03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Yanayowahusu Walii Na Mwoaji
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
03: Masharti Yanayowahusu Walii Na Mwoaji:
La kwanza:
Ni lazima kila mmoja wao awe na vigezo vya kumwezesha kufanikisha ‘aqd ya ndoa.
Vigezo vyenyewe ni awe amebaleghe, mwenye akili na mtambuzi. Ama mtoto mdogo ambaye bado hajabaleghe lakini mtambuzi, kama walii wake atamruhusu, basi ndoa yake itaswihi.
La pili:
Wawe na haki na mamlaka wao wenyewe ya kuzindua ‘aqd:
Hii ni kwa aliyebaleghe, mwenye akili na anayejitambua, huyu ana haki na mamlaka ya kufunga ndoa mwenyewe au kumwakilisha mwingine amfungie. Kadhalika walii, yeye kapewa haki na sharia ya kusimamia ndoa. Ama mtu kando aliyejiingiza bila idhini yake, huyo ‘aqd yake haishwihi.
La tatu:
Wote waridhie kwa hiari yao.
Kama ndoa itafungwa bila ya ridhaa yao au kwa ridhaa ya mmoja wao tu, basi haitoswihi.
La nne:
Kila mmoja wao ayasikie maneno ya mwingine na ayafahamu.
La tano:
Kila mmoja kati ya wanandoa watarajiwa (bwana harusi na bibi harusi) ajulikane na atambulike. Ikiwa walii ana binti zaidi ya mmoja na akasema: “Nimekuozesha mmoja ya binti zangu” bila kumtaja jina, hapo ndoa haitoswihi.
La sita:
Kusiwepo kati ya wanandoa watarajiwa sababu ya kuharamisha kuoana. Katika milango ya nyuma, wanawake walioharamishwa kuwaoa wametajwa.