06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa:Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (c) Kumlazimisha Bikra Aliye Baleghe

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

عَقْدُ الزَّوَاجِ

 

Kufunga Ndoa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

06:  Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza:  (c) Kumlazimisha Bikra Aliye Baleghe:

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na bikra aliye baleghe.  Je, walii wake anaweza kumlazimisha kuolewa?  Wamekhitilafiana hili katika kauli mbili.  Kauli iliyo sahihi zaidi ni kuwa haijuzu kwa walii wake kumlazimisha.  Ni kauli ya Abu Haniyfah, riwaayah toka kwa Ahmad, Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy, Abu ‘Ubayd, Abu Thawr, na Ibnul Mundhir.  Sheikh wa Uislamu ameikhitari.  Dalili zao ni:

 

1-  Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: 

 

"إِنَّ جَارِيَةً بِكْرًا أَتَتْ رَسُولَ اللَّهِ َصَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَذَكَرَتْ لَهُ أَنَّ أَبَاهَا زَوَّجهَا وَهِي كَارِهًة، فَخَيَّرَهَا النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم"

 

“Kwamba msichana bikra alimjia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamweleza kwamba baba yake amemwozesha bila ridhaa yake, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamchaguza (kati ya kuivunja ndoa au kuendelea nayo)”.  [Hadiyth Hasan Lishawaahidih.  Imechakatwa na Abu Daawuwd (2099) na Ibn Maajah (1875)]

 

2-  Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 

 

"وَلَا تُنْكَحُ الْبِكْرُ حَتَّى تُسْتَأْذَنَ"

 

“Na bikra haolewi mpaka atakwe idhini yake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5136) na Muslim (1419)]

 

3-  Kwa vile walii kujiamulia aonavyo yeye kuhusiana na ndoa ya binti yake, ni sawa na kujiamulia aonavyo katika mali ya binti huyo.  Sasa ikiwa walii huyu haruhusiwi kuamua aonavyo katika mali ya binti yake ambaye ni mwelewa na mtambuzi isipokuwa kwa idhini yake, basi vipi itajuzu kumwamulia ndoa ambayo ni jambo zito bila ridhaa yake ilhali binti anajitambua?  [Majmuw’ul Fataawaa (32/39)]

 

4-  Kumwozesha bila ridhaa yake ni kinyume na misingi ya kishariy’ah na kiakili.  Allaah Ta’aalaa Hajamruhusu walii wake kumlazimisha kuuza au kukodisha kwa mfano ila kwa idhini yake, au hata chakula asichokipenda, au kinywaji au kivazi, basi vipi atamlazimisha kuolewa, halafu kuingiliwa na kuishi pamoja na mtu asiyemtaka au kumpenda?  Allaah Ta’aalaa Amejenga mapenzi na huruma kati ya wanandoa wawili, basi vipi hilo litapatikana ikiwa binti hayuko tayari kuishi na mwanaume asiyemtaka?!  [As-Saabiq:  (32/25)]

 

5-  Mwanamke kama amemchukia mume, basi ameruhusiwa na sharia kuachana naye.  Sasa vipi itajuzu kwa walii kumwozesha mtu ambaye kabla ya ndoa ashamchukia?

 

Faida:

 

Suala hili ni kama walii atakuwa ni baba au babu.  Na ikiwa si hawa wawili kama kaka yake au ami yake, Sheikh wa Uislamu amenukuu Ijma’a ya Waislamu kwamba bikra aliyebaleghe hakuna mwenye ruksa ya kumwozesha bila idhini yake isipokuwa baba yake au babu yake tu (wengine hawana mamlaka hayo).

 

 

Share