05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (b) Walii Hana Haki Ya Kumlazimisha Mwanamke Aliyebaleghe Kuolewa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
05: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (b) Walii Hana Haki Ya Kumlazimisha Mwanamke Aliyebaleghe Kuolewa:
(a) Kumlazimisha aliyewahi kuolewa (au asiye bikra “thayyib”):
Haijuzu kumwozesha “thayyib” na aliye baleghe na bila idhini yake, hana ruhusa baba yake wala mwingine yeyote. Na hii ni kwa itifaki ya Waislamu wote. Zifuatazo ni dalili za kuthibitisha hili:
1- Hadiyth ya Khansaa bint Khidhaam Al-Answaariyyah:
"أنَّ أبَاهَا زَوَّجَهَا وهْيَ ثَيِّبٌ، فَكَرِهَتْ ذلكَ، فأتَتْ رَسولَ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فَرَدَّ نِكَاحَهَا"
“Kwamba baba yake alimwozesha baada ya kuwa aliwahi kuolewa (thayyib), naye hakufurahishwa na hilo, akaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (kumshtakia), na Rasuli akaivunja ndoa”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5138), Abu Daawuwd (2101), An-Nasaaiy (6/86) na Ibn Maajah (1873)].
2- Abu Hurayrah: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا تُنْكَحُ الْأَيِّمُ حَتَّى تُسْتَأْمَرَ، وَلَا تُنْكَحُ الْبِكْرُ حَتَّى تُسْتَأْذَنَ . قَالُوا: يَا رَسُول الله، وَكَيف إِذْنهَا؟ قَالَ: أَنْ تَسْكُتَ"
“Mwanamke asiye na mume (ayyim) haolewi mpaka atakwe shauri lake, na bikra haolewi mpaka atakwe idhini yake. Wakauliza: Idhini yake inakuwaje? Akasema: Akinyamaza”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5136) na Muslim (1419)]
3- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَيْسَ لِلْوَلِيِّ مَعَ الثَّيِّبِ أَمْرٌ وَالْيَتِيمَةُ تُسْتَأْمَرُ فَصَمْتُهَا إِقْرَارُهَا"
“Walii hana lake jambo kwa aliyewahi kuolewa (thayyib), na yatima hutakwa shauri lake, na akinyamaza ndio kakubali”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2100) na wengineo]
Faida Mbili:
Ya kwanza: Msichana ambaye ubikira wake umeondoka kutokana na zinaa, anakuwa katika ndoa ni sawa na mwanamke aliyekwishawahi kuolewa (thayyib). Haitojuzu kwa walii wake kumlazimisha kuolewa. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah. Ama Abu Haniyfah mwenyewe pamoja na Maalik, wao wanasema kwamba mwanamke huyo ni sawa na bikra.
Na kama ubikira wake utaondoka bila kuingiliwa (kama kwa kuruka, au kwa kidole, au kwa kubakwa, au mfano wa hayo), basi atazingatiwa bikra kwa mujibu wa Maimamu wanne. [Majmuw’ul Fataawaa (32/29). Angalia pia Fat-hul Qadiyr (3/270), Rawdhwat At-Twaalibiyna (7/54), na Al-Mughniy (6)]
Ya pili: Kama walii atamwozesha aliyewahi kuolewa bila ya idhini yake, kisha yeye mwenyewe mwanamke akapasisha fungisho la ndoa hiyo, basi ndoa ni sahihi, haihitajii kufungwa tena upya. Hii ni rai ya ‘Ulamaa walio wengi akiwemo Abu Haniyfah, Maalik na riwaayah toka kwa Ahmad.
Lakini ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy wanaona kwamba ndoa iliyofungwa ni batili, na ni lazima ifungwe tena upya. [Majmuw’u Fataawaa Shaykhil Islaam (32/29)]