12-Majini: Mahala Wanakoishi Majini

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

12-  Mahala Wanakoishi Majini:

 

 

 

1-  Majini kiujumla wanaishi ardhini.  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"قَالَ اهْبِطُوا بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ ۖ وَلَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُسْتَقَرٌّ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ"

 

“Akasema:  Shukeni!   Nyinyi kwa nyinyi ni maadui.   Na ardhi itakuwa ndio mastakimu yenu na starehe kwenu mpaka muda mahsusi”.  [Al-A’araaf: 24]

 

Amesema Ibn ‘Aashuwr:  Wanaosemeshwa hapa ni Aadam na mkewe pamoja na Ibliys.  Na kwa amri hiyo, Aadam, mkewe na Ibliys wamekuwa ni katika wakazi wa ardhi”.

 

Allaah Amesema tena:

 

"وَالْأَرْضَ وَضَعَهَا لِلْأَنَامِ"

 

Na ardhi Ameiweka chini kwa ajili ya viumbe”.  [Ar-Rahmaan: 10]

 

Al-Hasan amesema viumbe hapa ni watu na majini.

 

Linalotilia nguvu kuwa wasemeshwa katika aayah hii ni majini na binadamu ni Kauli Yake Ta’alaa baada ya kutaja kila neema katika Neema Zake:

 

"فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ"

 

Basi ni zipi Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?”

 

2-  Majumbani mwa watu:

 

Kuna kundi la majini ambalo linaishi pamoja na watu majumbani mwao.  Hawa ni wale wanaojiweka katika umbo la nyoka kisha wakaingia majumbani.  Ni kama kisa kilichopita nyuma cha kijana aliyekuwa bado ni bwana harusi, akaliua joka lililokuwa nyumbani kwake, na joka nalo likamuua kijana.

 

Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuua nyoka wanaoonekana majumbani kabla ya kuwapa indhari, kwa kuwa wako majini Waislamu kati yao.

 

Toka kwa Naafi’i: 

 

"أنَّ أبا لُبابةَ كُلَّمَ ابن عمر ليَفتَحَ لَه بابًا في دارِهِ، يَستَقرِبُ بهِ إلى المَسجِدِ. فوجَدَ الغِلْمةُ جِلْدَ جانٍّ. فقال عَبدُ اللهِ: التَمِسوه فاقتُلوه. فقال أبو لُبابةَ: لا تَقتُلوه؛ فإنَّ رَسولَ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم نَهى عَن قَتلِ الجِنَّانِ الَّتي في البُيوتِ" 

 

“Kwamba Abu Lubaabah alizungumza na (‘Abdullaah) bin ‘Umar kumtaka amfungulie mlango wa nyumba yake ili Msikiti upate kuwa karibu yake.  Kijana ‘Abdullaah bin ‘Umar akakuta ngozi ya nyoka (wakati anaufungua mlango) na hapo hapo akasema: Msakeni mumuue.  Lakini Abu Lubaabah akasema:  Msimuue, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuua nyoka walioko majumbani”.  [Al-Bukhaariy (3312, 3313) na Muslim (2233)]

 

3-  Mwahala penye najisi nyingi kama vyooni, ndani ya mifumo ya maji taka na kadhalika. 

 

Zayd bin Arqam:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إنَّ هذه الحُشوشَ مُحتَضَرةٌ، فإذا أتى أحَدُكُمُ الخَلاءَ فليَقُلْ: أعوذُ باللهِ مِنَ الخُبُثِ والخَبائِثِ"

 

“Hakika sehemu hizi za kufanyia haja zimekaliwa (na majini na mashetani).  Hivyo basi, anapoingia mmoja wenu chooni aseme:  Najilinda kwa Allaah kutokana na majini wabaya wanaume na majini wabaya wanawake”.  [As-Silsilat As-Swahiyhah: 1070]

 

Kwa mujibu wa Hadiyth hii, vyooni, msalani, bafuni na kadhalika, ndio makazi ya majini na mashetani.  Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuamuru tujikinge kwa Allaah wakati wa kuingia sehemu hizi kutokana shari za viumbe hawa ambao wanaweza kumdhuru mtu.

 

4-  Sehemu wanakolala ngamia au kupumzikia.

 

Jaabir bin Samurah (Radhwiya Allaah ‘anhu amesema:  

 

"فعَن جابِرِ بْنِ سَمُرةَ رَضِيَ اللهُ عَنه: أنَّ رَجُلًا سَألَ رَسولَ الله صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: أأتَوضَّأُ من لُحومِ الغَنَمِ؟ قال: إنْ شِئْتَ فتوَضَّأْ، وإنْ شِئْتَ فلا توَضَّأْ، قال: أتَوَضَّأُ من لُحومِ الإبِلِ؟ قال: نَعَم فتَوَضَّأْ من لُحومِ الإبلِ قال: أصَلِّي في مَرابِضِ الغَنَمِ؟ قال: نَعَم، قال: أصَلِّي في مَبارِكِ الإبِلِ؟ قال: لا"

 

Toka kwa Jaabir bin Samurah (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimwambia:  Je, nitawadhe kama nimekula nyama ya mbuzi au kondoo?  Akamwambia:  Ukitaka unaweza kutawadha, na kama hutaki usitawadhe. Akamuuliza tena:  Je, nitawadhe kwa kula nyama ya ngamia? Akamwambia:  Naam, tawadha ukila nyama ya ngamia.  Akauliza tena:  Je, naweza kuswali kwenye zizi la mbuzi na kondoo?  Akamwambia naam.  Akauliza:  Naweza kuswali wanakopumzikia ngamia?  Akamwambia hapana”.  [Swahiyh Muslim: 360]

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema sababu ya katazo ni kuwa mwahala hapo ni makazi ya mashetani.

 

Abu Hurayrah:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"صَلُّوا في مَرابِضِ الغَنَمِ، ولا تُصَلُّوا في أعطانِ الإبِلِ"  

 

 “Swalini kwenye zizi la mbuzi na kondoo, lakini msiswali sehemu wanakolala na kupumzika ngamia”.

 

Ibn Taymiyah amesema:  “Mahala ambapo pamekatazwa kuswali kama chooni na mapumzikio ya ngamia ni makazi ya mashetani.  Kadhalika, mapango ambayo watu wanafunga safari kuyaendea kwa lengo la kuyatukuza pamoja na maeneo yake husika, kwa kuwa mahala popote ambapo watu wanapatukuza ambapo si Misikiti au maeneo ya kufanyiwa amali za hijja, basi mwahala hapo ni makazi ya mashetani.  Mashetani hao hujiweka katika maumbo ya wanadamu ili watu waone kwamba wao ni katika wanadamu kama Anavyosema Allaah Ta’aalaa:

 

"وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا"

 

“Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wanadamu wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu”.  [Al-Jinn: 06]

 

5-  Kwenye mashimo.

 

Toka kwa Qataadah toka kwa ‘Abdullaah bin Sarjas (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"أنَّ النَّبيَّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم نَهى أن يُبالَ في الجُحْرِ"
 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kukojoa kwenye tundu (la shimo)”.

 

Qataadah aliulizwa:  Kwa nini imekatazwa kukojoa kwenye tundu (la shimo)?  Akasema:  “Ilikuwa inasemwa kwamba shimo ni makazi ya majini”.

 

الجُحْر  kama alivyosema Al-Minaawiy ni kila pahali ambapo wadudu na wanyama wanajichimbia wenyewe kwa ajili ya kukaa humo na kuishi.

 

6-  Kwenye masoko ili kuwafitini watu.

 

 Kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kukaa sana masokoniAlisema akimuusia Salmaan Al-Faarisiy (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"لا تَكونَنَّ إنِ استَطَعْتَ أوَّلَ مَن يَدخُلُ السُّوقَ، ولا آخِرَ مَن يَخرُجُ مِنها؛ فإنَّها مَعْرَكَةُ الشَّيْطَانِ وبِها يَنصِبُ رايَتَه"  

 

“Ukiweza, usije kuwa mtu wa mwanzo kuingia sokoni wala wa mwisho kutoka humo, kwani soko ni medani ya vita ya shetani, na hapo ndipo anaposimika bendera yake”.  [Swahiyh Muslim (2451)]   

 

Share