10-Majini: Uwezo Wa Baadhi Ya Wanyama Kuwaona Majini

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

10-  Uwezo Wa Baadhi Ya Wanyama Kuwaona Majini:

 

 

Baadhi ya wanyama wana uwezo wa kuwaona majini.  Dalili zifuatazo zinathibitisha hili:

 

1-  Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إذا سَمِعتُم صياحَ الدِّيَكةِ فاسألوا اللهَ مِنْ فَضْلِه؛ فإنَّها رَأت مَلَكًا، وإذا سَمِعتُم نَهيقَ الحِمارِ فتَعوَّذوا باللَّهِ مِنَ الشيطان؛ فإنَّه رَأى شَيطانًا"

 

“Mkisikia jogoo wanawika, basi mwombeni Allaah Fadhla Zake, kwani wanakuwa wamemwona Malaika.  Na mnaposikia sauti kali ya punda, basi jilindeni kwa Allaah na shetani, kwani anakuwa amemwona shetani”.  [Al-Bukhaariy (3303) na Muslim (2729)]

Ibn Al-‘Abbaas Al-Qurtubiy amesema:  “Hii inaonyesha kwamba Allaah Ta’aalaa Amemuumbia jogoo utambuzi wa kuweza kumwona Malaika kama Alivyomuumbia punda utambuzi wa kuweza kumwona shetani”.
 

2-  Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إذا سَمِعتُمْ نِباحَ الكِلابِ، ونَهِيقَ الحَمِيرِ بِالليلِ فتَعَوَّذُوا بِاللهِ من الشيطانِ، فإنَّهُنَّ يَرَيْنَ ما لا تَرَوْنَ، وأَقِلُّوا الخُروجَ إذا هَدَأَتِ الرِّجْلُ؛ فإِنَّ اللهَ عزَّ وجَلَّ يَبُثُّ في لَيْلِهِ من خَلْقِهِ ما يَشاءُ، وأَجِيفُوا الأبوابَ، واذْكُرُوا اسْمَ اللهِ علَيْهَا؛ فإِنَّ الشَّيطانَ لا يَفتَحُ بابًا أُجِيفَ وذُكِرَ اسْمُ اللهِ عليْهِ، وغَطُّوا الجِرارَ، وأوْكِئُوا القِرَبَ، وأكْفِئُوا الآنِيَةَ"

 

“Mkisikia mbweko wa mbwa au mlio wa punda usiku, basi jilindeni kwa Allaah na shetani, kwa kuwa wao wanaona msivyoviona.  Na punguzeni kutoka (usiku) barabara zikiwa hazina watu, kwani Allaah ‘Azza wa Jalla Hueneza katika usiku Wake vyovyote Anavyovitaka katika Viumbe Vyake.  Na fungeni milango, na litajeni Jina la Allaah wakati wa kuifunga, kwani shetani hawezi kufungua mlango uliotajiwa Jina la Allaah wakati wa kuufunga.  Na funikeni vyombo, midomo ya vyungu itatieni kitambaa, na vyombo vitupu vipindueni”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Abu Daawuwd (5103) na Ahmad (14422)] 

 

‘Umar Al-Ashqar amesema:  “Wanyama kuweza kuona vile tusivyoviona si jambo geni.  Wataalamu wamethibitisha kwamba baadhi ya viumbe vinaweza kuona vitu ambavyo sisi hatuwezi kuviona.  Kwa mfano, buma anaweza kumwona panya ndani ya giza totoro”. 

 

 

Share