kufahamu kutokana na Hadiyth hii kama jini huyo ambaye kijana alimuua, alikuwa ni Muislamu au la, na kama pia jini huyo naye alimuua kijana kulipiza kisasi.  Vile vile, kijana huyu pia hakukusudia kuua nafsi ya Muislamu kwa kuwa hakuwa akijua, bali alikusudia kuua kile ambacho kisharia kimeruhusiwa kuuawa.  Hivyo basi, tunaloweza kusema hapa ni kuwa majini makafiri au waovu wao ndio waliomuua kijana kiuadui na kulipizia kisasi. 

 

4-  Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa):

 

"أنَّه كانَ يَقتُلُ الحَيَّاتِ ثُمَّ نَهى، قال: إنَّ النَّبيَّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم هَدمَ حائِطًا لَه، فوَجَدَ فيه سِلْخَ حَيَّةٍ، فقال: انظُروا أينَ هوَ؟ فنَظَروا، فقال: اقتُلوه. فكُنتُ أقتُلُها لذلك، فلَقِيتُ أبا لُبابةَ، فأخبَرَني أنَّ النَّبيَّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم قال: لا تَقتُلوا الجِنَّانَ إلَّا كُلَّ أبتَرَ ذي طُفْيَتَينِ؛ فإنَّه يُسقِطُ الوَلَدَ، ويُذهِبُ البَصَرَ، فاقتُلوه"  

 

“Kwamba yeye alikuwa anaua nyoka, kisha akakataza akisema:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kubomoa ukuta wake, akakuta chini yake gamba la nyoka.  Akasema:  Mtafuteni alikojificha, wakamtafuta, wakamwona, akawaambia:  Muueni.  Nikawa nawaua kutokana na amri hiyo.  Kisha ‘Abdullaah bin ‘Umar akasema:  Nikaja kukutana na Abu Lubaabah, akanieleza kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  Msiwaue nyoka waliozoeleka kuonekana majumbani, isipokuwa kila mwenye mkia mfupi na mistari miwili mgongoni, huyo huangusha mimba na huleta upofu, muueni”.  [Swahiyhul Bukhaariy (3310)]

 

Ibn Hajar Al-Haytamiy amesema:  Kuwavua wenye sifa hizi mbili, kunamaanisha kwamba jini hawezi kujiweka katika umbo lao (la kasoro ya kimwili), hivyo hawa ni vyema kuwaua.

 

5- Jaabir bin ‘Abdullaah amesema:

 

"أَمَرَنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِقَتْلِ الْكِلَابِ حَتَّى إِنَّ الْمَرْأَةَ تَقْدَمُ منَ الْبَادِيةِ بِكَلْبِهَا فَنَقْتُلَهُ، ثُمَّ نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ قَتْلِهَا وَقَالَ: عَلَيْكُمْ بِالْأَسْوَدِ الْبَهِيمِ ذِي النُّقْطَتَيْن فَإِنَّهُ شَيْطَان"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru kuwaua mbwa, hata ikawa mwanamke anakuja tokea majangwani na mbwa wake nasi tunamuua.  Kisha baadaye Rasuli akakataza kuwaua, na akasema:  Muueni tu mweusi mwenye vitone viwili, kwa sababu huyo ni shaytwaan”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1572) na Abu Daawuwd (2846)].

 

6-  Toka kwa Abu Dharr (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إذا قامَ أحَدُكُم يُصَلِّي، فإنَّه يَستُرُه إذا كانَ بَينَ يَدَيهِ مِثلُ آخِرةِ الرَّحلِ، فإذا لَم يَكُن بَينَ يَدَيهِ مِثلُ آخِرةِ الرَّحْلِ، فإنَّه يَقطَعُ صَلاتَهُ الحِمارُ والمَرأةُ والكَلبُ الأسوَدُ. قُلتُ: يا أبا ذر، ما بالُ الكَلبِ الأسوَدِ مِنَ الكَلبِ الأحمَرِ مِنَ الكَلبِ الأصفَرِ؟ قال: يا ابنَ أخي، سَألتُ رَسولَ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم كما سَألتَني فقال: الكَلبُ الأسوَدُ شَيطانٌ"

 

“Anaposimama mmoja wenu kuswali, basi na ajiwekee mbele yake kizuizi (sutrah) chenye urefu wa kwenda juu wa kiasi cha sogi ya ngamia.  Na kama hana chenye urefu huo, basi kwa hakika swalah yake itakatwa na punda, au mwanamke au mbwa mweusi.  Nikasema:  Ee Abu Dharr!  Mbwa mweusi ana nini hata awe tofauti na mbwa mwekundu au mbwa wa njano?!  Akasema:  Ee mtoto wa ndugu yangu, nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) swali hilo hilo uliloniuliza, naye akasema:  Mbwa mweusi ni shetani”.   [Hadiyth Swahiyh.  Swahiyh Muslim (510)]
 

Kuhusiana na kauli ya Rasuli “Mbwa mweusi ni shetani” Ulamaa wamesema yafuatayo:

 

-  Kwamba kikawaida shetani hujiweka katika umbo la mbwa mweusi, na kwa ajili hiyo akasema:  Waueni kila mweusi ti ti ti kati yao.”.

 

-  Kwa vile mbwa mweusi ndiye mwenye madhara zaidi kuliko mwingine na mwenye kutisha zaidi, na mwenye kuswali anapomwona, basi hutetereka akapoteza khushuu, na swalah yake ikakatika.

 

-  Anayekusudiwa ni mbwa mweusi kama alivyo, na si vinginevyo.

 

-  Jini hujimathilisha katika sura ya mbwa mweusi na pia paka mweusi, kwa sababu weusi ni chanzo cha mkusanyo wa nguvu za kishetani, na ndani yake kuna nguvu ya joto.

 

Kuna Uwezekano Wa Kiasi Gani Wa Mwanadamu Kumwona Jini?

 

Kiujumla, mwanadamu anaweza kumwona jini katika umbo jingine lisilo umbo lake la asili.

 

Muhammad Rashiyd Ridhwaa amesema:  “Malaika au jini akijiweka katika picha ya mwanadamu au kiumbe kingine, basi mwanadamu anaweza kumwona, lakini mwanadamu hawezi kuwaona hao katika umbo lao la asili”.

 

Ibn Baaz amesema:  “Jini anaweza kujidhihirisha kwa baadhi ya watu, na baadhi ya watu wanaweza kuwasiliana nao, wanaweza kuwasemesha wakajibishana, baadhi ya watu wanaweza kuwaona, lakini kiuhalisia, majini hawaonekani kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa:

 

"إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ"

 

“Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni”.

 

Na jini anaweza kujitokeza akaonekana na baadhi ya watu majangwani au katika nyumba, na anaweza akamsemesha mwanadamu.  ‘Ulamaa wengi wametuhadithia matukio mengi kuhusiana na hili.  Hata baadhi yao wameeleza kwamba baadhi ya majini wamewahi kuhudhuria majaalisi zao za kiilmu, na wakauliza baadhi ya maswali ya kiilmu wakiwa hawaonekani”.

 

Kiufupi, ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na uwezekano kwa binadamu kuwaona majini katika maumbile yao halisi.  Baadhi yao wanasema kwamba uwezekano huo uko kwa Manabii basi, lakini wengine wanasema hilo pia linawezekana kwa yeyote ambaye Allaah Ametaka awaone katika Waja Wake.

 

Ibn Al-‘Arab amesema:  “Hakuna kizuizi cha kumzuia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaona majini katika umbile lao asili kama anavyowaona Malaika.  Ama kwa sisi, mara nyingi wanadhihiri katika umbo la nyoka”.

Na Hadiyth zinazogusia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wake kuwaona majini, matamshi yake ni jumuishi.  Ima yanabeba uwezekano wa kuwaona katika umbile lao halisi, au kuwaona katika umbo jinginelo.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Kati ya Hadiyth hizo ni:

 

1- -  Toka kwa Abu Hurayrah:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"إنَّ عِفْريتًا مِنَ الجِن ِّتَفَلَّتَ البارِحةَ ليَقطَعَ عَليَّ صَلاتي، فأمكَنَني اللَّهُ مِنه فأخَذْتُه، فأرَدتُ أن أربِطَه على ساريةٍ من سَوارَي المَسجِدِ حَتَّى تَنظُروا إليهِ كُلُّكُم، فذَكَرْتُ دَعوةَ أخي سُلَيمانَ: رَبِّ هَبْ لي مُلْكًا لا يَنبَغي لأحَدٍ من بَعْدي، فرَدَدتُه خاسِئًا" 

 

“Hakika afriti mmoja katika majini alinitokezea ghafla ili anivurugie swalah yangu, lakini Allaah Alinipa nguvu nikaweza kumdhibiti.  Nikataka kumfunga kwenye nguzo moja kati ya nguzo za Msikiti ili nyinyi nyote muweze kumwona.  Na hapo nikakumbuka dua ya ndugu yangu Sulaymaan:  Rabb wangu!  Nitunukie ufalme asiupate mtu yeyote baada yangu, kisha nikamwachia aende zake akiwa amedhalilika”..  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (461)]

 

2-  Hadiyth ya Abu Hurayrah inayohusiana na shetani aliyekuja kuiba chakula cha zaka, akmkamata akiwa katika umbo la binadamu.

 

 

 

Share