11-Majini: Wana Spidi Ya Juu Na Uwezo Wa Kufanya Kazi Ngumu

 

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

11-  Wana Spidi Ya Juu Na Uwezo Wa Kufanya Kazi Ngumu:

 

 

Kati ya majini hao, ni wale ambao Allaah Alimtiishia Nabiy Sulaymaan (‘alayhis salaam) wakawa wanamfanyia kazi kubwa za sulubu.  Allaah Ta’aalaa Analielezea hili Akisema:

 

" وَمِنَ الْجِنِّ مَن يَعْمَلُ بَيْنَ يَدَيْهِ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَمَن يَزِغْ مِنْهُمْ عَنْ أَمْرِنَا نُذِقْهُ مِنْ عَذَابِ السَّعِيرِ يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ ۚ اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ"

 

Na (Tulimtiishia pia) kati ya majini wanaofanya kazi mbele yake kwa Idhini ya Rabb wake.  Na yeyote atakayezikengeuka Amri Zetu, Tunamuonjesha adhabu ya moto uliowashwa vikali mno  ●  Wanamfanyia kazi atakayo; (kujenga) ngome ndefu za fakhari na tasawiri, na madeste makubwa kama mahodhi na masufuria makubwa yaliyothibiti imara.  (Tukasema):  Tendeni enyi familia ya Daawuwd huku mkishukuru!  Na wachache miongoni mwa Waja Wangu ndio wenye kushukuru”.  [Sabaa:  13]

 

Na Anasema tena:

 

"فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ رُخَاءً حَيْثُ أَصَابَ    وَالشَّيَاطِينَ كُلَّ بَنَّاءٍ وَغَوَّاصٍ"

 

Basi Tukamtiishia upepo unaokwenda kwa amri yake polepole popote anapotaka kufika  ●  Na mashaytwaan, kila ajengaye na mpiga mbizi”.  [Swaad:  36-37]

 

Na Nabiy Sulaymaan (‘alayhis salaam) alipotaka kukileta kiti cha enzi cha Malkia wa Sabaa, alisema kama inavyosema Qur-aan:

 

"قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَن يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ  •  قَالَ عِفْرِيتٌ مِّنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن تَقُومَ مِن مَّقَامِكَ ۖ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ"

 

Akasema:  Enyi wakuu!  Nani kati yenu ataniletea kiti chake cha enzi kabla hawakunijia wakiwa wamesilimu? ●  Akasema ‘Ifriti miongoni mwa majini:  Mimi nitakuletea kabla hujasimama kutoka mahali pako, na hakika mimi kwa hilo, bila shaka ni mwenye nguvu mwaminifu”.  [Sabaa:  38-39]

 

Kadhalika, Qur-aan imegusia uwezo wao wa kuzifikia anga za juu kabisa na kuzivinjari ili kudukua habari za mbinguni.  Allaah Anasema:

 

"وَأَنَّا لَمَسْنَا السَّمَاءَ فَوَجَدْنَاهَا مُلِئَتْ حَرَسًا شَدِيدًا وَشُهُبًا  •  وَأَنَّا كُنَّا نَقْعُدُ مِنْهَا مَقَاعِدَ لِلسَّمْعِ ۖ فَمَن يَسْتَمِعِ الْآنَ يَجِدْ لَهُ شِهَابًا رَّصَدًا"

 

Na kwamba sisi tulitafuta kuzifikia mbingu, basi tukazikuta zimejaa walinzi wakali na vimondo    Na kwamba sisi tulikuwa tukikaa huko vikao kwa ajili ya kusikiliza, basi atakayetega sikio kusikiliza sasa atakuta kimondo kinamvizia”.  [Al-Jinn:  8-9]

 

Vile vile, Nabiy Sulaymaan (‘alayhis salaam) alikuwa akitumikiwa na majini wapiga mbizi na wafanyao kazi nyinginezo.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَمِنَ الشَّيَاطِينِ مَن يَغُوصُونَ لَهُ وَيَعْمَلُونَ عَمَلًا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ وَكُنَّا لَهُمْ حَافِظِينَ"

 

Na (Tukamtiishia) miongoni mwa mashaytwaan wakimpigia mbizi na wakimfanyia kazi nyinginezo zisizokuwa hizo.  Nasi Tulikuwa Ni Wenye Kuwalinda”.  [Al-Anbiyaa: 82]

 

Ash-Shinqiytwy amesema:  “Walikuwa wakizamia kwenye vina vya bahari na kumtolea kutoka humo vito vya thamani kama lulu na marijani.  Walikuwa pia wakimfanyia kazi nyingine kama kujenga miji, makasri, vyungu vikubwa na mengineyo katika kazi zenye ufanisi wa hali ya juu”.

Lakini majini haya pamoja na uwezo huo mkubwa waliopewa, hawawezi kufanya baadhi ya mambo .  Kati yake ni:

 

1-  Hawawezi kuleta muujiza wowote kama ile waliyokuja nayo Mitume (‘alayhimus Salaam).  Allaah Ta’aalaa Amekanusha Qur-aan kuwa ni kazi ya mashetani, na Akabainisha kwamba hawawezi kuleta chochote katika Qur-aan, Akisema:

 

"وَمَا تَنَزَّلَتْ بِهِ الشَّيَاطِينُ • وَمَا يَنبَغِي لَهُمْ وَمَا يَسْتَطِيعُونَ  • إِنَّهُمْ عَنِ السَّمْعِ لَمَعْزُولُونَ"

 

Na wala hawakuteremka nayo (hii Qur-aan) mashaytwaan  •  Na wala haipasi kwao na wala hawawezi  ● Hakika wao bila shaka wametengwa mbali kuisikiliza”.  [Ash-Shu’araa: 210-212]

 

Na hata majini na wanadamu kwa pamoja, Allaah Amewapa changamoto kwamba hata kama wataungana, hawawezi kuleta mfano wa Qur-aan hii.  Allaah Amesema:

 

"قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا "

 

Sema: Ikiwa watajumuika wana Aadam na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan; hawatoweza kuleta mfano wake na japokuwa watasaidiana wao kwa wao”.  [Al-Israa:  88]

 

2-  Hawawezi kujimathilisha wakaja kwenye ndoto au njozi ya mtu katika sura ya Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"من رَآني في المَنامِ فقد رَآني؛ فإنَّ الشيطان لا يَتَمَثَّلُ بي"

 

“Atakayeniona usingizini basi atakuwa ameniona kikweli, kwa sababu shetani hawezi kujimathilisha katika sura yangu”.  ”

 

Ibn Hajar amesema:  “Hadiyth inaashiria kwamba pamoja na kwamba Allaah Ta’aalaa Amempa jini au shetani uwezo wa kujigeuza katika umbo lolote alitakalo, lakini Hakumpa uwezo wa kujiweka katika sura au umbo la Nabiy Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

3-  Hawawezi kuvuka mipaka maalum kwenye mbingu za juu.

 

Allaah Anasema:

 

"يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَن تَنفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانفُذُوا ۚ لَا تَنفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ"

 

Enyi jamii ya majini na watu!   Mkiweza kupenya kwenye zoni za mbingu na ardhi, basi penyeni.  Hamtoweza kupenya isipokuwa kwa mamlaka (ya Allaah).  [Ar-Rahmaan: 33]

 

4-  Hawawezi kufungua mlango uliotajiwa Jina la Allaah wakati wa kuufunga

 

Toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"فإنَّ الشَّيْطَانَ لا يَفتَحُ بابًا مُغلَقًا، وأوكُوا قِرَبَكُم، واذَكُروا اسمَ اللَّهِ، وخَمِّروا آنيَتَكُم، واذَكُروا اسمَ اللَّهِ، ولَو أن تَعرِضوا عليها شَيئًا، وأطفِؤوا مَصابيحَكُم"

 

“Kwani hakika shetani hawezi kufungua mlango uliofungwa, zibeni midomo ya vyungu vyenu, litajeni Jina la Allaah, funikeni vyombo vyenu na litajeni Jina la Allaah ijapokuwa kwa kuweka kitu juu yake, na zimeni taa zenu”.   [Al-Bukhaariy (5623) na Muslim (2012)]  

5-  Hawakuweza kumdhuru ‘Iysaa na mama yake wakati walipozaliwa

 

Toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"ما من مَولودٍ يُولَدُ إلَّا والشَّيْطَان َيمَسُّه حينَ يُولَدُ، فيَستَهِلُّ صارِخًا من مَسِّ الشّيْطَانِ إيَّاه، إلَّا مَريَم وابنَها، ثُمَّ يَقولُ أبو هُريرةَ: واقرَؤوا إنْ شِئتُموَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
 

“Hakuna mtoto yeyote anayezaliwa isipokuwa shetani humgusa wakati anapozaliwa na mtoto huanza kulia kutokana na mguso huo wa shetani, isipokuwa Maryam na mwanaye (hawa hawakuguswa)”.  Kisha Abu Hurayrah akasema:  Someni mkitaka:

 

"وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"

 

“Nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shetani aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”.  [Aal ‘Imraan:  36]

 

Ibn Hubayrah amesema:  “Hadiyth hii inatuonyeha ni namna gani ulivyo uadui wa shetani kwa mwanadamu kiasi cha kwamba anapoona mtoto kazaliwa tu, hapo hapo humchokonoa mtoto apate kulia.  Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatutaka tuwe tunajilinda nyakati zote na adui huyu pamoja na watoto wetu”.

 

Pia Hadiyth inatufunza kwamba Allaah Ta’aalaa Alimlinda Bi Maryam pamoja na mwanaye kutokana na shetani baada ya Bi Maryam kuomba kinga hiyo kutoka Kwake.

 

 

Share