01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
01: Kufunga Ndoa:
Fungamano la ndoa ni sawa na mikataba mingineyo ambayo makubaliano yake yanakuwa juu ya msingi wa utashi wa watu wawili wanaoingia mkataba kwa ridhaa yao. Ridhaa na utashi ni vitu vya ndani ya moyo ambavyo hakuna binadamu anayeweza kuviona au kuvijua, na kwa ajili hiyo, imekuwa ni lazima kitoke kwa wawili wanaoingia mkataba chenye kuonyesha kukubali kwao mkataba na kuuwafiki.
Kwa upande wa wanandoa, kinachoonyesha kukubali na kuwafiki kwao ni matamshi yanayojulikana kama "الإِيْجَابُ" (Al-Iyjaab) na "القَبُوْلُ" (Al-Qabuwl). Matamshi haya ndio nguzo mbili za kufungika ndoa.
Al-Iyjaab "الإيجاب" , ni tamshi toka kwa walii wa mwanamke au mwakilishi wake ambapo humwambia mwenye kuoa: “Nimekuozesha binti yangu fulani”.
Ama Al-Qabuwl "القَبُوْلُ", hili ni tamshi toka kwa anayeoa au anayemwakilisha ambapo humjibu walii kwa kusema: “Nimekubali”.
Matamshi haya mawili ndiyo ambayo kwayo ndoa inafungika.