04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa:Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Kwanza: (a) Idhini Ya Walii Wa Mwanamke
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
04: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (a) Idhini ya walii wa mwanamke:
Haya ni masharti ambayo kuswihi ‘aqdi ya ndoa kunasimamia juu yake pamoja na athari zake, na inabatilika kwa kukosekana moja katika masharti haya. La kwanza ni idhini ya walii wa mwanamke.
Walii ni msimamizi wa mwanamke katika zoezi la kufunga ndoa. Jumhuwr ya ‘Ulamaa wakiwemo ‘Umar, ‘Aliy, Ibn Mas-‘uwd, Abu Hurayrah, ‘Aaishah, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, Abu ‘Ubayd, Ath-Thawr na Ahlu Adh-Dhwaahir, wanasema kwamba walii ni sharti ya kuswihi kwa ‘aqdi. Ikiwa mwanamke atajiozesha mwenyewe, basi ndoa yake ni batili. Dalili zao ni hizi zifuatazo:
(a) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ"
“Na waozesheni wajane miongoni mwenu”. [An-Nuwr: 32]
Hapa Allaah Ta’aalaa Ameelekeza agizo la kuozesha wajane kwa wanaume. Lau kama amri ya kuozesha inawahusu wanawake, basi Allaah Asingeliwaamuru wanaume.
(b) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَلَا تُنكِحُوا الْمُشْرِكِينَ حَتَّىٰ يُؤْمِنُوا"
“Na wala msiwaozeshe (wanawake wa Kiislamu) wanaume washirikina mpaka waamini”. [Al-Baqarah: 221)]
(c) Mzee kikongwe alimwambia Muwsaa (‘alayhis salaam):
"إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ"
“Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili”. [Al-Qaswas: 27]
(d) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُم بِالْمَعْرُوفِ"
“Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali) ikiwa wameridhiana baina yao kwa mujibu wa ada”. [Al-Baqarah: 232]
Hapa Allaah Ta’aalaa Amewakataza Mawalii wasiwazuie wanawake kurudi kwa waume zao. Na hii ni dalili tosha ya kumzingatia walii, na kama si hivyo, basi kuambiwa asimzuie kusingelikuwa na maana yoyote. Isitoshe, kama angelikuwa na haki ya kujiozesha mwenyewe, basi asingelimhitajia walii wake.
(e) Kauli Yake Ta’aalaa:
"فَانكِحُوهُنَّ بِإِذْنِ أَهْلِهِنَّ"
“Basi waoeni kwa idhini ya watu wao”. [An-Nisaa: 25]
Hapa imeshurutishwa idhini ya walii wa msichana ili ndoa iswihi, na inaonesha kwamba hawezi kujiozesha mwenyewe.
(f) Kauli Yake Ta’aalaa:
"الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ"
“Wanaume ndio wasimamizi wa wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine.” [An-Nisaa: 34]
(g) Bibi ‘Aaishah akiizungumzia Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَمَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ فِي يَتَامَى النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا تُؤْتُونَهُنَّ مَا كُتِبَ لَهُنَّ وَتَرْغَبُونَ أَن تَنكِحُوهُنَّ"
“Na (hukmu ya) yale mnayosomewa katika Kitabu kuhusu mayatima wanawake ambao hamuwapi (mahari) waliyoandikiwa nanyi mna raghba ya kuwaoa”. [An-Nisaa: (127)]
…anasema:
"هذا في اليَتِيمَةِ الَّتي تَكُونُ عِنْدَ الرَّجُلِ، لَعَلَّهَا أنْ تَكُونَ شَرِيكَتَهُ في مَالِهِ، وهو أوْلَى بهَا، فَيَرْغَبُ عَنْهَا أنْ يَنْكِحَهَا، فَيَعْضُلَهَا لِمَالِهَا، ولَا يُنْكِحَهَا غَيْرَهُ؛ كَرَاهيةَ أنْ يَشْرَكَهُ أحَدٌ في مَالِهَا"
“Hili linahusiana na binti yatima anayelelewa na mwanaume. Binti huyu anaweza kuwa na mali akaichanganya na ya mwanaume huyo na kuwa mshirika wake kiubia. Na yeye (kwa kuwa ni mlezi wake) anastahiki zaidi kuwa na ubia huo na binti. Lakini ikaja kutokea asimpende penzi la kumwoa na hapo akamzuia kuolewa na mtu mwingine kwa ajili ya mali yake kwa kuhofia kwamba mtu huyo atafaidika na mali ya binti”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5128)]
Ama kipande cha aayah kinachosema:
"وَتَرْغَبُونَ أَن تَنكِحُوهُنَّ"
“nanyi mna raghba ya kuwaoa”, hiki kinahusiana na aayah ya tatu ya Suwrat An-Nisaa ambapo Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تُقْسِطُوا فِي الْيَتَامَىٰ فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ"
“Na mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu kwa mayatima; basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne”.
Ni kwamba ‘Taabi’iy ‘Urwah bin Az-Zubayr alimuuliza khalati yake Mama wa Waumini Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) kuhusiana na aayah hii, naye akamwambia: “Ee mtoto wa dada yangu, aayah hii iliteremka kuhusiana na binti yatima anayelelewa na mtu, na mali (yake na ya mlezi wake) ikawa ya ushirika baina yao, na mlezi huyo akaifanyia biashara. Halafu ikatokea akavutiwa na mali yake na uzuri wake na akataka amuoe, lakini kwa mahari chache kulinganisha na wanawake wengine. Na hapo ndipo walipokatazwa kuwaoa ila kama watawapa mahari wanayostahiki kama wanavyostahiki wanawake wengine wote. Na kama hawataki hilo, basi waoe wanawake wengineo; wa pili, wa tatu na wanne, kwa hao bila shaka watalipa mahari kamili, na wawaache mabinti hao mayatima (lakini pia wasiwazuie kuolewa na wengineo)”.
Na dalili zilizo wazi zaidi kuliko zote zilizotangulia, ni hizi zifuatazo:
(a) Hadiyth ya Abu Muwsaa kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا نِكَاحَ إِلَّا بِوَلِيٍّ"
“Hakuna ndoa bila walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2085), At-Tirmidhiy (1101), Ibn Maajah (1879), Ahmad (4/394) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (6/234)]
(b) Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَيُّمَا امْرَأَةٍ نَكَحَتْ بِغَيْرِ إِذْنِ موَالِيْهَا فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ وَلَهَا ْمَهْرُهَا بِمَا أَصَابَ مِنْهَا، فَإِنِ اشْتَجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ من لَا ولي لَهُ ".
“Mwanamke yeyote ambaye ataolewa bila idhini ya mawalii wake, basi ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili. Na mahari yake atapewa kama mume atakuwa amemuingilia. Na kama mawalii watazozana, basi kiongozi (Kadhi) ni walii kwa asiyekuwa na walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2083), At-Tirmidhiy (1101), Ibn Maajah (1879) na Ahmad (6/156)]
(c) Maana hii imethibiti kutokana na kauli za ‘Umar bin Al-Khattwwaab, ’Aliy bin Abiy Twaalib na Ibn ‘Abbaas. [Angalia Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/327-328)]
(e) Toka kwa Abu Hurayrah, amesema:
"لا تُنْكِحُ الْمَرْأَةُ نَفْسَهَا، فَإِنَّ الزَّانِيَةَ تُنْكِحُ نَفْسَهَا"
“Mwanamke hajiozeshi mwenyewe, bali mzinifu ndiye anayejiozesha mwenyewe”. [Isnadi yake ni swahiyh. Imechakatwa na Abdul Razzaaq (6/200) na Ibn Abiy Shaybah (4/135)]
Wakati huo huo, kinyume na hayo, Abu Haniyfah anasema kwamba mwanamke aliye huru, mwenye akili zake timamu na aliyebaleghe, hashurutishiwi kuwepo walii wake ili ndoa yake iswihi, anayeshurutishiwa hilo ni msichana mdogo tu!! Na hoja yake ni haya yafuatayo:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
" فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ"
“Na akimtaliki (mara ya tatu), basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine”. [Al-Baqarah: (230)]
Amesema: “Ndoa imetegemezewa kwao, na kwa hivyo basi, ni dalili kwamba ndoa inaswihi kwa matamshi yao bila sharti ya walii”.
2- Kauli Yake Ta’aalaa:
" وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ"
“Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali)”. [Al-Baqarah: (232)]
Amesema: “Utohoaji dalili kwa aayah hii ni kwa njia mbili:
1- Allaah Ametegemeza ndoa kwao wanawake.
2- Inawezekana katazo la kuwazuia kuolewa kwenye aayah linawahusu waume. Aayah imewakataza wasiwazuie wake zao waliowataliki kuolewa na mwanaume yeyote wamtakaye baada ya kumalizika eda zao.
Ninasema: “Sababu ya kuteremka aayah hii imeshaelezwa nyuma, na sababu hiyo inaradd taawiyl hii”.
3- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mwanamke asiye na mume (ayyim) ana haki zaidi ya kujiamulia kuliko walii wake, na msichana bikra hutakwa idhini kwa nafsi yake mwenyewe, na idhini yake ni kunyamaza.”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim]
"الأَيِّمُ"] kiasili, ni mwanamke asiye na mume, ni sawa akiwa bikra au bila bikra, ametalikiwa, au amefiwa na mumewe.
"الأَيِّمُ" pia ina maana ya mwanaume asiye na mke. Inasemwa: "رَجُلٌ أَيِّمٌ" mwanaume asiye na mke, na kwa mwanamke inasemwa: "امْرَأَةٌ أَيِّمَةٌ" mwanamke asiye na mume. Na Allaah Anaposema:
"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ "
“Na waozesheni wajane miongoni mwenu”, hapa inakusudiwa wanaume wasio na wake na wanawake wasio na waume.]
Faida:
1- Kama ilivyotangulia, Abu Haniyfah amejuzisha mwanamke kujiozesha mwenyewe, lakini pamoja na hivyo, amempa haki walii kuvunja ndoa kama mume haendani kwa kiwango na mwanamke!!
2- Mwanamke hamwozeshi mwanamke mwenzake, na wala ndoa haifungiki kwa matamshi yake. Kwa kuwa kiasili, mwanamke hafai kujiozesha mwenyewe, na kwa hivyo kumwozesha mwenzake ndio haifai kabisa.