02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kufungika ‘Aqdi Ya Ndoa: Masharti Ya Tamko La ‘Aqdi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

عَقْدُ الزَّوَاجِ

 

Kufunga Ndoa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

02: Masharti Ya Kufungika ‘Aqdi Ya Ndoa:  Masharti Ya Tamko La ‘Aqdi:

 

Sharti la kwanza:

 

Tamko la “Iyjaab” na “Qabuwl” ni lazima  libebe maana ya ndoa kama vile

  "أَنْكَحْتُ" au"زَوَّجْتُ"  au "مَلَّكْتُ" au "وَهَبْتُ" na mfano wa hivyo, na hili ni kwa mujibu wa ada.  Na si sharti muundo uwe kwa tamko la kuozesha, kwa kuwa linalozingatiwa ni makusudio na maana, na si tamko.  Na hii ndio kauli iliyo sahihi zaidi ya ‘Ulamaa, na pia ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na Maalik, na chaguo pia la Ibn Taymiyah.

 

Linalotilia nguvu hili ni lile lililothibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha mtu fulani mwanamke akamwambia:

 

"فَقَدْ مَلَّكْتُكَهَا بِمَا مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ"

 

“Basi nimekumilikisha (nimekuozesha) kwa kiasi ulichohifadhi katika Qur-aan”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (1425) na Muslim (5871)]

 

Ama ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali, wao wanaona kwamba ndoa haiswihi isipokuwa kwa tamko lililonyambulika kutokana na kuozesha "التَّزْوِيْجُ" au"الإِنْكَاحُ"  , kwa kuwa hakuna tamshi jingine lolote lililokuja ndani ya Qur-aan zaidi ya haya mawili.  Hivyo ni lazima kuyatumia ki‘ibada, kwani nikaah ni ‘ibada, na matamshi au adhkaar huwa yanachukuliwa toka ndani ya shariy’ah, na si vinginevyo.

 

Kufunga Ndoa Kwa Lugha Nyingine Isiyo Kiarabu:

 

Ikiwa wafungao ndoa au mmoja wao hafahamu Kiarabu, basi itajuzu kufunga kwa lugha inayofahamika.  Na ikiwa wanaifahamu vizuri lugha ya Kiarabu na wanaweza kufungishiwa kwayo ndoa, basi hapo haitojuzu kufungwa ndoa kwa lugha nyingineyo.  Hii ni kauli ya ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali. 

 

Lakini lililo sahihi, ni kwamba inajuzu.  Sheikh wa Uislamu amesema:  “Kulazimisha tamko la Kiarabu katika kufungisha ndoa kuko mbali kabisa na misingi ya kisharia, kwa kuwa ndoa inaswihi kwa Muislamu na kwa kafiri.  Ndoa ni sawa na kuacha huru mtumwa au kutoa sadaka.  Na kama ilivyo au ilivyozoeleka, mkataba wowote hauna lazima ya kuwa na tamshi, si kwa Kiarabu au kwa lugha nyingine yoyote.  Vile vile sadaka, au waqfu, au tunu, haya yote hayana lazima kutamkiwa kwa Kiarabu kwa mujibu wa Ijmaa ya ‘Ulamaa.  Isitoshe, ikiwa asiye Mwarabu atajifundisha papo kwa hapo Kiarabu, anaweza asifahamu makusudio ya tamshi hilo kama anavyolifahamu katika lugha yake anayoijua.

 

Ndoa Haifungiki Kwa Ishara Isipokuwa Kwa Bubu Tu:

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa kinyume na ‘Ulamaa wa Kimaalik, wamekubaliana kwamba mwenye uwezo wa kutamka na badala yake akatumia ishara, basi ishara yake hiyo haizingatiwi katika kufunga ‘aqdi ya ndoa.  Ama kwa bubu, ishara yake iliyozoeleka na kufahamika  inakubalika kisharia.  Lakini hapo hapo wamekhitilafiana katika swali lisemalo:  Je, utumiaji wa ishara ni sharti uende sambamba na kutoweza bubu kuandika?  Ilivyo sahihi ni kwamba ni sharti, kwa maana ikiwa anaweza kuandika, basi ishara haitozingatiwa.

 

Sharti la pili:

 

Muundo wa tamshi ni lazima ubebe maana ya upapo kwa hapo.  Ikiwa utabeba maana ya wakati ujao au wakati maalum, basi ‘aqdi ya ndoa haifungiki.  Ni kama kusema:  “Ikifika tarehe mosi ya mwezi, basi nitakuwa nimekuozesha”, au “Nimekuozesha binti yangu wakati atakapokuwa amefaulu mtihani”, kwa kuwa hili linakuwa limefungamanishwa na sharti ambalo halipo kwa wakati uliopo.  Lakini kama atafungamanisha na sharti ambalo limeshapatikana, basi ndoa itafungika.

 

Sharti la tatu:

 

“Qabuwl” na “Iyjaab” zikubaliane kwa pande zote.  Hili ndilo ambalo ‘Ulamaa wa Fiqh wameafikiana.  Hivyo basi, ikiwa qabuwl itatofautiana na iyjaab kwa jambo, basi ndoa haitoswihi.  Ikiwa walii atasema kwa mfano:  “Nimekuozesha binti yangu Fatmah kwa mahari ya shilingi laki moja”, na mwoaji akasema:  “Nimekubali kumwoa binti yako ‘Aaishah kwa mahari ya shilingi elfu 50”, basi ndoa haitoswihi”.

 

Sharti la nne:

 

Qabuwl na Iyjaab ziungane.  Kwa maana kwamba kikao cha kufungisha ndoa ni lazima kiwe kimoja, na qabuwl na iyjaab zitamkwe kwa pamoja ndani ya kikao hicho kimoja.

 

Lakini pamoja na hivyo, si sharti kutamkwa qabuwl moja kwa moja baada ya iyjaab.  Muda kupita hakuna neno madhali qabuwl itatamkwa ndani ya kikao kimoja.  Upapo kwa hapo haukushurutishwa na Jumhuwr ya ‘Ulamaa.  [Al-Badaai’u (5/137), Mawaahibul Jaliyl (4/241) na Kash-shaaful Qinaa (3/147)]

 

Faida:

 

Fuqahaa walishurutisha siku za nyuma kikao kuwa kimoja kutokana na uduni wa njia za mawasiliano.  Ama enzi yetu ya leo, bila shaka teknolojia ya mawasiliano imepiga hatua kubwa.  Tuna simu za viganjani na mfano wake ambazo zinaweza kutuletea tukio lolote, toka popote lilipo, na kwa wakati huo huo.  Watu wote wanaweza kulishuhudia toka kona yoyote ya dunia.  Hivyo basi, hakuna kizuizi kufunga ndoa hata kama vikao viko sehemu mbili tofauti, muhimu ni upapo kwa papo uwepo wa “qabuwl” na “iyjaab”.  Isitoshe, ni lazima kila mmoja wa wafungaji ndoa ahakikishe utambulisho wa mwingine na usiwepo udanganyifu.

 

Sharti la tano:

 

Mtamkaji wa “iyjaab” asilirejeshe tamko lake kabla ya upande wa pili wa “qabuwl” kukubali.  Jumhuwr kinyume na Maalik wanasema kwamba “iyjaab” si lazima ipite, na mtamkaji wake anaweza kulirejesha tamko lake kabla ya upande wa pili kukubali.  Akilirejea tamko lake, basi ndoa haifungiki.

 

Kadhalika, ikiwa mmoja wa wafungao ndoa (walii au mwoaji) atakufa baada ya “iyjaab” na kabla ya “qabuwl” kutamkwa, basi ndoa inakuwa haijafungika.

 

 

 

Share