20-Majini: Je, Ibliys Ni Katika Majini Au Malaika?

 

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

 

20   Je, Ibliys Ni Katika Majini Au Malaika?

 

 

 

"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ "

 

“Na pale Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri”.  [Al-Baqarah:  34]

 

"وَلَقَدْ خَلَقْنَاكُمْ ثُمَّ صَوَّرْنَاكُمْ ثُمَّ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ لَمْ يَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ"

 

“Na kwa yakini Tumekuumbeni kisha Tukakutieni sura; kisha Tukawaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys hakuwa miongoni mwa waliosujudu”.  [Al-A’araaf: 11]

 

"فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ"    إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ "

 

Wakamsujudia Malaika wote pamoja  ●  Isipokuwa Ibliys, alitakabari na akawa miongoni mwa makafiri”.  [Swaad: 73-74]

 

Kadhalika, imeelezwa kiwazi ndani ya Qur-aan kwamba Ibliys ni katika majini.  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا "

 

Na pindi Tulipowaambia Malaika:  Msujudieni Aadam.  Wakasujudu isipokuwa Ibliys,  alikuwa miongoni mwa majini, akaasi Amri ya Rabb wake.  Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui?  Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu!”.  [Al-Kahf: 50]  

 

Ibliys hakuwa katika Malaika, bali yeye anatokana na majini.

 

Al-Hasan Al-Baswriy amesema:  “Ibliys hakuwa kamwe katika Malaika, bali asili yake ni majini kama alivyo Aadam ambaye ni asili ya wanadamu”.

 

‘Abdulrahmaan bin Zayd bin Aslam amesema:  “Ibliys ndiye baba wa majini kama alivyo Aadam ambaye ni baba wa wanadamu”. 

 

Ibn Shihaab amesema:  “Ibliys ni baba wa majini kama ilivyo kwa Aadam ambaye ni baba wa wanadamu.  Ibliys ametokana na majini, naye ndiye baba yao.  Na hili liko wazi kwa wote kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا "

 

Na pindi Tulipowaambia Malaika:  Msujudieni Aadam.  Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini, akaasi Amri ya Rabb wake.  Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami, na hali wao kwenu ni maadui?!  Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu!”.  [Al-Kahf: 50]

 

Az-Zajjaaj amesema:  “Kundi la mabingwa wa lugha wamesema:  “Ibliys hakuwa kamwe katika Malaika.  Na dalili ya hilo ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

“Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini”.  Wakaulizwa:  Imewezekana vipi akatolewa nje ya kundi lao?  Wakajibu kwamba Malaika pamoja na yeye waliamuriwa kusujudu, na dalili ya kwamba aliamuriwa pamoja nao kusujudu ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ "

 

“Na pale Tulipowaambia Malaika:  Msujudieni Aadam.  Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri”.  [Al-Baqarah: 34]

 

Hivyo basi, yeye hakukataa isipokuwa kwamba aliamrishwa, akagoma.  Kauli hii sisi ndio tunaichagua”.

 

Ibn Hazm kasema:  “Baadhi ya watu wanadai kwamba Ibliys alikuwa ni Malaika, kisha akaasi.  Hili haliwezekani kwa Utakasifu wa Allaah Ambaye Amelikadhibisha hilo katika Kauli Yake:

 

إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ

 

“Isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini”.

 

Na Kauli Yake pia:

 

أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي

 

.”Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami”,  na Malaika hawana kizazi.  Kadhalika, Allaah Ameeleza kwamba Amemuumba Ibliys kutokana na moto wenye mwako mkali huku Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akitueleza kwamba Malaika wameumbwa kutokana na nuru aliposema:

 

"خُلِقَتِ المَلائِكةُ من نُور"

 

“Malaika wameumbwa kutokana na nuru”. 

 

Na nuru bila shaka si moto, hivyo ni dhahiri kabisa kwamba majini si Malaika.  Aidha, Malaika wote ni viumbe wema waliokirimiwa na Allaah kama inavyoeleza Qur-aan, wakati ambapo katika majini na wanadamu kuna waliolaumiwa na kuna waliosifiwa.

 

 

 

Share